TANROADS YATOA UFAFANUZI KUTOZWA FAINI GARI LA SIMBA LOGISTICS KITUO CHA MIZANI YA VIGWAZA MKOA WA PWANI



Na Gustaphu Haule Pwani 

WAKALA ya Barabara Tanzania ( TANROADS) imetoa ufafanuzi kuhusu gari la mizigo la kampuni ya Simba Logistics Limited lililozuiliwa katika kituo cha  Mizani ya Vigwaza Mkoani Pwani baada ya kupimwa na kukutwa limezidisha uzito.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage,amesema kuwa gari la Simba Logistics Limited lilifika katika kituo cha Mizani ya Vigwaza Machi 13 mwaka huu likitokea katika nchi jirani ya Zambia likiendeshwa na Pamela Bukumbi.

Meneja Wakala ya Barabara  (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage, akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari kuhusu kutozwa faini kwa gari la mizigo la Simba Logistics Machi 13,2025 katika kituo cha Mizani ya Vigwaza iliyopo Mkoani Pwani .

Amesema gari hilo lilikuwa limebeba mzigo wa Madini ya Shaba( Copper ) na baada ya kupimwa  lilibainika kuzidi uzito na hivyo kupaswa kulipa gharama ya Sh. 900,000 za Kitanzania.

Mwambage, amesema kuwa shughuli za upimaji na udhibiti wa uzito inafanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 na kwamba kilichofanyika ni utekelezaji wa majukumu kama yalivyoainishwa katika Sheria hiyo.



Amesema, kituo cha mizani ya Vigwaza hakina mashaka katika utendaji wake  kwakuwa vituo vya mizani hufanyiwa ukaguzi na marekebisho kila baada ya miezi mitatu na kituo cha Vigwaza kimefanyiwa ukaguzi huo Februari 15 mwaka huu.

Mwambage, amesema kuwa baada ya gari hilo kupimwa na kuzidi uzito lililipishwa faini ya Sh.900,000 kwa mujibu wa Sheria lakini alichokiona ni kwamba gari hilo lilikuwa linabadilika uzito wake tangu lilipotoka Nchini Zambia hadi linaingia nchini Tanzania.

Amesema kuwa,kilichofanyika badala ya gari hilo kutozwa faini malalamiko yametolewa sehemu nyingine na hivyo kuzua taharuki katika jamii na kwamba kilichopaswa ni kufuata utaratibu wa kutoa malalamiko sehemu sahihi.

Aidha, Mwambage ametoa wito kwa wasafirishaji kuwa ikitokea changamoto ya Mizani hatua ya kwanza ni kufikisha malalamiko kwa Mkuu wa Mizani na meneja wa Mkoa na endapo malalamiko hayo yana sura ya rushwa basi ni vyema kutumia namba za Takukuru zilizopo katika vituo hivyo.

Mwambage amesema kuwa  kama hiyo haitoshi, malalamiko hayo yanaweza kufikishwa kwa mtendaji Mkuu wa TANROADS na Wizara ya Ujenzi.

Mtaalam wa Kitengo cha Mizani TANROADS Makao Makuu Mhandisi Vicent Tarmo,amesema kuwa gari hilo lenye namba T .137 DLQ ni kati ya magari 819 yaliyopimwa Machi 13 katika upande wa Kaskazini wa Mizani ya Vigwaza lakini kati ya hayo magari Saba yalikuwa yamezidisha uzito ambapo magari mengine yalilipa na kuendelea na safari.

Mtaalam wa Kitengo cha Mizani kutoka TANROADS Makao Makuu Mhandisi Vicent Tarmo, akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari kuhusu Sheria ya udhibiti uzito wa magari yanayopimwa katika  Mizani mbalimbali hapa nchini,Tarmo amezungumza na Waandishi hao Machi 19 katika Mzani wa Vigwaza uliopo MKoani Pwani kufuatia malalamiko ya dereva wa gari la mizigo la Simba Logistics Limited lililotozwa faini Machi 13 mwaka huu.

Tarmo,amesema malalamiko ya dereva Pamela Bukumbi yalidai amebambikiwa uzito jambo ambalo sio sahihi kwakuwa Mizani ya Vigwaza imefungwa mitambo ya kisasa na hakuna mtu anayeweza kuandika risiti kwa mkono huku akisema mezani ya Vigwaza ni yakisasa (automated).

Amesema, TANROADS inasimamia Sheria ya udhibiti uzito wa magari ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 ambazo zinamtaka msafirishaji yeyote mwenye gari inayoanzia Tani tatu na nusu( 3.5) kupita katika vituo vya mizani kwa ajili ya kuhakiki uzito wa gari lake ili kuepusha uharibifu wa barabara.

Tarmo,amesema kutokana na hali hiyo gari lenye namba T 137 DLQ linalomilikiwa na Simba Logistics Limited lilifika katika kituo cha Mizani ya Vigwaza iliyopo Mkoani Pwani Machi 13 mwaka huu  likitokea katika nchi ya Demokrasia ya Kongo likiwa limebeba mzigo wa Madini ya Shaban( Copper).

Gari hilo likapimwa upande wa Mizani ya Vigwaza  Kaskazini na kubainika kuzidi uzito kwenye kundi la mitaimbo ( Difu) kwa zaidi ya kilo 1,450 nje ya uwezo ambao umewekwa kisheria. 

Tarmo amesema sambamba na hilo,kulikiwa na uzito wa jumla kwani gari hilo linatakiwa kubeba tani 48 lakini ilibeba tani 48.150 na hivyo kutakiwa kulipa tozo ya kuzidisha uzito kwa mujibu wa Sheria.

Amesema kuwa,Dereva baada ya kupewa tiketi yake ya kuzidisha mzigo na kuelekezwa kiwango anachotakiwa kulipa aligomea na kusema kuwa iweje ametoka kote huko halafu gari yake ije kuzidi uzito katika Mzani wa Vigwaza.

Tarmo ameongeza kuwa Siku ya Machi 13 , upande wa Kaskazini wa Mizani ya Vigwaza yalipimwa jumla ya magari 819 yakitokea Bara na Mataifa mengine yakiwemo yaliyobeba mzigo wa Madini ya Shaba ambapo kati ya hayo magari Saba yalizidisha uzito na hivyo kupaswa kulipa tozo .

Amesema, magari mengine yalilipa na kuendelea na safari lakini malalamiko ya Dereva Pamela Bukumbi wa gari la Simba Logistics alionyesha kutoamini vipimo ambavyo vimetokea kituo cha Mizani na kuamini kuwa amebambikiwa uzito ndio maana alikuwa anasisitiza katika Vyombo vya habari na mitandao mingine ya kijamii kuwa arudie kupima uzito kwasababu kilichoonekana kwenye vipimo ni tofauti na kilichoandikwa kwenye tiketi.

"Naomba nitoe ufafanuzi kuwa ,Mzani huu ni automated na kwamba sio operator( muendeshaji)au mfanyakazi wa mizani anaweza kuandika uzito eti kwasababu ya gari fulani limeingia hapa Mizani,Mzani huu ni automated unachukua uzito unaoonekana pale,"amesema Tarmo.

Amesema kuhusu hoja yake kutaka gari lake lirudiwe kupimwa kwamba suala hilo halipo kisheria na kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu.

Amesema Sheria ya udhibiti uzito ya Afrika Mashariki kifungu cha 17 ,kifungu kidogo cha 1 na kifungu kidogo cha pili inamtaka msafirishaji yeyote ambaye atabainika kuzidisha uzito kulipa kwanza tozo ya uzidishaji uzito na baada ya kulipa tozo hiyo aende kupunguza kiwango kilichozidi au kupanga mzigo wake vizuri.

Baada ya kufanya hivyo, ataruhusiwa  kurudia  kupima na kama gari itaonekana kuwa na viwango vya uzito vinavyokubalika kisheria ataruhusiwa na kuendelea na safari yake na sivyo kama dereva wa Simba Logistics alivyokuwa anataka .

Tarmo amesema kuwa kutokana na hali hiyo taasisi ilijaribu kufanya ufuatiliaji wa gari hilo kuanzia nchini Zambia katika Mizani zake mbili na hivyo kupata taarifa sahihi za vipimo vya gari hilo katika Mizani ya Kafulafuta na Mizani ya Mpika zote zikiwa nchini Zambia.

Katika Mizani ya Kafulafuta, Tarmo amesema kuwa vipimo vimeonyesha kuwa gari hilo ekseli ya mbele ilisoma Q - 6200 na katikati kwenye Difu ilisoma 17,600 na kisheria kwenye Difu ilitakiwa isome 16000 na akipewa asilimia tano inatakiwa isome 16,400 kwamba katika vipimo vya huko Zambia tayari alikuwa amezidisha uzito wa Q -1200.

Amesema, katika kundi lenye difu tatu huko katika Mzani wa Kafulafuta ilisoma 25,200, ambapo alifika mpaka katika mstari wa mwisho ( magine) wa asilimia tano na kwakuwa asilimia tano ya kundi la mwisho ni kilo 1200 maana yake Sheria inataka kubeba tani 24 na ukipewa asilimia tano maana kilo 1200 na inakuwa 25,200.

Amesema, katika Mizani hiyo GVM (Tani) ilikuwa 49 na gari hiyo ilitakiwa kubeba tani 48 tu na kwamba alikuwa amepitiliza tani nzima na kwenye ekseli alikuwa na kilo 1200 za ziada.

Katika Mzani wa pili wa Mpika huko Nchini Zambia, pia gari hilo katika ekseli ya mbele ilisoma kilo 6000 katikati ilisoma 16,800 na mwisho kwenye difu ilisoma 24,870 na hapo alikuwa amezidi kilo 400.

"Kwa haraka haraka kama dereva ambaye alikuwa anaendesha chombo hicho alipaswa kujua kutoka Kafulafuta hadi Mpika ndani ya nchi Moja ya Zambia kujua kwanini kuna utofauti huo wa kilo 1300 na alipaswa kujiuliza ni kitu gani kimepelekea uzito kuzidi,"amesema Tarmo

Amesema, gari hilo likiwa nchini Tanzania lilipima katika Mizani ya Makambako Mkoani Njombe ambapo uzito wa jumla ulikuwa tani 46,200 na kwamba ukiangalia mtiririko (Trend) Kunakuwa na utofauti wa zaidi ya tani mbili.

Tarmo, amebainisha kuwa gari hilo lilipofika katika Mizani ya Vigwaza Machi 13  mwaka huu baada ya kupimwa ilisoma tani 48.150 ikiwa imezidi kilo 150 na hivyo kulazimika kulipa tozo kwa mujibu wa Sheria.

Hatahivyo, Tarmo amesema vituo vya mizani vinafanyika kazi kwa mujibu wa Sheria huku akitoa wito kwa  madereva kufuata utaratibu wa kisheria pale ambapo Kunatokea changamoto kuzidisha uzito katika magari yao.


Mwisho.


Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA