MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAPIGA KAMBI PWANI
Na Gustaphu Haule,Pwani
Club News Editor
TIMU ya madaktari bingwa 64 ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan imepokelewa Mkoani Pwani kwa ajili ya kuanza kazi maalum ya kutoa huduma ya matibabu na uchunguzi wa Wananchi wa maeneo mbalimbali yaliyopo Mkoani Pwani.
Timu hiyo imepokelewa leo Juni 9, 2025 katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Pwani na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Kusirye Ukio ambaye katika hafla hiyo Ukio amemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani Kusirye Ukio, akizungumza na madaktari bingwa wa Rais Samia mara baada ya kuwasili Mkoani humo leo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwa jamii.
Akizungumza katika hafla ya kuwapokea madaktari hao Ukio amewapongeza madaktari hao kwa utayari wao huku akiwaomba kwenda kujitoa kwa ajili kuwasaidia Wananchi na jamii kiujumla katika kupata huduma bora ya uchunguzi na matibabu.
Ukio, amesema kuwa Rais Dkt.Samia ameanzisha jambo kubwa na nzuri lenye maslahi ya Wananchi wake na kwamba anataka kuona kampeni hiyo inakuwa na msaada kwa Watanzania wote katika kuwaondolea changamoto za kimatibabu zinazowakabili.
Amesema kuwa, katika kufikia malengo ya Rais Samia madaktari ndio wamepewa heshima na dhamana kubwa ya kufanyakazi hiyo huku akisema ni vyema sasa wakafanyekazi bila kuchoka na wakajitume kwa nguvu na uwezo wao wote.
Madaktari bingwa wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wakipokelewa leo Juni 9, 2025 katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Pwani tayari kwa kuanza kazi ya kutoa huduma kwa Wananchi wa Halmashauri mbalimbali Mkoani Pwani.
Ukio, amewatoa wasiwasi madaktari hao kuwa maeneo waliyopangiwa yapo vizuri kwakuwa miundombinu imeboreshwa na kuwekwa vifaa vya kutosha vitakavyorahisisha utendaji wa kazi zao.
"Najua mpo madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali na wauguzi kwahiyo niwaombe msichoke ,nendeni mkawahudumie Wananchi na mkawape huduma sahihi lakini mkatangaze upendo na msiogope kusema ukweli ," amesema Dr Ukio
Pamoja na mambo mengine, Ukio amewaomba madaktari hao katika kutoa huduma wahakikishe wanawasimamia vizuri wataalam wengine ili kuhakikisha huduma inayotolewa inakuwa bora zaidi.
Ukio, ameongeza kuwa Mkoa utakwenda kufanyiakazi yale yote yatakayojitokeza katika zoezi hilo kwakuwa lengo la Rais Samia ni kutaka kuboresha huduma ya afya hapa nchini.
Kwa upande wake afisa programu kutoka Wizara ya afya Joachim Masunga, amesema kuwa madaktari hao wanatoka katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo hospitali ya Taifa Muhimbili.
Afisa programu kutoka Wizara ya afya Joachim Masunga akizungumza na madaktari bingwa wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan walipowasili Mkoani Pwani Juni 9,2025 kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwa jamii
Masunga, amesema kuwa Mkoa wa Pwani imeingia timu ya madaktari bingwa na wauguzi wakiwa jumla 64 ambao wamegawanywa na kupelekwa katika Halmashauri zote za Mkoa.
Amesema kuwa, timu hiyo itafanyakazi kwa muda wa siku tano na mgonjwa atapata huduma ya kibingwa papo hapo na wale ambao watagundulika kuwa na shida zaidi utaratibu mwingine utafanyika.
Masunga, ametaja baadhi ya magonjwa yatakayochunguzwa kuwa ni magonjwa ya Wanawake na Uzazi, magonjwa ya watoto, Upasuaji, dawa za usingizi, magonjwa ya ndani na magonjwa ya kinywa na meno
Mratibu wa timu ya madaktari bingwa Mkoa Pwani Aden Mpangile, amesema mpaka sasa zoezi linaendelea vizuri kwa kila Halmashauri ambapo amewaomba Wananchi kujitokeza na kutumia fursa hiyo Kwa ajili ya kuchunguza afya zao.
Madaktari bingwa wa Rais Samia wakiwa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani Kusirye Ukio leo Juni 9,2025 walipopokelewa katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Pwani.
Daktari bingwa wa magonjwa ya Wanawake na Uzazi Dr.Mdoe Gumbo kutoka katika Manispaa ya Kibaha amesema yeye na wenzake wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa huduma hiyo kikamilifu kwa jamii .
Comments
Post a Comment