RAIS SAMIA AWAFUTURISHA YATIMA PWANI, NI UTARATIBU WAKE WA KILA MWAKA
Na Gustaphu Haule,Pwani
Club News Editor
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewafuturisha zaidi ya watoto yatima 400 na wale waishio katika mazingira magumu kutoka katika Wilaya tofauti za Mkoa wa Pwani .
Rais Samia amewafuturisha watoto hao Machi 9,2025 katika viwanja vya Ikulu ndogo ya Mkoa wa Pwani ambapo katika iftari hiyo Rais Samia amewakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.
Akizungumza katika iftari hiyo Kunenge amesema kuwa Rais Samia amekuwa na tabia ya kila mwaka kukaa na watoto yatima katika mwezi mtukufu na kuwaandalia futari na kwamba mwaka huu ni mara yake ya nne.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika hafla fupi ya iftari iliyofanyika Machi 9,katika viwanja vya Ikulu ndogo ya Mkoa wa Pwani, Iftari hiyo imetolewa na Rais Samia kwa watoto yatima.
Kunenge, amesema kuwa katika futari hiyo Rais Samia angependa kuungana pamoja na watoto hao lakini kulingana na majukumu yake imebidi amwakilishe katika kutimiza adhma yake.
"Futari hii imeandaliwa na Rais Samia kwa ajili ya watoto yatima na hata wale wanaoishi katika mazingira magumu na alipenda kuwa mahali hapa lakini kutokana na majukumu yake kuwa mengi imebidi mimi nimwakilishe "amesema Kunenge
Viongozi wa dini na Serikali wakiwahudumia futari watoto yatima katika hafla iliyofanyika Machi 9,2025 katika viwanja vya Ikulu ndogo iliyopo Kibaha Mjini.
Aidha, Kunenge amewaomba watoto hao pamoja na washiriki wengine katika iftari hiyo kuendelea kumuombea Rais ili aweze kuwa na afya njema ya kulitumikia Taifa na watu wake.
Katika hatua nyingine, Kunenge amesema kuwa mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi hivyo ni vyema Wananchi wakajitokeza kupiga kura ili kuwachagua viongozi wazuri watakaoongoza nchi sambamba na kuiletea maendeleo.
Mbali na hilo lakini pia Kunenge ametumia nafasi hiyo kuwaambia Wananchi wa Mkoa wa Pwani kuwa Mkoa wa Pwani umepata heshima ya kuwa mwenyeji katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025.
Watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu wakiwa katika Iftari iliyoandaliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Machi 9,2025 katika viwanja vya Ikulu ndogo iliyopo Mjini Kibaha .
Kunenge,amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi wa Mwenge huo yamekamilika na utazinduliwa katika viwanja vya Shirika la Elimu Tumbi Kibaha huku akiwaomba wananchi kujitokeza katika hafla hiyo kubwa ya Kitaifa.
Kwa upande wake Shekhe Mkuu wa Mkoa Hamis Mtupa, amemshukuru Rais Samia pamoja na Mkuu wa mkoa wa Pwani kwa kuona umuhimu wa kuandaa Iftari kwa watoto hao
Mtupa,amesema kuwa wadau wengine wanapaswa kumuombea Rais Samia kwa jambo hilo kubwa analofanya huku akiwaomba wadau hao kuiga mfano huo ambao unawaunganisha Wananchi na Jamii nzima .
Mtupa, amesema kuwa Bakwata Mkoa wa Pwani wameunga mkono jambo hilo kwani tayari mpaka sasa wametoa futari kwa taasisi 35 zilizopo katika Wilaya zote za Mkoa wa Pwani huku akisema wataendelea kufanya hivyo kulingana na michango ya wadau itakavyokuwa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge watatu kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini ya kiislamu mara baada ya iftari iliyofanyika Machi 9,2025 katika viwanja vya Ikulu ndogo iliyopo Kibaha Mjini.
Hatahivyo, katika iftari hiyo watoto yatima pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu walifanya Dua Maalum ya kumuombea Rais Samia.
Mwisho
Comments
Post a Comment