TANZANIA NA UINGEREZA KUENDELEZA MADINI MKAKATI.
Na Gustaphu Haule, Tanzania
#KAZIINAONGEA
SERIKALI ya Tanzania imeihakikishia Serikali ya Uingereza kuendeleza ushirikiano kwenye sekta ya madini hususani katika kuwajengea uwezo watu wake, kubadilishana uzoefu, uongezaji thamani ya madini na kuwekeza kwenye kufanya tafiti mbalimbali.
Lengo ni kukuza sekta ya madini na kupanua mnyororo wa thamani ili kuongeza ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la taifa.
Hayo, yameelezwa hivi karibuni na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika ofisi ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young.
"Kwanza kabisa Balozi Young amefika ofisini kujitambulisha kwa kuwa ana muda mfupi nchini tangu awasili lakini pia tumezungumzia ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Tanzania na Uingereza,"amesema Mavunde
Waziri wa Madini Anthony Mavunde katika katika mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania ofisi ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam
Katika mazungumzo hayo, Tanzania na Uingereza zimekubaliana katika kuwajengea uwezo watu wake na kubadilishana uzoefu hususani katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini nchini ''Geological Survey of Tanzania" (GST) na British Geological Survey (BGS) ya Uingereza ili kuwajengea uwezo Watanzania kwa kuwa na ujuzi stahiki katika masuala ya uendelezaji wa sekta ya madini
Eneo la pili lililozungumzwa kwa urefu ni katika Madini Mkakati ambapo Uingereza wameonesha utayari katika kushirikiana na Tanzania katika eneo la mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini mkakati ambapo Tanzania imejipanga kuhakikisha inavutiwa uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini hapa nchini.
Mavunde amesema kuwa kwasasa ni muda muafaka wa kuhakikisha madini ya kimkakati yanawanufaisha Watanzania na taifa na ndiyo maana umeandaliwa Mkakati maalumu wa kutekeleza azma hiyo huku ikizingatiwa kuwa madini hayo kwa sasa yana mahitaji makubwa duniani.
"Tupo katika hatua za mwisho kukamilisha mkakati huu maalum wa Madini Mkakati muhimu ambao pia ni sehemu ya Kampeni ya Dunia katika kupunguza hewa ya ukaa kupitia matumizi ya nishati safi," amesema Waziri Mavunde.
Akizungumza katika Mkutano huo Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marriane Young amesema Uingereza inapongeza jitihada kubwa za kukuza sekta ya madini zinazofanywa na serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuahidi kuimarisha ushirikiano mkubwa baina ya nchi hizi hasa katika kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kupitia Taasisi za madini nchini Uingereza na Tanzania.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania katika mazungumzo Ofisi ndogo ya Wizara ya Madini iliyopo jijini Dar es Salaam
Balozi Young ameunga mkono mpango wa uongezaji thamani madini nchini na kuahidi kwamba Uingereza itashirikiana na Tanzania kwa ukaribu ili malengo hayo yatimie.
*#KAZIINAONGEA*
Comments
Post a Comment