MAANDALIZI YA UZINDUZI MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA YAMEFIKIA ASILIMIA 96
Na Gustaphu Haule,Pwani
Club News Editor - Charles Kusaga
MAANDALIZI ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa unaotarajia kuwashwa April 2, 2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Tumbi Kibaha Mkoani Pwani yamefikia asilimia 96.
Uwanja wa Shirika la Elimu Tumbi Kibaha Mkoani unaotarajia kutumika katika hafla ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa April 2, 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari leo Machi 25 katika viwanja vya Shirika la Elimu Tumbi Kibaha mahali ambapo uzinduzi huo utafanyika.
Kunenge,amezungumza na Waandishi wa habari hao mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo akiwa pamoja na timu ya maandalizi kutoka katika ofisi yake pamoja na timu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Kunenge, amesema Mkoa wa Pwani upo vizuri na umejipanga kikamilifu katika kuhakikisha tukio hilo kubwa la kihistoria na heshima linafanyika ndani ya Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa habari leo Machi 25 kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa unaotarajia kuwashwa April 2,2025 Kibaha Mkoani Pwani
Kunenge, amesema uwanja umekamilika na kwamba tayari mpaka sasa jukwaa kubwa na nzuri limejengwa ikiwa pamoja na kuweka sehemu maalum ya viongozi wa kitaifa (VIP) 1,11 ,111 na IV huku akisema pia matenti yapo ya kutosha.
Aidha, Kunenge amesema katika tukio hilo Mkoa unategemea kuwa na watu 16000 kutoka maeneo mbalimbali ya ndani ya Mkoa ,mikoa jirani na hata kutoka Taifa.
"Miundombinu ya maji imejengwa vizuri,tumekarabati na sehemu ya kuegesha magari ya viongozi na tumeweka kokoto laini ( Bustdust) kwa ajili ya kuhakikisha hakuna vumbi,"amesema Kunenge
Kunenge,amesema kuwa katika uwanja huo pia zitafungwa taa za kutosha,ulinzi,mifumo ya Maji Safi na Maji taka ipo ya kutosha na kwamba kila kitu muhimu kimeangaliwa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge watatu kutoka kushoto mwenye kofia akikagua uwanja wa Shirika la Elimu Tumbi Kibaha Mkoani Pwani unaotarajia kutumika katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa April 2, 2025.
Mkuu huyo wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha Wananchi wa Mkoa wa Pwani,mikoa jirani na watanzania kiujumla waje katika sherehe hiyo nzuri yenye Alaiki ya kuvutia .
Hatahivyo,amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa utazinduliwa April 2,2025 ukiwa na kauli mbiu ya Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa amani na Utulivu.
Mwisho
Comments
Post a Comment