MKOA WA PWANI WATATHMINI MALEZI YA AWALI YA MTOTO: ZAIDI YA VITUO 400 VYA DCCA VIMESAJILIWA


Na Julieth Ngarabali, PWANI.

Mkoa wa Pwani umefanya tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026, kinacholenga kuimarisha ustawi na huduma kwa watoto wenye umri wa miaka 0 mpaka 8.

Kwenye tathmini hiyo pamoja na mambo mbalimbali yaliyowasilishwa imeelezwa jumla ya vituo 858 vya kulelea watoto wadogo mchana (DCC) vimeainishwa, ambapo vituo 477 tayari vimesajiliwa na vinahudumia watoto 19,478—sawa na asilimia 56 ya vituo vyote vilivyotambuliwa kimkoa.


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Lidya Mafole amesema pia kuna vituo saba vya malezi ya jamii (Community ECD) vilivyoanzishwa na shirika la BRAC tangu mwaka 2025 ambavyo mchakato wa usajili wake unaendelea.

Bi. Lidya Mafole Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani

Mafole amebainisha kuwa katika kipindi hicho, vikao vya tathmini vimefanyika katika Halmashauri zote tisa za mkoa huo na kwamba programu hiyo inalenga kujenga uwezo wa watoa huduma, kuimarisha mifumo ya lishe na afya, pamoja na kuwajengea uwezo wazazi na jamii katika kutoa malezi bora na salama.

Awali Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la ya Anjita Mkoa wa Pwani linalojihusisha na masuala ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto, Janeth Malela ametangaza mpango wa miaka mitatu wa kujenga vituo vya kijamii vya kulelea watoto mchana, ukianzia katika Halmashauri za Chalinze na Mkuranga kabla ya kusambaa Halmashauri ya Kibaha  na nyinginezo.

Janeth alifafanua mradi huo utatoa huduma jumuishi zikiwemo elimu ya awali kupitia michezo, ufuatiliaji wa afya na lishe, pamoja na kuweka mazingira salama yatakayowawezesha kina mama na vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi wakijua watoto wao wapo salama.

Bi. Janeth Malela Mkurugenzi wa Shirika la Anjita 


Kwa upande wao baadhi ya washiriki wametoa Wito  kwa wamiliki wa vituo zaidi ya  300 vilivyosalia na ambavyo havijasajiliwa Mkoani Pwani kukamilisha taratibu za usajili.

Wadau na Watekelezaji wa PJT - MMMAM Pwani


Wamepongeza kuwa jamiii ikumbuke kuwa  Usajili sio tu takwa la kisheria, bali ni hakikisho la usalama, afya, na ubora wa mazingira anayokulia mtoto.

Kikao kazi  hicho kilichofanyika , Agosti 11, 2026, mjini Kibaha na  kimekutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Waganga Wakuu wa Halmashauri, Waratibu wa Afya ya Mama na Mtoto, Makatibu wa Afya, Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na wawakilishi wa Taasisi ya Anjita.



Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

MWENYEKITI KITONGOJI CHA KWAKIBOSHA MAPINGA AWAPIGA MSASA VIJANA 500 KULINDA AMANI YA TAIFA.

WIZARA YA AFYA YASEMA:UGONJWA WA SIKOSELI SIO WA KUROGWA, YAHAMASISHA JAMII KWENDA KUPIMA VINASABA

TAIFA GAS TANZANIA YAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA