CPA MAKALLA AWAOMBA WATANZANIA KUSIMAMA NA RAIS SAMIA
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi, Siasa na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) CPA Amos Makalla, amewaomba Watanzania kuhakikisha wanasimama na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Makalla, ametoa kauli hiyo Aprili 23, 2025 wakati akifungua mkutano mkuu maalum wa Jimbo la Kibaha Mjini lililopo Mkoani Pwani uliokuwa unahusu uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2020/2025 chini ya mbunge Silvestry Koka.
Makalla, amesema kuwa Rais Samia ni kiongozi mahiri na mpenda maendeleo ambaye toka aingie madarakani amekuwa Rais wa kwanza kuvunja rekodi ya kutoa fedha za miradi ya maendeleo kuliko awamu zote zilizopita.
"Nawaomba Watanzania wasimame na Dkt.Samia Suluhu Hassan maana amevunja rekodi ya kuwa Rais wa kwanza kutoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuliko awamu zote zilizopita," amesema Makalla
Makalla, amesema Rais Samia amefanyakazi kubwa ya kuiletea maendeleo Tanzania halafu anatokea mtu mmoja anasema Rais hakufanya kitu wakati wengi wao wanamheshimu Dkt.Samia ambapo amesema watu kama hao wapingwe kwa nguvu zote.
"Yaani Rais huyu amefanyakazi kubwa Kwa kipindi kifupi alichokaa madarakani na amegusa kila sekta na sote tumeona halafu anatokea tu mtu mmoja anasema Rais Samia hakufanya kitu,loooh!mtu wa namna hiyo lazima apingwe kwa nguvu zote ,"ameongeza Makalla
Aidha, katika mkutano huo Makalla amesema kuwa mwaka huu CCM imekuja na utaratibu mpya wa kuongeza wigo wa wapiga kura katika uchaguzi wa kura za maoni na moja ya wajumbe ni mabalozi.
Amesema katika mchakato huo, Makalla amesema kuwa, wagombea wote watachukua fomu lakini watateuliwa watatu na kisha mkutano Mkuu wa Jimbo kupiga kura za maoni kwa ajili ya kumpata mgombea mmoja ambaye atapewa ridhaa ya chama.
Amesema kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kupunguza makundi katika kipindi cha uchaguzi huku akiwasisitiza wagombea wanaotroti wawe na nidhamu kwakuwa wanaweza kutroti sana lakini wasiteuliwe.
Makalla, amesema kuwa baada ya kura za maoni wanachama washikamane ili CCM iendelee kuwa imara tofauti na vyama vingine huku akitolea mfano Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) kinavyovurugana baada ya uchaguzi wao.
Ameongeza kuwa, miaka kadhaa mbele Chadema kitakuwa kama jukwaa la wanaharakati kwakuwa wao wenyewe ndio wanaokivuruga huku akisema hataki kuona hali hiyo inajitokeza CCM.
"Hapa namaanisha kampeni za CCM ziwe za kistaarabu hasa katika uchaguzi wa ndani wa kura za maoni ili kudhihirisha Umma CCM ni Chama kikubwa na kura za maoni zitakazofanyika sasa ziendelee kuimarisha chama na kukifanya kishike dola 2025," amesema Makalla
Aidha, Makalla akiwa katika mkutano huo amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka kwa kazi nzuri aliyoifanya na namna ambavyo ameipambania Kibaha Mjini katika suala la maendeleo.
Makalla amewaomba wanaCCM pamoja na wananchi wa Kibaha Mjini kiujumla kuendelea kushirikiana na mbunge huyo ili kusudi Jimbo la Kibaha Mjini liweze kusonga mbele zaidi kimaendeleo.
Kwa upande Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amemshukuru Makalla kwa kujitoa kwake na kushiriki pamoja na wanachama wa Kibaha Mjini huku akisema yupo tayari kuendelea kushirikiana na WanaKibaha katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Koka, amesema kuwa Kibaha Mjini imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kupata Manispaa na mafanikio hayo yametokana na nguvu kubwa za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa utoaji fedha za miradi ya maendeleo.
"Binafsi nitumie nafasi hii kumshukuru Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoifanya na hata sisi hapa Kibaha Mjini tumepata mafanikio kutokana na wepesi wake wa kutuletea fedha za miradi kwa wakati , kwahiyo lazima tumuunge mkono juhudi zake ,", amesema Koka
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka, amesema kuwa Ilani ya CCM Kibaha Mjini imetekelezeka Kwa asilimia 87 na kazi hiyo imefanywa na Rais Samia , Mbunge na Madiwani.
Hatahivyo , mikutano ya kuwasilisha utekelezaji wa ilani ya CCM Kibaha Mjini bado inaendelea kufanyika kwa kujumuisha Kata tatu kila siku na inatarajia kukamilika Aprili 27 mwaka huu .
Mwisho
Comments
Post a Comment