WAKILI MKOLWE-WANAFUNZI TOENI TAARIFA ZA UKATILI WA KINGONO ,ASEMA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA IMEKUJA KUWAKOMBOA


Na Gustaphu Haule, Pwani 

MRATIBU wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini Egidy Mkolwe, amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilangalanga kuhakikisha wanatoa taarifa zinazoashiria ukatili wa Kingono.

Mkolwe ambaye pia ni Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ametoa wito huo wakati alipotembelea shuleni hapo akiambatana na timu ya wataalam mbalimbali katika utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyoanza kufanyika leo Februari 25 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani.

Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini Egidy Mkolwe alitoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa Kingono kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilangalanga ikiwa ni sehemu ya kampeni hiyo iliyoanza Februari 25 mwaka huu 

Mkolwe, amewaambia wanafunzi hao kuwa zipo tabia na vitendo viovu vinavyoashiria ukatili wa Kingono ambavyo hufanyiwa na watu mbalimbali lakini wanafunzi hao ukaa kimya.

Amesema, vitendo hivyo ni pamoja na kushikwa bila ridhaa maeneo ya makalio, sehemu za maziwa na wakati mwingine kutaka  kuingiliwa kinguvu kimwili jambo ambalo halikubaliki.

Mkolwe, amesema vitendo hivyo na vingine vikiachwa vinaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo mwanafunzi kupata mimba,magonjwa na hata Kwa upande wa Wanaume kuwa mashoga na hivyo kukatisha ndoto zao.

"Nawaomba kuanzia leo yeyote anayekutana na viashiria vya ukatili wa Kingono ni vyema akatoa taarifa katika mamlaka husika ikiwemo katika ofisi ya Serikali ya Kijiji, Kitongoji,Mtaa, Jeshi la Polisi,walimu na hata wazazi naamini tukifanya hivyo mtakuwa salama,", amesema Mkolwe.

Mkolwe,amewaambia wanafunzi hao kuwa mambo mkubwa ya kuzingatia ni kuhakikisha wanajua kuwa ni kosa kwa mtoto kufanya mapenzi na mtu mzima kwakuwa adhabu yake ni miaka 30 huku jambo lingine ni kosa mtoto wa kike na Kiume kushikwashikwa hovyo katika maeneo ya sehemu za Siri na hata katika makalio.

Amesema kuwa, kutokana na changamoto hizo Serikali ipo macho na ndio maana Serikali kupitia Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuja na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ili kusudi kuweza kuwasaidia Wananchi wa ngazi za chini wanaokosa haki kwasababu ya kukosa fedha na hata uelewa wa kisheria.

Timu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) wakiwa katika majukumu yao leo Februari 25 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Aidha, Mkolwe amewasisitiza wanafunzi hao pia kuacha tamaa ya fedha na vitu vidogovidogo kutoka kwa watu wenye Nia hovyo ikiwemo zawadi,chips ,lifti za bodaboda na mambo mengine kwakuwa vitu hivyo vinachangia na kusababisha ukatili wa Kingono.

Kwa upande wake mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka Shule ya Sekondari Kilangalanga Beatus Kalegezi,ameishukuru Serikali kwa kuwaletea elimu hiyo huku akisema kwasasa wameelewa namna ya kuepuka na vitendo hivyo kwakuwa awali hawakujua viashiria vya ukatili wa Kingono.

Nae Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Dayana Brandus, ukatili wa Kingono ni moja ya Jambo ambalo linawanyima usingizi hivyo kwasasa wamejipanga kikamilifu kukomesha hali hiyo.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Msaidizi wa Kisheria Dayana Brandus akiwa katika kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Shule ya Sekondari Kilangalanga leo Februari 25.

Hatahivyo, Brandus amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kuona namna ya kuwasaidia Wananchi wake na anaimani kupitia kampeni hiyo masuala hayo yatapungua huku akisema baada ya kumalizika kwa kampeni bado watapita tena kufuatilia masuala hayo na hivyo waweze kuchukua hatua.

Mwisho.

Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA