MWENEZI CCM PWANI AKOLEZA MOTO USIKU WA COREFA,ASIFU MAANDALIZI YAKE
Na Gustaphu Haule, Pwani
CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kimetoa tuzo kwa wachezaji na wadau mbalimbali waliochangia kwa namna au nyingine katika kuendeleza mchezo wa mpira wa Miguu katika msimu wa mwaka 2024/2025.
Hafla hiyo imefanyika Agosti 9, 2025
katika ukumbi wa Maisha Plus uliopo karibu na ofisi ya Kamanda wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Pwani ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo Katibu wa Siasa,
Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Pwani.
Zaidi ya wadau 50 walishiriki hafla
hiyo wakiwemo waamuzi wa mpira wa miguu, wachezaji wa mpira wa miguu
,viongozi wa vyama vya michezo kutoka Wilaya za Mkoa wa Pwani,walimu
timu,mashabiki wa michezo ,na wajumbe kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Pwani Robert Munisi alisema ni mara ya pili kufanyika kwa hafla
hiyo kwani kwa mara ya kwanza uliofanyika msimu wa mwaka 2023/2024 ambapo
lengo la kuandaa hafla hiyo ni kuwakutanisha pamoja wanamichezo ili kuweza
kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya michezo hususani mpira wa miguu.
Munisi amesema jambo la pili ni kutambua mchango wa wachezaji pamoja na kuthamini michango ya wadau waliyoitoa katika kuendeleza soka la Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa Corefa inasimamia mpira ikiwa pamoja na kuinua vipaji kwa vijana lakini pia ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisaidia kuinua michezo na vipaji kwa vijana hapa nchini.
Amesema ili kuendeleza mpira wa Miguu ndani ya Mkoa wa Pwani kila kiongozi anatakiwa atimize wajibu wake kwa kuhakikisha wanawasimamia vijana katika kukuza vipaji vyao licha ya kuwa Corefa imekuwa ikijitolea katika kusaidia vijana .
Alisema changamoto kubwa ya Mkoa wa Pwani ni ukosefu wa viwanja vizuri vya michezo ambapo ameiomba kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani itembelee viwanja vilivyopo na ikiwezekana vikarabatiwe kwa ajili ya kusaidia kuendeleza vipaji vya watoto na vijana .
Akizungumza wakati akifungua hafla hiyo Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani David Mramba amesema kuwa michezo sio tu burudani bali ni nyenzo muhimu ya kuimarisha umoja,kujenga afya bora, kuendeleza vipaji na kujenga uchumi.
Amewapongeza wadau wote waliojitoa kufadhili na kudhamini michezo mbalimbali katika msimu uliopita lakini Serikali na vyama vya michezo vina wajibu wa kuendeleza sera ya miundombinu bora ya michezo,kuweka vituo vya kukuza vipaji ili kuhakikisha Mkoa unapata heshima .
Amesema kuwa ,michezo ni fursa na daraja linaloweza kukupeleka mbali kielimu na kucheza katika nchi mbalimbali lakini unaweza kufika huko ukiwa na nidhamu,hekima na maadili.
Maramba amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya hasa katika michezo kwani amekuwa kiongozi bora wa michezo Tanzania lakini pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia pamoja na Katibu wa CCM Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi kwa kuchukua fomu ya kugombea Urais.
Tuzo zilizotolewa katika hafla hiyo ni tuzo ya mfungaji bora wa kiume na wakike,tuzo ya wachezaji bora,tuzo ya magolikipa bora,waamuzi bora,kocha bora,meneja bora wa uwanja,msimamizi bora wa michezo,timu bora,timu bora yenye nidhamu na utoaji wa vyeti vya shukrani kwa wadau waliochangia michezo Mkoa wa Pwani akiwemo Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga.
Hata hivyo, Makamu mwenyekiti wa
Corefa Mohamed Lacha amewashukuru wadau kwa kufika katika hafla hiyo huku
akitambua michango ya wadau mbalimbali waliofanikisha michezo kufanyika Mkoa wa
Pwani akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara Selemani Jafo,Naibu Waziri wa
Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga,aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha
Mjini Silvestry Koka na Mjumbe wa Mkutano mkuu wa TFF Rugemalila Rutatina.
Comments
Post a Comment