MADEREVA WA POLISI PWANI WATAKIWA KUWA MFANO BARABARANI



Na. Julieth Ngarabali, PWANI.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Edson Mwakihaba, amewataka madereva wa Jeshi la Polisi mkoani humo kuwa kioo cha jamii na mfano wa kuigwa wanapokuwa barabarani.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi 
(SSP) Edson Mwakihaba


Mwakihaba ameyasema hayo , Agosti 14, 2026, wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa madereva wa magari ya polisi, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa Polisi Mkoani Pwani. Mafunzo hayo yanalenga kuwakumbusha umuhimu wa kutii sheria za usalama barabarani bila shuruti.

Amesisitiza kuwa kuwa askari polisi hakumpi dereva haki ya kuvunja sheria za barabarani. Hivyo, amewataka kuzingatia kanuni zote ikiwemo kuepuka mwendo kasi, kuheshimu taa za kuongozea magari, na kutoa kipaumbele kwenye vivuko vya watembea kwa miguu (zebra crossings).


Washiriki wa Mafunzo ya Madereva wa Magari ya Polisi

"Ili kufanikiwa katika mapambano dhidi ya ajali mkoani Pwani, tumeamua kuanzia ndani ya jeshi letu ili madereva wetu wawe mfano wa kuigwa. Nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa kuzingatia sheria ili muwe mabalozi wa kupunguza na kutokomeza ajali zinazosababishwa na ukiukwaji wa sheria unaofanywa kwa makusudi," alisema SSP Mwakihaba.



Akiwasilisha shukrani kwa niaba ya washiriki, Sajenti Bakari Kemkem ameahidi kuwa wako tayari kubadilika, kutekeleza maelekezo hayo kwa vitendo, pamoja na kuwasambazia elimu hiyo madereva wengine wa vyombo vya serikali.



Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewataka pia wananchi na watumiaji wote wa barabara kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa sheria za barabarani bila kujali kama anayevunja sheria hiyo ni dereva wa chombo cha binafsi, cha umma, au cha serikali ili kwa pamoja kuokoa maisha na mali za Watanzania.


Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

MWENYEKITI KITONGOJI CHA KWAKIBOSHA MAPINGA AWAPIGA MSASA VIJANA 500 KULINDA AMANI YA TAIFA.

WIZARA YA AFYA YASEMA:UGONJWA WA SIKOSELI SIO WA KUROGWA, YAHAMASISHA JAMII KWENDA KUPIMA VINASABA

TAIFA GAS TANZANIA YAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA