SERIKALI YAMBANANISHA MKANDARASI BARABARA YA TUNGAMA- MKANGE
Na Gustaphu Haule, Tanzania
*●Aomba radhi ajipange upya*
SERIKALI inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega imemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta kumpa taarifa ya kitaalamu kuhusu Mkandarasi M/s China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara ya Tungamaa-Mkwaja-Mkange yenye kilomita 95.2 ambayo ni sehemu ya barabara ya Tanga-Pangani-Bagamoyo ili achukue hatua stahiki.
Mapema Januari 02, 2025 akizungumza mjini Pangani Waziri Ulega amesema haridhishwi na kasi ya mkandarasi huyo anayejenga sehemu ya tatu ya barabara hiyo kwa kuwa asilimia 40 badala ya 90 huku muda wa kukamilisha kazi ukiwa umebaki miezi mitatu.
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega akizungumza na mkandarasi anayejenga barabara ya Pangani- Mkange- Bagamoyo katika ziara yake aliyoifanya jana.
"Haikubaliki na haivumiliki kutoa visingizio vya mvua wakati wakandarasi wengine wanafanya vizuri katika maeneo hayo hayo", amesema Ulega.
Aidha, Waziri Ulega amempongeza Mkandarasi Shandong anayejenga daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 kwa kazi nzuri na kumtaka kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha daraja hilo kwa wakati.
"Asilimia ya daraja inaridhisha ongezeni bidii,wataalam na muda wa kufanya kazi ili muwe mbele ya muda na barabara unganishi kilomita14.3 nazo zikamilike" amesisitiza Ulega.
Pichani muonekano wa daraja la mto Pangani katika ujenzi kama inavyoonekana
Kuhusu mkandarasi CHICO anayejenga sehemu ya kwanza ya Tanga-Pangani Kilomita 50, Waziri Ulega amesema kwamba tayari Serikali
imeshamlipa Mkandarasi huyo Shilingi Bilioni 4.7 ili kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo.
Naye Mbunge wa jimbo la Pangani Jumaa Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa daraja hilo na kusisitiza ujenzi huo utaongeza shughuli za kiuchumi mkoani Tanga, Pwani na ushoroba wa Bahari ya Hindi kwa ujumla.
Pia Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Batilda Buriani ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa Barabara ya kimkakati ambapo inaunganisha nchi jirani ya Kenya na mikoa ya Tanga,Pwani na Dar es salaam na kusisitiza wananchi kutumia fursa za miradi hiyo kukuza biashara na kuibua fursa za ajira.
Barabara ya Tanga-Pangani-Bagamoyo ni sehemu ya barabara kuu ya ushoroba wa pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia Malindi-Mombasa hadi Lungalunga nchini Kenya na Horohoro-Tanga-Pangani- Bagamoyo hadi Dar es salaam nchini Tanzania ambapo kwake kutakuza Uchumi, Utalii na Biashara.
*#KAZIINAONGEA*


Comments
Post a Comment