TISEZA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI KWALA YATENGA EKARI 100 KWA AJILI YA UWEKEZAJI
Na Gustaphu Haule, Pwani
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesema imetenga ekari 100 katika eneo la Kwala katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Kaimu Meneja Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma kutoka TISEZA Adelina Rushekya ametoa kauli hiyo Septemba 30,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika mkutano maalum uliofanyika eneo la Kwala.
Rushekya amesema kuwa maeneo ya Kwala yana vivutio vinavyotakiwa kwa ajili ya uwekezaji huku akisema fursa za uwekezaji zipo vizuri katika kila sekta.
Rushekya amesema mwekezaji atakayekuwa tayari kuwekeza katika eneo hilo atapatiwa ekari moja na pia anatakiwa kuwa na mtaji wa dola za Kimarekani milioni tano kwa wazawa na kwa raia wa kigeni anatakiwa kuwa na dola milion kumi.
Aidha Rushekya amesema kuwa mwekezaji atakayepata eneo hilo atatakiwa kuliendeleza ndani ya miezi 12 kwa kujenga kiwanda ambacho amelenga kuwekeza.
Moja ya Maeneo ya uwekezaji eneo la Kwala
Ameongeza kuwa wawekezaji katika kongani ya viwanda Kwala mbali ya kupata ardhi bure pia watanufaika na msamaha wa kodi.
"Tunatoa kipaumbele kwa wazawa kuja kuwekeza mahali hapa lakini nafarajika kuona hadi sasa wazawa waliojitokeza kutaka kuwekeza eneo hili ni wengi na tunahamasisha zaidi kuja kuwekeza hapa kwakuwa fursa bado zipo zakutosha,"amesema Rushekya.
Kaimu Meneja Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma kutoka TISEZA Adelina Rushekya akikagua bidhaa aina ya majokofu( Friji) zinazozalishwa na kampuni ya Snowsea iliyopo katika eneo la Kwala Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.
Rushekya, amesema kuwa mwekezaji yeyote anayekuja kuwekeza katika kongani ya viwanda atakuwa amepata unafuu katika usafirishaji wa malighafi kwakuwa viwanda eneo hilo vipo vingi na itakuwa rahisi katika kupata malighafi zinazohusika.
Kwa upande wake msimamizi wa kampuni ya Snowsea ambao ni watengenezaji wa majokofu Gerald Wilfred amesema kampuni hiyo tayari imetoa ajira 30 wengi wao wakiwa wazawa.
Wilfred amesema wafanyakazi wa kampuni hiyo wamepewa ujuzi wa namna ya kutengeneza majokofu hayo jambo ambalo kwasasa wanaendelea nalo wenyewe bila msaada wa raia wa kigeni.
Amesema wafanyakazi hao ambao idadi kubwa ni wakazi wa Kwala wamenufaika na mradi huo kwa kupata ajira sambamba na wafanyabiashara wadogo wadogo kuendelea na biashara zao.
Comments
Post a Comment