SPIKA WA BUNGE DKT.TULIA ACKSON AWAANGUKIA WATANZANIA KUULINDA MUUNGANO KWAKUWA NDIO KIELELEZO CHA AMANI NA UTULIVU
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson amewataka Watanzania kuendelea kuulinda Muungano wa Tanzania kwakuwa ndio kielelezo cha amani na utulivu.
Dkt. Ackson ambaye pia ni Rais wa 31 wa Jumuiya ya mabunge duniani ametoa kauli hiyo Aprili 25 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa Serikali pamoja na wananchi katika katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Kibaha Shopping Mall.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Aprili 25 katika viwanja vya soko kubwa la Kisasa ( Kibaha Shopping Mall); lililopo katika Manispaa ya Kibaha Mjini baada ya kutembelea kiwanda cha Tanzania Biotech Products Ltd na kukagua mradi wa soko hilo.
Dkt.Tulia amefanya ziara hiyo katika Manispaa ya Kibaha Mjini ikiwa ni sehemu ya kuelekea katika Maadhimisho ya Siku ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika Aprili 26, 2025 ambapo awali amefika katika kiwanda cha kutengenezea dawa za viuadudu wa mazalia ya mbu (Tanzania Biotech Products Ltd) kilichopo katika Manispaa ya Kibaha Mjini na kupokea changamoto mbalimbali.
Amesema kuwa Muungano wa Tanzania umekuwa na mafanikio makubwa kwani kielelezo cha kwanza ni kuendelea kuwa kisiwa cha amani duniani na kwamba lazima Muungano huo ulindwe kwa nguvu zote.
Dkt.Tulia amesema kuwa wakati Tanzania inasherehekea siku ya Muungano ni vyema pia wakakumbukwa waasisi wa Muungano huo akiwemo Shekhe Amani Abeid Karume na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambao wamefanyakazi kubwa mpaka hapa tulipo.
Wananchi Kibaha Mjini pamoja na wafanyakazi wa Manispaa ya Kibaha Mjini wakimsikiliza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Kibaha Shopping Mall leo Aprili 25, 2025.
Amesema, Tanzania tunasauti moja na tunaheshimika duniani na kwamba hata cheo chake cha Urais wa mabunge ya duniani ni kudhihirisha amani na kwamba sio rahisi kupata nafasi hizo kama nchi haina amani.
"Hizi nafasi kubwa za uongozi tunazopata duniani ni kwasababu ya kuwepo kwa amani kama hakuna amani sio rahisi kuchaguliwa wala kuteuliwa na kwahiyo Watanzania tusijidharau tuendelee kuulinda Muungano wetu," amesema Ackson
Dkt.Ackson ameongeza kuwa mafanikio yote yaliyopatikana yanatokana na Muungano pamoja na ushirikiano mkubwa kati ya Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi.
"Kazi nzuri inafanywa na Rais Samia pamoja na Rais Mwinyi ndio maana yale yanayofanyika Zanzibar na Bara yanafanyika vile vile lakini hayo yote ni kutokana na Muungano kuwa imara ambao unasababisha biashara zifanyike vizuri na hivyo uchumi kukua," amesema Ackson
Kuhusu masuala ya uchaguzi Dkt.Tulia amesema kuwa wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani jambo la kwanza kulieleza lilikuwa kuhusu amani na kwamba Bunge lilichukua hatua ya kurekebisha baadhi ya vifungu vya sheria.
Amesema mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi lakini mwaka jana Bunge lilisikiliza maoni ya wadau mbalimbali na kisha kufanya mabadiliko katika baadhi ya vifungu vya sheria vya uchaguzi lengo likiwa ni kuimarisha amani na utulivu katika uchaguzi ambapo amewataka wadau kusoma Sheria hizo.
Aidha Dkt. Tulia ameipongeza Manispaa ya Kibaha Mjini kwa Uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa soko la Kisasa la Kibaha Shopping Mall kwakuwa mradi huo unakwenda kuimarisha mapato ya Halmashauri,Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson wa pili kutoka kulia akikagua mradi wa soko la Kisasa (Kibaha Shopping Mall) leo Aprili, 25 alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kuelekea katika Siku Muungano na wa kwanza ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Mjini Dkt . Rogers Shemwelekwa.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson akiwa katika duka maalum (Super Market ) ndani ya Kibaha Shopping Mall Mkoani Pwani alipofanya ziara leo Aprili 25,2025 ya kutembelea soko hilo lililopo katika Manispaa ya Kibaha Mjini
Amesema pongezi hizo lazima ziende kwa Rais wa awamu ya Sita Dkt .Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba amezitaka Halmashauri nyingine kujifunza kutoka Manispaa ya Kibaha Mjini.
Awali Dkt.Tulia alifanya ziara ya kutembelea katika kiwanda cha kutengenezea dawa ya viuadudu vya mazalia ya mbu kilichopo katika Manispaa ya Kibaha Mjini na kupokea changamoto mbalimbali ambapo ameahidi kuzifanyiakazi changamoto hizo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson wa kwanza (kushoto) akiwa katika kiwanda cha Tanzania Biotech Products Ltd kilichopo katika Manispaa ya Kibaha Mjini kwa ajili ya kukagua na kujionea maendeleo ya kiwanda hicho April 25, 2025.
Kiwanda cha uzalishaji wa dawa za viuadudu wa mazalia ya Mbu Cha Tanzania Biotech Products Ltd kilichopo katika Manispaa ya Kibaha Mjini
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete, amewapongeza waasisi wa Muungano ambao unaunganisha Tanzania Bara na Zanzibar huku akiahidi kuulinda Muungano huo sambamba na kuwasihi wanaPwani kutumia fursa ya Muungano huo katika kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka,amesema kuwa yaliyofanyika Kibaha Mjini ni makubwa hasa katika miradi ya huduma za jamii.
Koka, amesema kuwa kila jambo limetekelezwa kwa asilimia kubwa ndio maana leo wanafuraha ya kusherehekea Muungano huku akiwaomba Wananchi wa Jimbo la Kibaha Mjini kuendelea kushirikiana kwa ajili ya kuhakikisha Kibaha inakua zaidi kimaendeleo.
"Siku ya Muungano ni kumbukumbu nzuri na ni siku maalum ya kuwakumbuka waanzilishi wa Muungano lakini kikubwa zaidi ni kuona ilani ya CCM imetekelezwa vizuri na mambo mengi yanaonekana yamekamilika katika kipindi hiki cha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,"amesema Koka.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema kuwa Rais Samia amekuwa na maono makubwa na ndiye mchapakazi hodari na mkoa wa Pwani umenufaika na uchapakazi wake kwakuwa tangu aingie madarakani Pwani imepokea kiasi cha Sh.Trilioni 1.53 za miradi ya maendeleo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza Leo katika mkutano uliofanyika katika soko la Kisasa la Kibaha Shopping Mall ikiwa ni ziara ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson
Kunenge, amesema Mkoa wa Pwani mpaka sasa unajumla ya viwanda 1,553 ambapo kati ya hivyo Viwanda vikubwa ni 128 na tangu Rais Samia aingie madarakani tayari Viwanda vikubwa 78 vimejengwa.
Kunenge amesema kuwa Mkoa wa Pwani hauwezi kumlipa Rais Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya lakini ameahidi wakati wa uchaguzi Rais kushinda kwa kishindo ili aweze kuwatumikia zaidi ya Watanzania.
Hatahivyo, katika ziara hiyo ya Dkt .Tulia viongozi wengine waliokuwepo ni pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Mjini Dkt . Rogers Shemwelekwa na watumishi wengine.
MWISHO.
Comments
Post a Comment