PROFESA KITILA MKUMBO ASEMA BIDHAA ZA KINGLION ZINAITANGAZA NCHI KIMATAIFA,AAHIDI KUTOA USHIRIKIANO KWA WAWEKEZAJI.

Na Gustaphu Haule,Pwani
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema vifaa vya ujenzi vinavyozalishwa hapa nchini vinajitosheleza na kwamba hakuna sababu ya watanzania kuendelea kununua vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
Aidha, Mkumbo amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia kwenye uwekezaji wa viwanda ili viweze kulipa wafanyakazi kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Mkumbo ameyasema hayo Mjini Kibaha alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua uzalishaji unaofanyika katika kiwanda cha Kinglion kinachounganisha pikipiki, kutengeneza mabati na vifaa vingine vya ujenzi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo wa pili kutoka kushoto akiangalia namna bati zinavyozalishwa katika kiwanda cha Kinglion kilichopo Kibaha Mkoani Pwani alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho Machi 26, 2025.
Mkumbo,amesema kuwa kwasasa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda na uwekezaji kiujumla na kwamba bidhaa nyingi zinazalishwa hapa nchini na zina ubora mzuri zaidi ya zile zinazotengenezwa nje .
Profesa Mkumbo ameongeza kuwa Serikali imeboresha mazingira ya Uwekezaji na kwamba inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kutatua changamoto za miundombinu ya barabara katika maeneo ya uchumi hususani viwandani.
Amesema, kiwanda cha Kinglion ni kati ya viwanda vikubwa Afrika na kimekuwa kikiuza bidhaa zake ndani na nje ya nchi na kwamba kutokana na vifaa vyake kuwa bora wamesaidia kuiongezea nchi uwezo wa kushindana kwenye masoko ya kimataifa.
Muonekano wa ndani wa Kiwanda cha Kinglion kilichopo Kibaha Mkoani Pwani kinachozalisha Bati na kuunganisha pikpiki za magurudumu matatu na mwili.
"Kiwanda hiki kina maabara zake na huwa wanapima viwango vya ubora wa bidhaa kabla ya Shirika la Viwango Tanzania ( TBS) kuja kuzikagua jambo ambalo limekuwa likitutangaza dunianu kote kupitia bidhaa za kiwanda hiki,"amesema Mkumbo
Profesa Mkumbo ameahidi kutoa ushirikiano katika kiwanda hicho ikiwa pamoja na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili ili kuondoa mkwamo katika uzalishaji wake.
Amepongeza Uwekezaji wa kiwanda cha Kinglion ambacho tayari kwasasa kimeshatumia dola milioni 42 kati ya dola Milion 62 wanazotarajia kutumia katika Uwekezaji wao huku wakitoa ajira 2000 kati ya hizo 800 za moja kwa moja na 1200 za muda.
Afisa masoko wa kiwanda cha Kinglion kilichopo Kibaha Mkoani Pwani John Maduka (Kulia), akimueleza jambo wa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo watatu kutoka kushoto aliyetembelea kiwandani hapo Machi 26, 2025
Meneja wa kiwanda hicho Anold Lyimo ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaowapatia katika shughuli zao za Uwekezaji huku akisema vikwazo wanavyokabiliana navyo tayari wameviwasilisha kuomba vitatuliwe.
",Tunaishukuru Serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wawekezaji wanakuwa katika mazingira mazuri na sisi Kinglion tunafaidika na jitihada za Rais na tunaona changamoto zetu zinafanyiwakazi ,"amesema Lyimo.
Hatahivyo,Lyimo amebainisha mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na Serikali kuwa ni pamoja na kuunganishiwa nishati ya gesi na kuboreshewa barabara inayoingia kiwandani pamoja na umeme.
Comments
Post a Comment