WAANDISHI WA HABARI PWANI WAJENGEWA UWEZO KUANDIKA HABARI ZA MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor
BAADHI ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Pwani wamepewa mafunzo ya kujengewa uwezo kuhusu kuandika habari za Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto.
Mafunzo hayo yametolewa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Anjita (ANJITA CHILD DEVELOPMENT FOUNDATION) kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa Pwani (CRPC) chini ya ufadhili wa Taasisi ya TECDEN (TANZANIA EARLY CHILDHOOD DEVELOPMENT NETWORK) yaliyofanyika Februari 12 Mjini Kibaha.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano Serikalini kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Zablon Bugingo ameishukuru taasisi ya Anjita kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa Wanahabari.
Bugingo, amesema mradi wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto ni mradi unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii lakini unashirikisha Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC).
Bugingo, amewaomba Waandishi wa habari kujikita zaidi katika kuelimisha jamii ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto ili kusudi nchi ipate kuwa na vizazi bora vyenye kuleta faida kwa Taifa .
"Niwaombe Waandishi wa habari tutumie Kalamu zetu kuelemisha jamii juu ya suala la Malezi na Makuzi ya watoto kwani naamini tukifanya hivyo tutakuwa tumeokoa vizazi vingi vya Tanzania na hapo ndipo tutakapotoa viongozi bora wa kuongoza Taifa letu hapo baadae"amesema Bugingo
Aidha, Bugingo amesema ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani ili kuhakikisha kazi zao zinafanyika kwa urahisi zaidi ili kuhakikisha programu hiyo inafikia malengo yake.
Kwa upande wake afisa Programu na Mafunzo kutoka UTPC Victor Maleko, ambaye alikuwa mkufunzi wa mafunzo hayo amesema kuwa Waandishi wa habari ni watu muhimu katika kuleta mabadiliko chanya katika suala la Malezi na Makuzi ya watoto.
Afisa Programu na Mafunzo kutoka Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Victor Maleko akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani kuhusu kuandika habari za Malezi, Makuzi,na Maendeleo ya awali ya mtoto (MMMAM) mafunzo hayo yamefanyika Februari 12,2025 Mjini Kibaha
Maleko, amesema kuwa nia ya mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwenye masuala ya uandishi wa habari wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto (MMMAM) ambayo ni Programu mama ya Kitaifa inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii na taasisi nyingine ikiwemo UTPC.
Aidha, amesema kuwa awali mpango huo ulianza kwa Wanahabari wachache ambao wamekuwa vinara lakini wameona ni vyema kuendelea kuwajengea uwezo Waandishi wengi zaidi ili kutoa fursa kwa Waandishi juu ya kuelimisha jamii .
Maleko, amesema katika programu hiyo Waandishi wanamaeneo matano ya kuyafanyiakazi (Afua) ambayo ni Afya Bora, Lishe, Ujifunzaji wa awali,Malezi na Muhitikio, pamoja na suala la Ulinzi na Usalama ambapo amewaomba Waandishi wa habari kuongeza nguvu katika kuandika habari hizo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Akifunga mafunzo hayo afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha Elia Kabora, amesema kuwa Vyombo vya habari vitumike kuandika habari za kumsemea na kumlinda mtoto.
Mwisho.
Comments
Post a Comment