WANACHAMA CCM NYANG'HWALE WASIKITISHWA KUKWAMA KWA UJENZI WA OFISI YAO ,WATAKA FEDHA ZILIZOCHANGWA ZITUMIKE KUKAMILISHA OFISI HIYO.
Na Mwandishi wetu, Geita
BAADHI ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyang'hwale Mkoani Geita wameeleza kusikitishwa na kitendo kinachofanywa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kukwamisha ujenzi wa jengo la ofisi ya CCM Wilayani humo.
Wamesema viongozi hao ,wamekuwa wakitoa sababu ya kukosa fedha za kuendeleza ujenzi wa ofisi hiyo ili hali zipo fedha kutoka kwa wadau pamoja na mmoja wa viongozi wakubwa ambazo zimewekwa bila kutumika ndani ya miezi mitatu sasa.
Wanachama hao wamewaambia Waandishi wa habari Mei 03,2025 kuwa mpaka sasa wanafahamu kuwa mmoja wa kiongozi ambaye ni Naibu Waziri Mkuu Dkt.Dotto Biteko tayari amechangia fedha zinazokadiriwa kuwa Sh. milioni 50 lakini hazijatumika .
Kwa mujibu wa wanachama hao wamesema kuwa fedha za mchango kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu zilipokelewa na Mbunge wa Jimbo la Nyang'hwale Hussein Nassoro Amar miezi mitatu iliyopita lakini mpaka sasa hakuna kazi iliyofanyika.
Wamesema kuwa,fedha hizo zilitolewa ili kukamilisha ahadi ya Naibu Waziri Mkuu alipofanya ziara fupi katika Wilaya hiyo mwaka jana ambapo akiwa katika mkutano wa hadhara alisema atachangia fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha jengo la ofisi ya CCM Wilaya.
Wamesema,wanatambua fedha hizo zilipitia katika akaunti ya mbunge huku mwenyekiti wa CCM Wilaya Adam Mtore ambaye ni Mdogo wake na Mbunge anafahamu na ndiye aliyeagiza fedha hizo ziingie katika akaunti ya Mbunge.
"Shughuli za ujenzi wa jengo la ofisi ya Chama zimesimama kwa madai kwamba hakuna fedha wakati fedha zimetolewa miezi mitatu iliyopita,sisi tunataka ofisi yetu ijengwe kwakuwa tunafahamu fedha zipo na hatutaki usiri unaofanywa na Mbunge pamoja na Mwenyekiti ,"wamesema wanachama hao.
Wamesema kuwa,Wilaya ya Nyang'hwale ndiyo Wilaya pekee ambayo haina jengo jipya la ofisi ya CCM ndani ya Mkoa wa Geita ambapo zipo Wilaya mpya ambazo tayari zimejenga majengo mazuri yenye hadhi ya Chama Cha Mapinduzi.
Wamemuomba Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM )Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi kufuatilia kwa karibu na kufanya uchunguzi wa kina ili kujua kwanini jengo hilo halikamiliki wakati wapo viongozi wanachangia.
Hatahivyo,wamesema wanataka fedha zilizochangwa na Naibu Waziri Mkuu pamoja na michango kutoka kwa wadau wengine zitumike kukamilisha ofisi ya Chama Wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale Grace Kingalame amesema yeye hausiki na chochote huku akimtaka mwandishi wa habari atafute wahusika ili apate ufafanuzi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo John Isaka amesema kuwa yeye anashughulika na Halmashauri na kwamba akiulizwa swali linalohusu Halmashauri yupo tayari kujibu lakini suala la Chama ni vyema akatafutwa Katibu wa Chama Wilaya au mwenyekiti wa Chama Wilaya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyang'hwale Adam Mtore, alipopigiwa simu Kuulizwa juu ya jambo hilo hakuweza kuweka bayana kama fedha hizo zimetolewa aula lakini alichokisema ni kwamba ni kweli walimuomba kiongozi huyo awasaidie ujenzi wa jengo lao la ofisi ya Chama.
Mtore, amesema hajui chochote kuhusu fedha hizo lakini utoaji wa malalamiko katika Chama unautaratibu wake na mara nyingi uanza ngazi ya chini ya tawi lakini kwakuwa suala hilo linagusa ngazi ya Wilaya ilitakiwa wapeleke malalamiko yao kwa Katibu wa Chama Wilaya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyang'hwale Adam Mtore
Amesema, kama hawakuridhika ndipo upande ngazi ya juu kwa Katibu wa Mkoa lakini sio hilo tu,Chama kina Vyombo vyake vya kimaadili ambavyo vinaongozwa na Mwenyekiti na Katibu .
Amesema,kama wanaona kuna kitu kimeenda kinyume hata huko wanakotaka kwenda kwa Katibu Mkuu ambaye ndiye bosi na mtendaji Mkuu wa Chama atawauliza kama wamepita ngazi za Wilaya na mkoa kupeleka malalamiko hayo.
"Kama Kuna ishu unaona haijaenda sawa ukifika kwa Katibu wa Wilaya hamna ,si utaenda kwa Katibu wa CCM Mkoa na ukiona kama nae hajakutendea haki basi utaenda kwa Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi,"amesema Mtore.
Mtore, amesema Naibu Waziri Mkuu hakuahidi kutoa hela lakini aliahidi kusapoti ujenzi ,na ujenzi una kamati kwahiyo aliyekuambia kwamba Kuna hela sijui ngapingapi yeye amejuaje ? alihoji mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyang'hwale Hussein Nassoro Amar,ameeleza kusitikishwa na malalamiko ya wananchama hao huku akisema jambo hilo halina usiri wowote.
Amar,amesema kuwa wanavyosema yeye ana milioni 50 hakatai lakini jambo jema ni kwamba wangemuuliza yule aliyezitoa na kwamba ingekuwa bora sana kuliko kulalamika bila kuwa na ukweli.
