TAKUKURU PWANI YAOKOA ZAIDI YA SH. MILIONI 385 ZA KIJIJI CHA MSUFINI MKURANGA.
Na Gustaphu Haule,Pwani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh.milioni 385 zilizopotea kupitia akaunti feki ya Kijiji cha Msufini Kidete Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Domina Mukama, ametoa taarifa hiyo leo Mei 29, 2025 katika mkutano wake na Waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha Januari- Machi 2025.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Domina Mukama akizungumza na Waandishi wa habari Mei 29,2025 Mjini Kibaha ikiwa sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha Januari-Machi 2025
Mukama, amesema kuwa katika kipindi hicho Takukuru Mkoa wa Pwani ilifanya uzuiaji wa vitendo vya rushwa ambapo moja ya vitendo hivyo ni kufanikiwa kuokoa mapato ya asilimia 10 ya mauzo ya ardhi ya Halmashauri ya Kijiji cha Msufini Kidete Wilayani Mkuranga.
Mukama, amesema kuwa fedha hizo ambazo ziliwekwa kwenye akaunti feki ya Kijiji hicho iliyoghushiwa na Mwanasheria wa kampuni iliyouziwa eneo la Kijiji ambayo ni Brilliant Sanitary Ware Company Limited.
"Halmashauri ya Kijiji ilitakiwa kulipwa zaidi ya Sh. Milioni 385 kama asilimia 10 ya mauzo ambapo fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti feki yenye jina kama la akaunti ya Kijiji iliyowasilishwa na Mwanasheria wa kampuni hiyo ", amesema Mukama.
Mukama, ameongeza kuwa kampuni ya Brilliant Sanitary Ware Company Limited ilifanya malipo ya kiasi cha fedha hizo wakiamini kuwa wanalipa ushuru wa Kijiji cha Msufini katika akaunti halali ya Kijiji kumbe ilikuwa akaunti feki iliyotengenezwa na Mwanasheria huyo.
Amesema kuwa, baada ya kufanyika malipo hayo Mwanasheria huyo alizitoa fedha zote na kuzifanyia matumizi binafsi na hivyo kukifanya Kijiji kubaki na sintofahamu.
Mukama, amesema baada ya ufuatiliaji Takukuru imefanikiwa kurejesha fedha zote Serikalini kupitia Halmashauri ya Kijiji cha Msufini na tayari fedha hizo zimepangiwa matumizi ya kujenga jumla madarasa mawili ya Shule ya Sekondari Mbezi Gogoni na madarasa mawili Shule ya Msingi Msufini.
Kuhusu uchambuzi wa mifumo, Mukama amesema kuwa katika kipindi hicho ofisi ilifanya chambuzi za mifumo 14 ikiwa pamoja na eneo la makadirio ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Mafia, na kituo cha utalii Kazimzumbwi huku katika uchambuzi wa mfumo wa usambazaji maji uliofanyika kuna mapungufu yalibainika na hatua zilichukuliwa.
Aidha, Mukama amesema kuwa katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo Takukuru Mkoa wa Pwani imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 338 yenye thamani zaidi ya bilioni 18 na utekelezaji wake unaridhisha.
Amesema, Takukuru Mkoa wa Pwani imeendelea kufanya uelimishaji wa Umma na kwamba katika kipindi hicho imefanikiwa kuwafikia Wananchi wa makundi mbalimbali ili waweze kuiunga mkono Serikali katika kuzuia vitendo vya rushwa kwa kupitia semina 67, mikutano ya hadhara 72, vipindi vya redio 5, pamoja na uimarishaji Klabu za wapinga rushwa 130.
Pia, amesema kesi 10 zimeamuliwa ambapo Jamhuri imeshinda kesi zote na jumla ya kesi 23 zinaendelea Mahakamani.
Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 Mukama amesema kuwa Takukuru Mkoa wa Pwani tumejipanga Kuzuia na Kupambana na vitendo vya rushwa katika uchaguzi mkuu .
Amesema, kwasasa inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi kwa kuwafikia wadau wote ambao ni vyama vya Siasa, wasimamizi wa uchaguzi, Wanahabari, Wananchi na jamii nzima kiujumla.
Hatahivyo, Mukama amewaasa Wananchi kufuata Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuwa salama na kuepuka migogoro yenye kuleta viashiria vya rushwa.
Comments
Post a Comment