WANANCHI KITONGOJI CHA KWAKIBOSHA MAPINGA WAMCHARUKIA PETER JUNIOR ANAYETAKA KUVUNJA NYUMBA ZAO, WAMUOMBA RAIS SAMIA KUINGILIA KATI
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor
WANANCHI wa Kitongoji cha Kwakibosha katika Kata ya Mapinga Bagamoyo Mkoani Pwani wameiomba Serikali kumchukulia hatua za kisheria Peter Junior ambaye anadaiwa kutaka kupora ardhi sambamba na kuvunja nyumba za wakazi wa eneo hilo.
Wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuingilia kati jambo hilo ili kusudi kuwafanya Wananchi hao kuishi kwa amani na utulivu na hivyo kuondokana na taharuki iliyopo hivi sasa.
Wametoa ombi hilo katika mkutano wao maalum wa kuzungumza na Waandishi wa habari juu ya kutoa kero hiyo ikiwa ni sehemu ya kuiomba Serikali kutafuta ufumbuzi juu ya mgogoro huo ambao hauna afya kwa maisha yao.
katika mkutano huo uliofanyika Mei 20, 2025 katika Kitongoji hicho mmoja wa Wananchi hao Elias Kashaga, amesema kuwa anashangazwa kuona Peter Junior amekuwa akiwasumbua na kutaka kupora eneo lao kinyume na utaratibu.
Mwananchi wa Kitongoji cha Kwa Kibosha kilichopo Kata ya Mapinga Bagamoyo Mkoani Pwani Elias Kashaga,akieleza masikitiko yake juu ya kubomolewa nyumba yake na mtu anayejulikana kwa jina la Peter Junior
Kashaga, amesema kuwa yeye ni mhanga wa eneo hilo ambaye nyumba yake awali ilivunjwa na Peter Junior kwa madai ya kuwa eneo hilo ni lake huku akisema mtu huyo amekuwa akiwatesa sana Wananchi wa eneo hilo.
"Tunaiomba Serikali iingilie kati jambo hili ikiwa pamoja nakumfanyia uchunguzi huyu mtu na ikiwezekana Takukuru,Wizara ya Ulinzi na Vyombo vya vingine vya usalama vimalize jambo hili kwa haraka ili kuzuia hatari inayoweza kutokea hapo baadae,"amesema Kashaga.
Nae Yolanda Mingoi, Mkazi wa Kwa Kibosha amesema kuwa Peter Junior anawafanya Wananchi wakose amani kwa vitisho vyake kwa jamii huku akisema anatumia ujanja na njia zisizo sahihi kutaka kupora ardhi ya Wananchi hao.
Yolanda Mingoi Mkazi wa Kitongoji cha Kwakibosha akizungumza na Waandishi wa habari leo Mei 20,2025 kuhusu namna wanavyopata taharuki ya kutaka kubomolewa nyumba zao na mtu anayejulikana Kwa jina la Peter Junior
Mingoi, ameiomba Serikali ya awamu ya Sita Chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo ili kuwafanya Wananchi hao waishi kwa amani kwakuwa anaamini Peter Junior hana viwanja Wala kipande chochote cha ardhi katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Shabani Rashid akifafanua jambo hilo katika mkutano huo, amesema kuwa eneo la Kwa Kibosha lina nyumba 120 na wakazi zaidi ya 300.
Rashid, amesema kuwa Peter Junior ndio amekuwa mtu msumbua kwa Wananchi wake akitaka kupora ardhi ya Wananchi kwa kutumia mabavu lakini hatahivyo hawezi kukubali kuona Wananchi hao wanapata shida.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwakibosha kilichopo Kata ya Mapinga Bagamoyo Mkoani wa Pwani Shabani Rashid akizungumza na Waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika eneo kuhusu Peter Junior anayedaiwa kutaka kupora maeneo ya Wananchi hao.
Amesema, Peter Junior hana eneo lolote na kwamba hata alipokwenda Mahakamani amekwenda kumshtaki mtu anayeitwa Peter Maro kuwa amevamia eneo lake jambo ambalo linashangaza kwakuwa Peter Maro hana eneo katika Kitongoji hicho na wala hajulikani katika Kitongoji hicho .
Amesema kuwa, vitendo vya Peter Junior kuwasumbua Wananchi hao vimekuwa vya mara kwa mara na hivyo kuwafanya Wananchi waishi kwa hofu kutokana na taharuki kubwa iliyopo huku akisema awali alibomoa nyumba 12 katika eneo hilo.
"Ni kweli Peter Junior alikwenda Mahakamani lakini hukumu ya Mahakama inamuhusu Peter Maro ambae hapa kwetu hana kipande cha ardhi,wala hajulikani na Wananchi wa hapa na Wala hajawai kuuza ardhi kwa yeyote miongoni mwetu,",amesema Rashid.
Rashid, amesema kuwa ndugu Peter Junior itakuwa busara kwake akienda kuonesha hiyo ardhi aliyoshinda kwa Peter Maro ili amuamuru kuondoka katika ardhi hiyo yeye na washirika wake kama ambavyo amri ya Mahakama ilivyohitaji.
"Ndugu Wananchi,ardhi hii hakuna kipande hata kimoja ambacho kinamilikiwa na Peter Maro Wala washirika wake isipokuwa ardhi hii inamilikiwa na watu tofauti tofauti wapatao 120 ambao hawajawahi kuuziwa na Peter Maro hata hatua Moja wala kuuziwa na washirika wake,", amesema Rashid
Mwenyekiti Rashid, ameongeza kuwa kwasasa yupo imara na msimamo wake ni kuwa hukumu inahusu shamba la Peter Maro na sio Wananchi 120 ambapo amemtaka Peter Junior aoneshe wawakilishi wa Mahakama ardhi aliyoshinda na aache kuchezea Wananchi wake.
"Naomba nitumie fursa hii kutangaza kuwa utapeli wa ardhi Kwakibosha ni marufuku na yeyote asijihusishe na watu wanaoamini kuwa wanaweza kuhonga fedha tafuteni wa kumhonga ila sio mimi,"amesema
Rashid,amesema kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na kilichombele yao ni kuhakikisha wanatimiza aadi ya kumpa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kura za kutosha kwakuwa amekuwa kiongozi wa mfano anayefanyakazi za kutatua kero za Wananchi sambamba na kuliletea Wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Peter Junior, amesema kuwa hao watu wanaolalamika walinunua eneo hilo kutoka kwa Ally Mguru kwa mujibu wa dokumenti (documents)zao ambazo walizitoa Mahakamani na hao Wananchi wanaolalamika waliwahi kufungua kesi Mahakama Kuu kesi namba 260 ya Mwaka 2003 na walishindwa.
Junior,amesema yeye haitaji msaada wa kiongozi yeyote na hivyo atabomoa kwa amri ya Mahakama na atalichukua eneo hilo kwa mujibu wa Sheria.
Comments
Post a Comment