MEDIA BRAINS YAWAPIGA MSASA WAANDISHI WA HABARI PWANI
Na Gustaphu Haule, Pwani
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya habari ya Media Brains iliyopo Jijini Dar es Salaam Jesse Kwayu wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya masuala ya uchaguzi kwa Waandishi hao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Julai 9, 2025 Mjini Kibaha yaliwashirikisha Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali huku yakiwa chini ya wakufunzi wawili akiwemo mwandishi wa habari mkongwe Absalom Kibanda na Jesse Kwayu.
Katika mafunzo hayo Kibanda alifundisha kuhusu masuala ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na sheria ya uchaguzi ya Rais,Wabunge na Madiwani huku Jesse Kwayu akifundisha wajibu wa Waandishi wa habari katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu na masuala ya Jinsia.
Katika mafunzo hayo Kwayu amesema kuwa waaandishi wa habari wamebeba dhamana kubwa ya kuelimisha jamii na ndio tegemeo kubwa katika masuala ya uchaguzi hivyo ni vyema kila mmoja akatumia kalamu yake kwa umakini.
Mwandishi wa Habari mwandamizi Victor Masangu (kushoto) akipokea cheti cha kushiriki mafunzo ya kuandika habari za uchaguzi kutoka kwa Meneja miradi wa KAS Damasi Nderumaki (Kulia) katika mafunzo yaliyofanyika Julai 9, 2025 Mjini Kibaha
Mwandishi wa Habari wa gazeti la Nipashe Julieth Mkireri (Kushoto) akipokea cheti cha kushiriki mafunzo ya kuandika habari za uchaguzi kutoka kwa meneja miradi wa KAS Damasi Nderumaki (Kulia).
Amesema kuwa ,Kwa kuzingatia umuhimu wa Waandishi wa habari hapa nchini hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu kampuni ya Media Brains imeona ni vyema ikawakumbusha Waandishi hao katika kutimiza wajibu wao kwa kufuata maadili,Sheria na kanuni zilizowekwa.
"Natambua kuwa wapo Waandishi wa habari wengi wameripoti masuala ya uchaguzi lakini sisi tumekuja hapa kukumbushana wajibu wetu lakini wapo wengine ambao hawajawai kuripoti hata chaguzi moja na wao watapata fursa mpya ya kwenda kutekeleza wajibu wao kikamilifu,"amesema Kwayu.
Nae Kibanda,amesema kuwa Tanzania kwa mara ya kwanza imepata Tume Huru ya uchaguzi ambapo aliipongeza Serikali kupitia Rais Dkt ,Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuundwa kwa Tume hiyo.
Aidha, Kibanda amesema kuundwa kwa tume hiyo kutasaidia kuondoa changamoto na malalamiko ya vyama vya Siasa kwakuwa kila kitu kitakuwa wazi na Vyama vitapata haki sawa.
"Mimi napongeza kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi lakini naamini kama kutafanyika mabadiliko kwa baadhi ya vipengele vilivyopo katika Tume hiyo hali ya uchaguzi itakuwa ya amani na utulivu,"amesema Kibanda.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo Neville Meena,amesema kuwa kampuni ya Media Brains imeanza kutoa mafunzo hayo katika mikoa mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Mbeya ,Mwanza na sasa Pwani, Morogoro,na Dar es Salaam na kisha baadae Kilimanjaro.
Meena,amesema kuwa mafunzo hayo yanafadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali kutoka nchini Ujerumani Kondrad Adenaeauer Stiftung (KAS).
Hatahivyo, Meneja miradi wa KAS anayesimamia upande wa Tanzania Damasi Nderumaki amesema kuwa Wajerumani wamejitoa kusaidia Watanzania kupitia kodi za wananchi wao na anapenda kuona fedha hizo zikitumika ilivyokusudiwa.
Nderumaki ,amewataka Waandishi hao kutumia fursa hiyo kikamilifu kwa ajili ya kuelimisha jamii juu ya kuona umuhimu wa kushiriki uchaguzi sambamba na kuchagua viongozi wazuri wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo.
Comments
Post a Comment