MHARIRI MAKALA UHURU PUBLICATIONS LTD SELINA WILSON ATETEA NAFASI YAKE KIBAHA.
Na Gustaphu Haule ,Pwani
MHARIRI Makala wa Uhuru Publications Ltd ya Jijini Dar es Salaam Selina Wilson Msenga amefanikiwa kutetea nafasi yake ya udiwani wa Vitimaalum katika Manispaa ya Kibaha kwa kupata kura 527.
Selina ambaye kwasasa ni awamu yake ya nne kushinda katika nafasi hiyo amekuwa na mvuto wa aina yake kwa Jamii ya Manispaa ya Kibaha licha ya kuwa katika uchaguzi huo amekutana na vipingamizi mbalimbali.
Aidha, katika uchaguzi wa UWT uliofanyika Julai 20, 2025 Kata ya Mkuza Kibaha Selina alipewa asilimia chache za ushindi kutokana na mvutano mkali wa kisiasa uliokuwepo kati yake na wapinzani wake lakini iliwaduwaza baadhi ya wanaCCM baada ya kuibuka kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Selina Wilson watatu kutoka kulia akiwa pamoja na wagombea wenzake katika uchaguzi wa UWT Manispaa ya Kibaha uliofanyika Julai 20,2025
Licha ya Selina kupewa asilimia chache za ushindi katika uchaguzi huo lakini alijikuta anapenya na kuwa miongoni mwa washindi waliokuwa wanahitajika katika nafasi tatu za ushindi kutoka Tarafa ya Kibaha .
Katika uchaguzi huo Selina alikuwa akitetea nafasi yake pamoja na wenzake watatu akiwemo Aziza Mruma (Kura 952), Shufaa Bashari(Kura 581) na Lidya Mgaya(Kura 575) lakini Safu hiyo imejazwa na Sarah Uled ambaye kwa mara ya kwanza ameingia akiwa ameongoza kwa kupata kura 864 akitokea tarafa ya Kongowe.
Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo Selina amesema kuwa anamshukuru mwenyezi Mungu kwa kumpigania kwakuwa haikuwa kazi rahisi kwake kutetea nafasi yake.
Amesema uchaguzi wa mwaka huu kwake ulikuwa mgumu kwakuwa alikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanaCCM wenzake lakini pamoja na hayo imeonyesha kuwa wajumbe bado wanamapenzi na imani kubwa kwake.
Aidha,Selina ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wajumbe wote waliomchagua na wale wasiomchagua na kusema hana cha kuwalipa lakini anaimani Mungu atasimama nao.
Amesema kikubwa kwasasa ni kushirikiana na wanachama wa UWT pamoja na wale wa CCM kiujumla kwa ajili ya kuchapakazi kwa faida ya Umoja na chama na kwamba yeye yupo tayari kutumwa na akatumika kwa faida na maendeleo ya Wananchi wa Manispaa ya Kibaha.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi mkuu wa uchaguzi Ally Kibwana amesema kuwa katika uchaguzi huo kulikuwa na wagombea 15 huku wapiga kura wakiwa 1094 ambapo kura halali ni 1083 na zilizoharika ni 11.
Kibwana ,amewashukuru wajumbe hao kwa uvumilivu na utulivu wao hali ambayo ilisababisha uchaguzi huwe huru ,utulivu na amani na kuwataka wajumbe hao kuendelea kushikamana zaidi katika chaguzi zijazo.
Msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo ambaye ni katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Bagamoyo Halima Dossa amewashukuru wagombea kwakuwa na moyo wa ujasiri ambaye alisema kuwa huo ndio uanasiasa na haitakiwa kwenda katika uchaguzi na matokeo mfukoni.
Hatahivyo,Dossa amewashukuru wanafunzi waliojitokeza kusaidia uchaguzi huo ambapo amesema wawe na moyo huo na kwamba imani yake watakuwa wanasiasa wazuri baadae.
Comments
Post a Comment