RC PWANI ATAKA MRADI WA IPOSA UTOE MATOKEO CHANYA KWA VIJANA
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, ameielekeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuhakikisha programu ya Mpango wa IPOSA inakuwa na matokeo chanya kwa kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuajirika. IPOSA ni Mpango ulioandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Watu wazima wa elimu changamani kwa Vijana walio nje ya Shule.
Kunenge ametoa maelekezo hayo wakati akifunga mafunzo ya walimu wa programu hiyo yaliyofanyika Oktoba 2,2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na wasimamizi wa mradi wa IPOSA katika mkutano uliofanyika Oktoba 2,2025 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Alisema kuwa elimu inayotolewa kupitia IPOSA haipaswi kubaki kwenye vyeti pekee, bali iwe chachu ya mabadiliko katika maisha ya vijana ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ajira.
“Mradi huu wa IPOSA lazima uwe na matokeo ya kweli, vijana wanapaswa kufundishwa stadi zitakazowawezesha kujitegemea kiuchumi, pamoja na kupunguza idadi ya watu wazima wasijua kusoma na kuandika",alisema Kunenge.
Aidha, Kunenge alimuagiza Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani Jimmy Nkwamo kuhakikisha anasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kuwanufaisha vijana katika kuendeleza maisha yao.
“Nakuagiza afisa elimu mkoa kuhakikisha kuwa programu ya IPOSA inaleta matokeo yanayoonekana kwa vijana na jamii kwa ujumla, tunahitaji kuona ushahidi wa mafanikio,” aliongeza Kunenge.
Programu ya IPOSA inalenga kuwafikia vijana waliopo nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kuwapatia ujuzi na maarifa mbalimbali, yakiwemo mafunzo ya stadi za maisha, ujasiriamali, kusoma, kuandika, kuhesabu na mafunzo ya amali, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Mafunzo hayo yamekuwa yakitekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha kundi la vijana lisilofikiwa na mfumo wa kawaida wa elimu linapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania Profesa Philipo Sanga,alisema kuwa mradi wa IPOSA unatekelezwa katika mikoa Sita ya Tanzania Bara ukiwemo Mkoa wa Pwani, Simiyu, Manyara, Singida, Shinyanga na Tanga.
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania Profesa Philipo Sanga akizungumza katika mkutano wa wasimamizi wa mradi wa IPOSA uliofanyika Oktoba 2,2025 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Sanga,alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu ya pili chini mfadhili KOICA kutoka Korea Kusini ambapo awamu ya kwanza ulikuwa ukitekelezwa chini ya ufadhili wa UNICEF,Plan - International pamoja na Care - International.
Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea hali ya ubunifu na msukumo wasimamizi wa mradi huo hata pale ambapo wafadhili watakoma kwakuwa mradi huo ni muhimu kwani unasaidia kupunguza changamoto za vijana hasa wale ambao walidondoka kutoka katika mtihani wa kitaifa.
Alisema kuwa mdondoko wa wanafunzi ni mkubwa na baadhi ya shule inafikia asilimia 45 ambapo kila mwaka wanafunzi 450,000 wanadondoka kutoka katika mfumo rasmi.
Wasimamizi na wathibiti ubora wa Program ya IPOSA wakiwa katika mkutano maalum uliofanyika Oktoba 2,2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha
"Jukumu la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ni kuwapa fursa vijana wa Tanzania waliokosa kuendelea na mfumo rasmi ndio maana kuna program ya IPOSA ambayo mbali na kuwaongezea elimu lakini inawapa ujuzi ambao unawasaidia katika maisha yao,"Alisema Profesa Sanga.
Profesa Sanga, alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa ipo mikoa 10 bora inayotekeleza program ya IPOSA ambapo Mkoa wa Pwani unashika nafasi ya Saba ukiwa na asilimia 13.7.
Alisema anamatumaini kuona vijana wanapata ujuzi wa kuendeleza maisha yao na matokeo hayo wameyaona kwenye mikoa ambayo imetekeleza mradi wa IPOSA ambapo baadhi ya vijana wameunda vikundi ambavyo vinawasaidia kupata mikopo.
Mwakilishi wa KOICA ambao ndio wafadhili wa mradi wa IPOSA awamu ya pili Efratha Kristos,alisema kuwa mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri 30 kukiwa na vituo 31 ambapo Kati ya hivyo vituo 27 vya kawaida,vituo vitatu vya mfano na kituo kimoja cha kipekee kilichopo Mkoa wa Tanga,
Mwakilishi wa Shirika la KOICA Efratha Kristos akizungumza katika mkutano wa wasimamizi na wathibiti ubora wa Shule kuhusu mradi wa IPOSA mkutano ambao ulifanyika Oktoba 2,2025 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Kristos,alisema IPOSA inatoa mafunzo mbalimbali kwa vijana ikiwemo ufundi seremala,umeme wa majumbani, kushona nguo,urembo,masuala ya saluni,utengenezaji wa batiki pamoja na Kilimo cha Mbogamboga na matunda.
Hatahivyo, alisema kuwa anatarajia kuona namna vijana waliopo katika mradi huo wanapata msaada ili waweze kujikwamua kiuchumi ikiwemo kupata mikopo ya Halmashauri na hata fursa za kazi pale zinapotokea.
Comments
Post a Comment