RC PWANI AZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA, SHEKHE WA MKOA AOMBA VYETI VYA NDOA YA KIISLAMU VITAMBULIKE KISHERIA.
Na Gustaphu Haule,Pwani
SHEKHE Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamis Mtupa ameiomba Serikali kuvitambua kisheria vyeti vya ndoa vinavyotolewa na dini ya kiislamu ili kuondoa usumbufu uliopo sasa.
Mtupa amewasilisha ombi hilo Februari 24 Mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa Kisheria ya mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) uliofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Pwani.
Akizungumza katika hafla hiyo Mtupa amesema wamekuwa wakitoa hati halali za ndoa lakini waumini wa dini hiyo wakizipeleka Serikalini wanaambiwa hazitambuliki na hivyo kuleta usumbufu katika jamii.
" Tunaomba Serikali ifanyie maboresho vyeti vinavyotolewa kwa wanandoa wa kiislamu, wakivipeleka Serikalini wanaambiwa vinatakiwa vya ndoa za Serikali wakati hawakufungia ndoa zao huko,naomba hili liangaliwe," amesema
Akizindua kampeni hiyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata Msaada wa Kisheria wa migogoro mbalimbali hususan ndoa,Ukatili wa Kinjisia,mirathi na Migogoro ya ardhi ikiwa ni hatua ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za Kisheria kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali katika uzinduzi wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika Februari,24,2025 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani .
Kunenge amesema kuwa kampeni hiyo ya msaada wa Kisheria kwa mkoa wa Pwani itafanyika kwa siku tisa katika Halmashauri zote na na Wilaya Saba za mkoa huo ambapo wananchi watafikiwa kusikiliza na kupatiwa msaada wa migogoro yao.
Kunenge, ameongeza kuwa huduma katika kipindi hicho itatolewa bure kwakuwa Rais Dkt.Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa jambo hilo akiwa na shauku ya kuwasaidia Wananchi wake katika kupata haki zao.
Awali, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini amesema tayari Kampeni hiyo imezinduliwa katika mikoa ya Mwanza, Lindi na leo Februari 24 inazinduliwa katika mikoa ya Pwani na Mbeya na ifikapo Februari 25 itaanza kazi rasmi katika Halmashauri mbalimbali.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia uliofanyika Februari 24 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani.
Sagini, amesema Wizara imejipanga kikamilifu kuhakikisha ifikapo mwezi Mei, 2025 Kampeni itakuwa imetekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Waziri huyo amesema pamoja na huduma za Msaada wa Kisheria, Wizara pia itatoa elimu ya uraia na utawala bora kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwemo Wajumbe wa Kamati za Usalama ngazi ya Mkoa, Wilaya, Wakuu wa Vitengo, Divisheni za Mkoa na Wilaya na Watendaji wa Kata.
Amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi kuhusu masuala ya uraia, haki za binadamu, misingi ya utawala bora na demokrasia.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akitembelea banda la dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyofanyika Februari 24 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani.
Naye Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaid Hamis amewataka wananchi kufika kwenye vyombo vya Sheria pindi wanapopata Changamoto.
Mwisho
Comments
Post a Comment