HALMASHAURI KUU YA CCM KIBAHA MJINI YAMWAGIA SIFA MBUNGE KOKA UTEKELEZAJI WA ILANI 2020/2025.
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor
WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kwa pamoja wameridhishwa na utekelezaji wa ilani uliofanywa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka katika kipindi cha mwaka 2020 /2025.
Mbali na Koka lakini pia wajumbe hao hawakusita kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa maendeleo aliyekubali kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Kibaha Mjini.
Kauli ya wajumbe kuridhishwa na Koka imekuja mara baada ya mbunge huyo kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa ilani ya CCM ya Mwaka 2020/2025 katika kikao kilichofanyika April 16, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.
Koka, amewasilisha taarifa hiyo ikiwa imegusa sekta mbalimbali ikionyesha kuwepo kwa mafanikio makubwa hususani katika kuimarisha, kujenga na kuboresha miundombinu katika Afya, Elimu, Barabara, Maji na hata katika sekta nyingine.
Akizungumza mara baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Koka amesema kuwa katika kipindi hicho mambo mengi yamefanyika huku akisema yaliyowasilishwa katika kikao hicho ni machache kwakuwa angeyaweka yote ni wazi kuwa wangekesha ukumbini hapo.
Koka, amesema mafanikio hayo yamepatikana kwa ushirikiano mkubwa uliofanyika baina yake na viongozi wa CCM katika Kata zote sambamba na Madiwani ambao walikuwa wanasimamia kikamilifu katika maeneo yao.
Koka, amesema katika mafanikio hayo huwezi kumuacha nyuma kinara wa maendeleo nchini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha miradi yote ya Kibaha Mjini inapata fedha na kutekelezwa kwa wakati.
Koka amewaomba wanaCCM na viongozi wote kuendelea kushirikiana ikiwa pamoja na kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ili kusudi waweze kufanya makubwa katika kipindi kijacho.
"Nawashukuru viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Madiwani na hata wanachama wote kiujumla kwa kuungana nami na Rais Samia katika utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi cha mwaka 2020/2025 kwa hakika mnajua mambo mengi yamefanyika na ninyi ni mashahidi hivyo nawaomba tuendelee kushirikiana zaidi," amesema Koka.
Diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi amesema kuwa ameipokea taarifa hiyo huku akisema Mbunge amefanyakazi kubwa na anapaswa kupongezwa kwa kazi aliyoifanya.
Lutambi, kwa niaba ya Madiwani wenzake amesema kuwa Koka amefanya mambo makubwa na hata katika uwasilishaji wa taarifa yake mambo mengi hakuyataja japo kayafanya hivyo ni wakati wa kwenda kuyasema kwa Wananchi yale yaliyofanyika ili kusudi chama kizidi kushika dola katika chaguzi zijazo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha ambaye pia ni diwani wa Kata ya Sofu Musa Ndomba, amesema kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na baraza la Madiwani ambao ndio walikuwa wanapambana kuhakikisha fedha hizo zinakwenda katika miradi.
Ndomba, amesema kutokana na juhudi za madiwani hao atafurahi kuona Madiwani wote wanarudi katika baraza hilo ili kuhakikisha wanaendelea kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo na kufanya Wananchi kupata huduma bora zaidi.
Mjumbe wa kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Alhaji Musa Mansour amesema kuwa maendeleo hayana chama na kwamba Koka amefanya vizuri lazima apongezwe na ikiwezekana mambo ya msingi lazima yasemwe kiufasaha.
Mansour, amesema kuwa kwenye jambo la maendeleo hakuna kubezana lakini kinachotakiwa ni kuungana kwa pamoja na kutengeneza umoja wa chama na ikibidi washuke chini kuzungumza na watu juu ya maendeleo yaliyopatikana.
"Nina mpongeza mbunge Koka,Rais na Madiwani na kiukweli maendeleo hayana chama na katika hili niwaombe wajumbe tumpigie makofi mbunge kwani hatuwezi kubeza maendeleo,"amesema Mansour akiwa katika kikao hicho
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka akihitimisha kikao hicho amesema kuwa Kibaha Mjini wamefanikiwa kutekeleza ilani kwa asilimia 87 na kwamba kilichoonyeshwa katika taarifa hiyo ni sehemu ya mafanikio ya miaka mitano ya Mbunge,Rais na Madiwani.
Nyamka, amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa wasikubali kupokea maneno ya mitandaoni yanayotolewa na vijana wanaotumika kukichafua chama kwani kufanya hivyo sio kama wanamchafua Koka bali wanakichafua Chama Cha Mapinduzi ( CCM).
Hatahivyo, Nyamka amewataka viongozi hao waende kuwaambia vijana hao mambo mazuri yaliyofanywa na CCM Kibaha Mjini kupitia Mbunge wake Silvestry Koka na badala yake waache kuwatumia vijana kwa mambo ambayo hayana maslahi kwa Chama.
MWISHO
Comments
Post a Comment