TAKUKURU PWANI YAONGEZA NGUVU UCHAGUZI MKUU 2025, YATOA ONYO KWA WATOA RUSHWA


Na Gustaphu Haule,Pwani

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imesema kuwa katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 imejipanga kikamilifu katika kudhibiti vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya wagombea.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Alli Sadiki, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu vitendo vya rushwa katika uchaguzi na namna ya kukabiliana navyo.


Sadiki, ambaye pia alikuwa akieleza utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha Oktoba na Desemba 2024 amesema kuwa suala la uchaguzi mwaka huu ndio jukumu ambalo wanakwenda kulifanya kwa ueledi mkubwa kwakuwa wanataka kuona viongozi wanapatikana kwa njia halali na haki.

Sadiki,  amesema kuwa kwasasa wataendelea kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi sambamba na kuwafikia wadau wote wanaohusika na uchaguzi ambao ni vyama vya Siasa,Wasimamizi wa Uchaguzi,Wanahabari, Wananchi na Jamii nzima kiujumla.


"Takukuru inatambua mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi,hivyo tumejipanga kutoa elimu kuhusu rushwa kupitia semina,mikutano ya hadhara,na vipindi vya Redio ili kuwafikia wadau wote wa Uchaguzi,"amesema Sadiki

Sadiki, amesema lengo ni kutaka kuona watu wanashiriki uchaguzi usiokuwa na vitendo vya rushwa lakini ni sehemu ya kutoa tahadhari kwa wale wote wenye tabia hizo ilikusudi anapokamatwa ajue wazi kubwa ametenda kosa.

Mbali na hilo lakini pia Mkuu huyo wa Takukuru amesema wataendelea kufanya udhibiti wa mapato ya Serikali na usimamizi wa rasilimali za Umma ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

"Takukuru ipo na inafanyakazi usiku na mchana, kwahiyo pamoja na masuala ya uchaguzi lakini tutaendelea kufuatilia fedha za miradi ya maendeleo na tupo tayari kupokea taarifa za vitendo vya rushwa na sisi tutazifanyia uchunguzi na kisha kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria,"amesema Sadiki

Sadiki,ameongeza kuwa mwaka huu katika utendaji wa kazi zake itawashirikisha zaidi Wananchi kwa kufanya vikao vya mara kwa mara kupitia mpango maalum wa "Takukuru Rafiki"ambao kazi yake ni kupokea kero na mrejesho kwa nia ya kusaidia wananchi kutatua kero zao.

Aidha, Takukuru Mkoa wa Pwani imetoa wito kwa Wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwafichua wale wote wanaoshiriki kufanya vitendo hivyo kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika.


Hatahivyo,Sadiki amewaasa Wananchi kufuata sheria,kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuwa salama na kuepuka migogoro yenye kuleta viashiria vya rushwa huku akitaka watumie namba 113 kutoa taarifa za vitendo vya rushwa au kufika ofisini.

MWISHO.

Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA