DKT.BITEKO AWATAKA WATANZANIA KUTOGAWANYIKA WAKATI WA UCHAGUZI MKUU
Na Gustaphu Haule
NAIBU Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi kutogawanywa kwa itikadi ya dini, ukabila na siasa katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Ubunge na Udiwani.
Dkt. Biteko amesema hayo Aprili 23, 2025 Wilayani Monduli mkoani Arusha wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika Kijiji cha Esilalei.
“ Ninatamani kuona hatugawanywi na mtu yoyote wala hatuwekwi kwenye makundi ya dini wala ukabila,kwahiyo niwaombe wananchi wa Monduli pendaneni na shirikianeni na uchaguzi utakapofika chaguaneni kwa haki,” amesema Dkt. Biteko.
Amewataka wananchi wa Monduli kuutunza mradi huo wa maji wa Esilalei huku akiipongeza Wizara ya Maji na RUWASA kwa kusimamia mradi huo mzuri na wa uhakika.
Pia, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapenda wananchi wa Monduli na inawapongeza kwa uchapakazi wao kwenye kilimo na ufugaji.
Aidha, amewataka wachape kazi na kuwa Rais Samia amefikisha mradi huo wa maji kwa kuwa anapenda pia mifugo yao istawi,vilevile amesema kuwa Rais amemtuma kuwahakikishia wananchi hao kuwa wafugaji nchini wanakuwa daraja la juu kama walivyo wananchi wengine.
Aidha, amesema wananchi hao wanachohitaji ni Serikali tu iwapatie nyenzo kama maji, umeme na barabara ili kufanikisha shughuli zao ambapo tayari Rais Samia ameapa kuwapatia nyenzo hizo.
Kuhusu umeme, Dkt. Biteko amesema kuwa vijiji vyote vya Wilaya ya Monduli vimepata umeme na katika vitongoji 236, vitongoji 72 vimepata umeme na vilivyosalia vitapata huduma hiyo mara baada ya Uchaguzi Mkuu.
Akijibu ombi la Mbunge wa Monduli, Freddy Lowasa “ Nguzo za umeme 20 alizoomba Mhe. Mbunge kuanzia Alhamisi hadi wiki inayokuja tutaanza kuona watu wa hapa wanapata umeme bila masharti yoyote, katika maisha tunapimwa kwa kazi si kwa maneno,”
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amezungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusema kuwa Muungano huo wa miaka 61 ni wa kipekee duniani kwa kuwa mataifa kadhaa yamejaribu kuungana lakini yameshindwa. Aidha, Tanzania imeendelea kubaki Taifa moja lenye amani.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Dkt. Steven Kiruswa amefurahishwa kwa Wilaya hiyo kupata maji na kusema kuwa maji ni uhai, hivyo anamshukuru Rais Samia kwa kusaidia pia mifugo kupata maji.
Mbunge wa Monduli, Freddy Lowasa amesema kuwa kazi aliyofanya Rais Samia wilayani humo ni kubwa kwa kuwa huduma ya maji ilikuwa changamoto kubwa kwao.
“ Kwa miaka mingi maji yamekuwa kero kubwa katika Wilaya yetu kwa kupata mradi huu tunaomba umpelekee shukrani zetu Rais Samia,” amesema Lowassa.
Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Monduli, Mhandisi Naville Msaki amesema kuwa mradi huo ulisanifiwa mwaka 2021 utahudumia wananchi 8,867 na mifugo 24,000 hadi sasa umefikia asilimia 96 na hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 2.7.
*#KazinaUtuTunasongaMbele*
Comments
Post a Comment