WAWEKEZAJI WA VIWANDA, MADEREVA MALORI ENEO LA ZEGERENI KIBAHA WALIA NA UBOVU WA BARABARA YA KINGLION ,WAMUOMBA RAIS SAMIA KUINGILIA KATI.
Na Gustaphu Haule,Pwani
WAWEKEZAJI wa Viwanda pamoja na madereva wa malori wanaotumia barabara ya Kinglion iliyopo eneo la viwanda la Zegereni katika Halmashauri ya Mji Kibaha wameshindwa kuendelea na uzalishaji kutokana na kukosa barabara ya kusafirishia bidhaa zao.
Hali hiyo imetokana na barabara hiyo ambayo wamekuwa wakiitumia mara kwa mara kuharibika vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kupelekea magari ya mizigo yanayosafirisha bidhaa kutoka katika Viwanda hivyo pamoja na yale yanayopeleka malighafi viwandani kushindwa kupita.
Kutokana na adha hiyo Wawekezaji wa Viwanda katika eneo hilo pamoja na wadau wengine wakiwemo madereva wa malori wameiomba Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwatatulia changamoto hiyo ili kuwa na uhakika wa kusafirisha bidhaa zinazozalishwa katika viwanda hivyo.
Lori la mizigo likiwa limenasa katika barabara hiyo likiwa linapeleka malighafi ya kutengenezea bati katika kiwanda cha Kinglion kilichopo eneo la viwanda la Zegereni katika Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani
Meneja wa kiwanda cha Dominick Milling Group Ltd kinachozalisha unga wa aina mbalimbali GoodLuck Patrice amewaambia Waandishi wa habari waliotembelea katika eneo hilo kuwa kwasasa wamesimamisha uzalishaji kwakuwa hawana barabara ya kupitisha bidhaa hiyo.
Patrice, amesema kuwa barabara hiyo ya Kilomita 2 inayojulikana kwa jina la Kinglion Road kwasasa ni mbovu kiasi ambacho magari ya mizigo hayawezi kupita kwani mengi yanayojaribu kupita hukwama.
Amesema, muda mrefu Serikali imetoa ahadi ya kuitengeneza kwa kiwango cha lami kwa ajili ya kuwasaidia Wawekezaji lakini mpaka leo hakuna lililofanyika licha ya kufanya jitihada kubwa za kufuatilia katika mamlaka mbalimbali zinazohusika .
"Barabara hii ya Kinglion yenye urefu wa Kilomita mbili kwasasa imesababisha kukwamisha shughuli zetu za uzalishaji kwakuwa tukizalisha hakuna sehemu ya kupitisha magari ya mizigo jambo ambalo linasabisha hasara kubwa,"amesema Patrice
Patrice, amesema kuwa kwa siku kiwanda chake kinauwezo wa kuzalisha tani za unga 50 na kwamba kinaposimama maana yake uzalishaji huo unakwama na hivyo kupelekea hasara kubwa huku akiendelea kumuomba Rais Samia kuona namna ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya barabara hiyo.
Meneja wa kiwanda cha Dominick Milling Group Ltd GoodLuck Patrice akiwaeleza Waandishi wa habari juu ya adha wanayoipata kutokana na ubovu wa barabara ya Kinglion yenye urefu wa Kilomita 2. katika eneo la viwanda Zegereni Kibaha Mjini
Nae George Ally, ambaye alikutwa gari lake limekwama katika barabara hiyo ameeleza adha wanayoipata katika barabara hiyo huku akisema uwekezaji katika eneo hilo bila kuwa na barabara nzuri uenda mipango yao ya uwekezaji ikashindwa kufikia malengo.
Ally, amewaambia Waandishi wa habari kuwa wao ni Wawekezaji ambao wamekuja katika eneo la Zegereni kujenga kiwanda tangu miezi mitatu iliyopita lakini adha waliyokutananayo ni kuwepo kwa barabara mbovu ambayo inawapelekea kukwama mara kwa mara.
Amesema ,hali hiyo inakatisha tamaa kwakuwa mpaka sasa wanashindwa kupitisha malori ya vifaa vya ujenzi huku akisema ujenzi wa kiwanda katika eneo hilo uenda ukasimama.
Ally, ameiomba Serikali ya awamu Sita kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya barabara katika eneo hilo ili kusudi waweze kujenga viwanda ambavyo vitasaidia kuliingiza Taifa mapato lakini pia hata kuzalisha ajira kwa Watanzania.
"Sisi ni Wawekezaji katika eneo hili la Zegereni lakini barabara tunayoitumia ni hii ya Kinglion ambayo ni mbovu na haipitiki,tuna miezi mitatu sasa tangu tuanze kuja huku kujenga kiwanda lakini barabara mbovu na tunakwama kila siku kama ambavyo mnaona hapa,"amesema Ally
Dereva wa Malori ya mizigo anayetumia barabara hiyo Issa Mohamed,amesema kuwa kwasasa amesimama kufanyakazi kwakuwa barabara hiyo haipitiki na kwamba mara ya mwisho alikuwa anasafirisha saruji kwa ajili ya kwenda katika eneo hilo katika shughuli za viwanda lakini alikwama siku tatu katika barabara hiyo.
Lori la mizigo likiwa limenasa katika barabara ya Kinglion iliyopo eneo la viwanda la Zegereni Kibaha Mjini Mkoani Pwani
Kwa upande wake Patrick Mapori, dereva wa gari la mizigo amesema kuwa barabara ya Kinglion imekuwa ikikwamisha shughuli za uwekezaji kwakuwa wapo madereva wanaoitumia kuleta malighafi na wengine kuchukua bidhaa viwandani na kupeleka sokoni lakini kipindi cha mvua barabara hiyo haipitiki.
"Bila kuwa na miundombinu mizuri ya barabara ni wazi kuwa hakuna uwekezaji imara,tunaomba Serikali hii ya Mama Samia ijenge barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuendelea kuwavutia Wawekezaji ambao watatoa ajira kwa vijana na hata kuchangia pato la Taifa,"amesema Mapori.
Hatahivyo,Machi mwaka huu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango, na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo alifanya ziara ya kutembelea kiwanda cha Kinglion ambapo moja ya changmoto aliyoipokea kiwandani hapo ni ubovu wa barabara hiyo.
Club News Editor


_1.jpg)

Comments
Post a Comment