SERIKALI KUTENGENEZA SERA YA UINGIZAJI MAGARI NCHINI, MAGARI MABOVU HAYATARUHUSIWA TENA.
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor - Charles Kusaga
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ipo mbioni kutengeneza sera ya magari ambayo itazuia uingizaji wa magari chakavu hapa nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo ametoa kauli hiyo Machi 26, 2025 mbele ya Waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuunganisha magari cha GF Vehicle Assemblers Limited kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo wa pili kutoka kulia akitembelea kiwanda cha GF Vehicle Assemblers Limited kilichopo Kibaha eneo la Tamco alipotembelea Machi 26,2025 kujionea maendeleo ya kiwanda hicho.
Kiwanda hicho kilichopo eneo la Tamco- Kibaha Mjini kinaunganisha magari makubwa ya mizigo aina ya FAW yenye uwezo wa kubeba mzigo tani 30.
Akiwa katika kiwanda hicho Profesa Mkumbo, amesema kuwa sasa hivi Tanzania mtu anaruhusiwa kuingiza magari hata kama lina miaka 50.
Amesema, magari hayo yanayoingizwa nchini mengi yanakuwa mabovu na kwamba ili viwanda vya magari vilivyopo nchini viweze kwenda mbali lazima kuja na sera ambayo itazuia uingizaji wa magari chakavu.
Kuwepo kwa sera hiyo pia itasaidia watu wote waliokuwa wanaingiza magari mabovu kutoka nje wanunue magari hayo kutoka Tanzania ambayo yatakuwa mazuri,mapya na ubora unaotakiwa.
"Changamoto ya kuingizwa magari mabovu tumeichukua na Serikali kupitia kituo cha Uwekezaji nchini ,(TIC) tutahakikisha changamoto hiyo inasimamiwa na kupatiwa ufumbuzi,", amesema Mkumbo.
Aidha, Mkumbo amekipongeza kiwanda hicho kwakuwa na maendeleo mazuri kwani mwaka 2020 walianza na magari 100 na sasa wamepiga hatua kubwa mpaka kufikia magari 3004 katika kipindi kifupi.
Kikao cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na uongozi wa kiwanda cha GF Vehicle Assemblers Limited kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema, Uwekezaji wa kiwanda hicho kwa hatua ya awali ilikuwa na mtaji wa bilioni 10 na sasa mtaji huo umekuwa zaidi kiasi ambacho kimepelekea kuzalisha magari mengi huku kikisaidia kutoa ajira kwa Watanzania 220.
Amesema, kazi ya Serikali ni kuendelea kusaidia kupitia kituo cha Uwekezaji (TIC) katika eneo la Viwanda na biashara ambapo lengo la Serikali ni kuhakikisha Viwanda vinakuwa vingi zaidi hapa nchini.
"Nimefika kukagua kiwanda hiki na kuona maendeleo yake lakini niseme tu,nimefurahi kuona kuna mipango na hatua ya tatu ya kuboresha magari kwa kuleta vifaa halafu gari nzima likiwa linatengenezwa kiwandani hapa,",amesema Mkumbo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo akikagua magari yanayounganishwa katika kiwanda cha GF Vehicle Assemblers Limited cha Kibaha Mkoani Pwani Machi 26,2025.
Mkumbo, amesema kuwa kwa niaba ya Watanzania kupitia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ina mipango mikubwa ya kuendelea kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na Viwanda vyakudumu.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Ezra Mereng, amemshukuru Waziri Mkumbo pamoja na timu yake kutoka kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania (TIC) kwa namna ambavyo wamesaidia kiwanda hicho kufikia mafanikio yaliyopo hivi sasa.
Mereng, amesema kuwa kupitia kiwanda hicho, vijana wakitanzania wanaweza kuunganisha magari kwa viwango vya kimataifa huku ndoto za kiwanda hicho ni kuunganisha magari makubwa na madogo.
Hatahivyo, Mereng ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt.Samia kupitia kituo cha Uwekezaji (TIC) kwakuwa imekuwa pamoja tangu mwanzo wa kuanza uzalishaji mpaka kufikia uwezo wa kuunganisha magari 3000 na kwamba malengo ni kuhakikisha Watanzania wote wananunua magari kiwandani hapo.
Comments
Post a Comment