"Kwasababu mimi ndiye niliyeomba atusaidie na sio maramoja na bahati nzuri alipokuja yenye mwenyewe pale nilimkumbushia ombi hilo na akakubali kusaidia lakini hakutamka kiwango,"amesema Amar
"Mwandishi,wewe waambie waende kwa Balozi Dkt.Nchimbi atawapokea na kuwasikiliza lakini kabla ya hapo si wangeenda kwanza kwa Naibu Katibu Mkuu Dotto Biteko awathibitishie? lakini najua hilo jambo la kisiasa na watu wanatengeneza Siasa japo muda wa miezi mitatu tu litakwisha,"amesema
Mbunge Amar ameongeza kuwa,kwasasa hawezi kujieleza sana kwasababu hizo ni kama tuhuma na zikifika kwa Dkt .Nchimbi ataitwa kwasababu Nchimbi ni bosi wake,anamuita,na atamuuliza Dkt Biteko.
Amesema, hakuna mahali Naibu Katibu Mkuu ametamka kutoa milioni 50 na kwamba hata yeye anazokumbukumbu sahihi kupitia Nyang'hwale TV kwakuwa siku hiyo walirekodi na wanaweza kurudia kuangalia hayo mazungumzo kwamba wapi alitamka kutoa milioni 50.
"Lakini mbali na hayo mimi kupewa, bwana fikisha hizi kupitia akaunti yangu kuna uharamu?halafu hilo la kusema fedha hizi zimepitishwa akaunti ya mbunge nadhani sio shida lakini shida inakuja pale wanaposema ninahujumu kwakuwa hii ni kashfa kwangu ,"amesema Mbunge huyo
Mbunge huyo ameongeza kuwa,yeye binafsi amekuwa na mchango mkubwa sana katika ujenzi wa ofisi hiyo ya Chama maana alishawai kutoa mashine zake na magari yake (Tipa) kufanyakazi katika ujenzi huo ,sasa nahujumu vipi ?
Lakini amesema kuwa kwasababu malengo yake ni kujenga ofisi ya Chama amekuwa akitafuta wadau kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale Grace Kingalame ambapo Kingalame amekuwa na mchango mkubwa sana katika usimamizi wa ujenzi wa jengo hilo lakini anashangaa kuambiwa eti wanamuhujumu Kingalame, kivipi? na ili afanywaje?
"Mimi sikatai nilipokea hizo fedha,lakini hao wanapozungumza alitoa ,hivi wanauhakika gani kama alitoa yeye? na je,kuna uharamu gani yeye kupewa au kuingiziwa fedha na Naibu Waziri Mkuu? Alihoji Mbunge Amar
Aidha,Amar amesema kuwa fedha hizo zilivyoingia na siku anazipokea alimpa taarifa Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Chama,Mwenezi,kamati ya Siasa,na kamati ya ujenzi na yeye ndiye aliyetafuta fundi na kuwashauri kuwa kuna fundi anaezeka banda lake kwahiyo ni vyema akatumika kwakuwa yupo vizuri.
Amesema hakuishia hapo, lakini siku moja akamwagiza yule fundi kwenda kuwapimia na akasema wakihitaji vifaa waseme kwakuwa yeye anapata vifaa Jijini Dar es Salaam kwa bei nafuu kuliko Mwanza.
"Kwahiyo nikawaambia mtakapokamilisha mniambie maana hela yenu ninayo,na hawajanielekeza niweke kwenye akaunti gani na kwasababu wananiamini mimi wakati wote,wanajua hela yao ipo salama mikononi mwangu na bahati nzuri nilisharipoti kwao na zaidi mimi sipo kwenye kamati ya ujenzi,"amesema
Mbunge huyo,amesisitiza kuwa baada ya mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kumuambia fedha hizo zipo tayari na ataingiziwa na yeye akachukua jukumu la kuripoti kwa viongozi wote na mpaka sasa wote wanajua.
"Lakini mimi ndiye niliyeomba ,mimi ndiye niliyezungumza nae,mimi najua tumetoka wapi na Biteko na hata katika mkutano Biteko aliwaambia tulikotoka na akasema, huyu ndiye mwenyekiti wetu wa wabunge wa Mkoa wa Geita na ndio maana hela ilipokuwa tayari akanipa kinoti akanielekeza niende wapi kuchukua ,"amesema
"Hela ipo mikono salama na hata leo (Mei 03,2025) nimeongea na Mkuu wa Wilaya kumweleza juu ya fedha zao kwamba zinatakiwa kufanyakazi iliyokusudiwa kwakuwa mimi sitaki kukaa na huo mzigo ,nipeni akaunti niwahamishie ,lakini Kingalame amesema atakaa na kamati yake ya ujenzi na akasema wakati huu aendelee kukaa nazo na wakihitaji kununua vifaa watamjulisha ili atoe hizo fedha",ameongeza Amar
Amesema kuwa jambo lolote la kufichiana Siri kati yake na Mwenyekiti wa CCM Wilaya halipo ndio maana baada ya kupata hela hizo alizungumza moja kwa moja ndani ya kikao cha kamati ya Siasa,kamati ya ujenzi na kuwapa njia sahihi za kupunguza gharama kwakuwa jengo hilo ni kubwa.
Amesema ,yeye na Mkuu wa Wilaya wapo vizuri na wanashirikiana vizuri na Nyang'hwale imetulia na ipo salama kwakuwa wanafanyakazi kwa kushirikiana na taasisi zote, idara zote ,ofisi ya mkurugenzi,ofisi ya DC, Chama na wananchama wake pamoja na Wananchi kiujumla.
Mwisho
Comments
Post a Comment