93 WAJITOKEZA KUCHUKUA FOMU ZA KUGOMBEA UBUNGE MKOA WA PWANI
Na Gustaphu Haule,Pwani
WANACHAMA 93 wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) kutoka Mkoani Pwani wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama kwa ajili ya kugombea nafasi ya ubunge katika majimbo mbalimbali yaliyopo Mkoani Pwani.
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Mkoa wa Pwani David Mramba ametoa taarifa hiyo Julai 2 ,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi za CCM Mkoa wa Pwani zilizopo Mjini Kibaha .
Mramba amesema kuwa Mkoa wa Pwani una majimbo tisa ambapo tangu dirisha la uchukuaji fomu za kuwania nafasi ya ubunge Mkoa wa Pwani umepata wagombea 93 na kati ya hao Wanaume ni 71 na Wanawake 22.
"Mchakato wa uchukuaji fomu na kurudisha kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika majimbo ulianza Juni 28 na kumalizika Julai 2, 2025 na katika mchakato huo Pwani wamejitokeza wanaCCM 93 katika majimbo yote tisa",amesema Mramba
Mramba ametaja majimbo hayo na idadi ya wagombea kuwa ni Chalinze yenye wagombea (3) Wanaume akiwemo Ridhiwani Kikwete ,Bagamoyo(11) kati ya hao Wanaume 7 na Wanawake (4) na Kibaha Vijijini (9) Wanaume 7 na Wanawake 2.
Katika Jimbo la Mafia waliojitokeza ni (6) Wanaume 5 na Mwanamke 1, Wakati Jimbo la Kisarawe wamejitokeza 12 Wanaume 10 na Wanawake 2 huku Jimbo la Mkuranga waliojitokeza ni 15 Wanaume 9 na Wanawake 6.
Jimbo la Kibiti Mramba amesema waliojitokeza ni 10 ambapo Wanaume 9 na Mwanamke 1 na Jimbo la Rufiji wapo 10 Wanaume 9 na Mwanamke 1 huku Jimbo la Kibaha Mjini waliochukua fomu ni 19 kati yao Wanaume 15 na Wanawake 4.
Aidha ,Mramba amesema kuwa mwaka huu kuna tofauti na mwaka 2020 kwani mwaka 2020 mhamko ulikuwa mkubwa wa kuchukua fomu lakini mwaka 2025 imeshuka.
Amesema imeshuka kwasababu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanyakazi kubwa na Mkoa wa Pwani umepata heshima kubwa kwakuwa Rais Samia ameleta miradi mingi ya maendeleo ambayo imesababisha hata wale waliokuwa wanataka kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge kuacha.
Hatahivyo, Mramba amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kwa ushirikiano wake mkubwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwakuwa amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha miradi ya yote inayoletwa na Rais Samia inatekeleza ipasavyo.
Club News Editor
Comments
Post a Comment