MANISPAA YA KIBAHA YAFANYA KIKAO KAZI KUIMARISHA UWAJIBIKAJI
Na Gustaphu Haule,Pwani
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imefanya kikao kazi maalum kilichowakutanisha Maafisa Kilimo na Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kukumbushana wajibu wa kila siku katika kutekeleza majukumu yao ya kiutumishi.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Kibaha Julai 1, 2025 kikilenga kuimarisha utendaji kazi, uwajibikaji, ubunifu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Baadhi ya Watumishi wa Manispaa ya Kibaha wakiwa katika kikao kazi cha kujadili uwajibikaji kazini kilichofanyika jana.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amewataka watumishi wote kuongeza ubunifu katika kazi zao, kuachana na kufanya kazi kwa mazoea, na kuhakikisha mapato ya ndani yanakusanywa kikamilifu kwa maendeleo ya Halmashauri na wananchi wake.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akizungumza katika kikao kazi na watumishi wake kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.
“Ni lazima tuwe wabunifu katika kila tunalolifanya. Tusifanye kazi kwa mazoea,Wananchi wanategemea huduma bora kutoka kwetu, na sisi ndiyo daraja la utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” amesema Dkt. Shemwelekwa.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Manispaa hiyo,Mrisho Mlela, amesema ofisi yake tayari inaendelea kufuatilia kwa karibu utendaji wa watumishi na kuwataka kufuata makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho, akisisitiza kuwa makubaliano hayo ni sheria inayopaswa kuheshimiwa na kutekelezwa ipasavyo.
Comments
Post a Comment