CPA AMOS MAKALLA : VIONGOZI ACHENI KUWABEBA WAGOMBEA MIFUKONI MKEKA UTACHANIKA
Na Gustaphu Haule,Pwani
KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi ( CCM),CPA Amos Makalla amewapiga marufuku viongozi wa chama wanaowahakikishia ushindi watia nia wa ubunge na udiwani kuacha maramoja tabia hiyo kwakuwa wao sio waamuzi wa mwisho.
Aidha, Makalla amezitaka kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa kuacha kubeba wagombea wao mfukoni kwakuwa kufanya hivyo kunachangia kuwanyima haki wanachama wengine wenye nia ya kugombea katika nafasi hizo.
Makalla ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano mkuu maalum wa Jimbo la Kibaha Mjini uliofanyika April 23, 2025 juu ya uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani katika kipindi cha mwaka 2020 / 2025 chini ya mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka.
CPA Amos Makalla Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) akisalimia wajumbe wa Mkutano
Amesema kuwa, wapo viongozi wanatembea na orodha ya wagombea wa ubunge na udiwani huku wakiwahakikishia kuingia katika tatu bora ambapo amesema waache kufanya hivyo kwakuwa hawana maamuzi ya mwisho.
Ameongeza kuwa kufanya hivyo ni sawa na mchezo wa kubahatisha (Betting) ambao siku ya mwisho mkeka unaweza kuchanika na ukakosa la kumwambia mgombea na hivyo kutafuta sehemu ya kujificha.
Amesema, CCM ni chama imara na kipo makini na kwamba mwaka huu chama kitateua wagombea wazuri na makini wenye kukubalika na Wananchi huku akisisitiza baada ya kura za maoni ni vyema wanachama wakashikama ili CCM iendelee kuwa imara.
"Mwaka huu chama kimekuja na uratibu mzuri utakaohakikisha wagombea watakaoteuliwa wanakubalika,sasa wewe ukiendelea kuwaahidi kwamba nafasi ya ubunge una uhakika nayo halafu mwisho wa siku mgombea wako akakosa utatafuta mahali pakujificha,"ameongeza Makalla.
Makalla katika hatua nyingine amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuiletea maendeleo Kibaha Mjini.
Amemtaka Mbunge huyo kuendelea kufanyakazi ya kuwatumikia wananchi kwakuwa bado muda upo wa kufanya hivyo na kwamba kama kuna watu wanajipitisha bila utaratibu ni wazi kuwa wanapoteza muda wao bure.
"Nimeona katika taarifa yako ya utekelezaji wa ilani ya CCM umeitendea haki kwa kugusa kila sekta lakini pia hata Wananchi wako nimewasikia wakizungumza vizuri basi niseme inshallah Mungu akusaidie,"amesema Makalla
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi, Siasa, na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) CPA Amos Makalla (Kushoto )na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (Kulia) katika mkutano Mkuu maalum wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM Jimbo la Kibaha Mjini katika kipindi cha mwaka 2020/2025 uliofanyika leo April 23,2025 Makalla alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo hilo Silvestry Koka amesema kuwa Kibaha Mjini ipo salama na kwamba katika kipindi cha miaka mitano mambo mengi na makubwa ya kimaendeleo yamefanyika Kibaha Mjini licha ya kuwa mengi hayakuoneshwa katika dokumentari.
" Kibaha Mjini imetoka mbali tangu ikiwa Mamlaka ya Mjini Mdogo na sasa tumepata Manispaa hivyo ni jambo la kujivunia lakini pia zipo huduma nyingi zimeimarika na zitazidi kuimarika kwakuwa Serikali ni sikivu na inafanyakazi kubwa ya maendeleo.
Koka, amesema yapo maeneo ambayo hayakuwa na zahanati lakini kwasasa Zahanati zimejengwa ikiwemo ya Mtaa wa Saeni Kata ya Misugusugu,ujenzi wa Shule mbalimbali za Msingi na Sekondari,umeme umefika kila sehemu,Maji na barabara .
Amesema kuwa,kwa upande wa barabara kwasasa Kibaha Mjini imepata bahati ya kuwa na mradi wa Tact ambao utakwenda kujenga barabara za Mitaa Kwa kiwango cha lami mpango ambao unatarajia kuanza mwaka huu.
Hatahivyo,Koka ameahidi kuendelea kushirikiana na wanachama pamoja na Wananchi wote wa Kibaha Mjini ili kuhakikisha Kibaha inazidi kusongambele katika suala la maendeleo.
Comments
Post a Comment