KISHINDO CHA MBUNGE KOKA SEMINA YA WAENEZI KIBAHA MJINI, AMFAGILIA RAIS SAMIA
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka, amewataka makatibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa ngazi Matawi na Kata kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi zao kuhakikisha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anakwenda kushinda Kwa kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Aidha, Koka amesema ushindi wa Rais Samia ni wazi kuwa utaambatana na ushindi wa nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kibaha Mjini kwakuwa kazi nzuri za kimaendeleo zimefanyika kwa kiwango kikubwa.
Koka, amesema hayo wakati akifunga semina ya makatibu hao iliyofanyika katika ukumbi wa Kibaha Shopping Mall ambapo semina hiyo iliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao hususani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Makatibu Uenezi Siasa na Mafunzo wakiwa katika Semina ya kujengewa uwezo iliyofanyika Februari 11 katika Ukumbi wa Kibaha Shopping Mall,semina hiyo iliandaliwa na CCM Kibaha Mjini
Amesema kuwa, Serikali kupitia Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanyakazi kubwa na kwamba kinachotakiwa ni kuona Katibu mwenezi na Kata wanakuwa mstari wa mbele katika kukitetea chama na Serikali kwakuwa ndio jukumu lao.
Amesema kuwa, kwasasa anashangaa kuona watu wengine wakiitumia mitandao kufanyakazi ambazo sio zao ili hali makatibu Uenezi wapo na ndio wenye jukumu la kuisemea Serikali na kusema lazima kwasasa wabadilike.
Koka, ameongeza kuwa,Waenezi ndio sauti ya Chama na kupitia semina hiyo lazima wajitambue kuwa wao ni akina nani huku akiahidi kuwatengenezea mfumo maalum ambao utawasaidia kumsemea Rais , Mbunge na Diwani kuanzia juu mpaka chini.
Amesema kuwa, yeye amekuwa Mbunge katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, kipindi cha Hayati John Magufuli na sasa Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini awali Kibaha haikuwa kama hivi ilivyosasa.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akizungumza wakati akifunga semina ya Makatibu Uenezi, Siasa na Mafunzo wa Kata na Matawi wa Kibaha Mjini iliyofanyika Februari 11,2025 katika ukumbi wa Kibaha Shopping Mall uliopo karibu na stendi ya Mabasi ya Mikoani .
Akieleza mfano wa mambo machache ya kimaendeleo ambayo ameyafanya Koka ,amesema kuwa mwaka 2010 wakati ameingia kuwa Mbunge alikuta baadhi ya maeneo ya Kibaha Mjini hayana mtandao wa simu lakini kwasasa kila mahali mawasiliano yapo.
Amesema, katika mwaka huo pia Kibaha Mjini ilikuwa Mamlaka ya Mji mdogo lakini alipambana kupata kuwa Mji lakini bado haitoshi akafanya kila jitihada kupata Manispaa na sasa Manispaa imepatikana.
Akitolea mfano Kata ya Sofu, Koka amesema Kata hiyo aliweka nguvu kubwa kuhakikisha inapata Shule ya Sekondari na Zahanati ambapo katika eneo la Sekondari alilazimika kutoa eneo lake lililokuwa na thamani ya Sh.milioni 300 na kuamuru ijengwe Sekondari.
"Eneo la ujenzi wa Sekondari Kata ya Sofu ni mimi niliyefanya jitihada kwani eneo hilo awali lilitaka kutwaliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mji Kibaha Jenifa Omolo lakini mimi nilivyosikia hivyo ikabidi nirudi kutoka Dodoma nije kulikomboa lile eneo na baadae nikaamua kujenga Shule ya Kata, kwahiyo ile Shule kuitwa Koka Sekondari haikuwa bahati mbaya japo baadhi ya watu walikuwa na mtazamo tofauti,"amesema
Amesema, upande wa Zahanati ya Kata ya Sofu ,Koka alitoa eneo lenye thamani ya Sh.milioni 250 bure ili kusudi Zahanati hiyo ijengwe na sasa kazi imefanyika na Wananchi wanapata huduma .
Koka,ameon geza kuwa amepigania eneo la Mitamba lirudi kwa Wananchi na akafanikiwa kwa awamu ya kwanza na sasa amefanikiwa tena kwa awamu ya pili jambo ambalo limefanya Kibaha hiwe katika mpango mzuri na hatimaye kupata Manispaa.
Katibu wa Itikadi,Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Kibaha Mjini Clement Kagaruki, akizungumza katika Semina ya kuwajengea uwezo makatibu wa Uenezi ngazi ya matawi na Kata iliyofanyika Februari 11 katika Ukumbi wa Kibaha Shopping Mall.
Ameongeza kuwa, kupatikana kwa Manispaa hiyo ni wazi kuwa kila kitu kitabadilika ikiwemo barabara nyingi za Mitaa kujengwa kwa kiwango cha lami kazi ambayo itafanyika mwaka huu kwa kila Kata.
"Wakati naingia kuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini nilikuta barabara ya lami moja tu,ikiwa kuanzia Tamco- Tumbi Hospitali hadi Picha ya Ndege, yaani hata barabara ya kutoka Mailimoja kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilikuwa ya vumbi lakini sasa lami ipo kila mahali na sasa kila Kata inakwenda kupata barabara ya lami,"amesema Koka
Amesema kuwa, maendeleo ya Kibaha Mjini hayakuja hivihivi lakini ipo kazi imefanyika na ndio maana anajivunia kuona maendeleo yaliyopatikana lakini endapo makatibu hao wataendelea kushirikiana na mbunge upo uwezekano hapo baadae Kibaha kuwa Jiji.
Amesema kwasasa anapigania eneo la Shirika la Elimu Kibaha lililopo barabarani liwe sehemu ya maendeleo ya Kibaha na tayari amewasilisha hoja bungeni kwakuwa eneo hilo linafanya Mji kuwa pori na hivyo kuharibu sura ya kuwa Manispaa.
Hatahivyo, Koka ameahidi kuendelea kushirikiana na makatibu Uenezi pamoja viongozi wengine wa chama kwa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo zaidi ili waweze kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani .
Mwisho
Comments
Post a Comment