MANARA AZINDUA MASHINDANO YA SAMIA CUP KIBAHA VIJIJINI, ACHANGIA SH.MILIONI 1
Na Gustaphu Haule,Pwani
MDAU wa mpira wa miguu Nchini Haji Manara, ameahidi kutoa kiasi cha Sh. milioni 1 kwa ajili ya kuchangia mashindano ya kombe la Samia "Samia Cup" yanayofanyika katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini chini ya uratibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilayani humo.
Manara ametoa ahadi hiyo kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mtongani uliopo Mlandizi Kibaha wakati akizindua michuano hiyo Januari 11,2025 ambayo inashirikisha timu 104 kutoka katika Kata zote za Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Mdau wa michezo Haji Manara akizungumza katika ufunguzi wa Mashindano ya Samia Cup yaliyofanyika Januari 11 ,2025 katika viwanja vya Mtongani Mlandizi Kibaha Vijijini,Kulia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Hamoud Jumaa na kushoto ni mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini Mkali Kanusu pamoja na mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu ( COREFA) Robert Munisi.
Kwa mujibu wa Manara amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha wananchi wakiwemo vijana kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Amesema kuwa ,amevutiwa na vijana kuandaa mashindano kama hayo ambayo yanaunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuchangia kwenye michezo kwani ni sehemu ya kuleta maendeleo nchini.
"Nimefurahi sana kuona Vijana wameanzisha mashindano ambayo kwa kiasi kikubwa yanaunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,hivyo kutokana na umuhimu huo nami nitawapatia kiasi cha Sh.milioni 1 ili mfanikishe mashindano haya,"amesema Manara.
Katibu wa hamasa wa UVCCM Kibaha Vijijini Godfrey Mwafulilwa, amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha watu kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura na kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwaka huu.
Mdau wa michezo Nchini Haji Manara akiwa pamoja na timu Moja ya timu inayoshiriki mashindano ya Samia Cup mara baada ya kuzindua mashindano hayo Januari 11 ,2025, na Kulia ni mwenyekiti wa COREFA Robert Munisi na watatu kutoka kushoto ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ( MNEC) Hamoud Jumaa
Mwafuliwa, amesema kuwa kila kata watacheza katika hatua ya awali kwa ajili ya kupata timu moja itakayoingia 16 bora ngazi Wilaya ambapo mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atapata zawadi ya guta la matairi matatu, mshindi wa pili atajinyakulia pikipiki na mshindi wa tatu atapata kiasi cha shilingi milioni 1.
Mwafulilwa,ameongeza kuwa kwenye mashindano hayo hakutakuwa na kiingilio na kila timu itapatiwa jezi na mipira miwili huku zawadi nyingine ni mchezaji bora, kipa bora na mfungaji bora kila mmoja atapata ngao na Sh. 50,000 na timu yenye nidhamu itapata Sh. 100,000.
Mwafulilwa ,amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kwa namna Moja au nyingine kuchangia mashindano hayo huku akiwaomba wadau hao kuendelea kusaidia michezo hiyo kwa ajili ya kuibua vipaji kwa vijana .
Kwa upande wake wenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani COREFA Robert Munisi amesema kuwa malengo yao ni kuhakikisha mpira Pwani unachezwa kwa kuzingatia taratibu.
Munisi,amesema kuwa COREFA itashirikiana na wadau wanaoandaa mashindano mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha vijana wanakuza vipaji vyao kwakuwa mpira wa miguu ni ajira,
Munisi,amewapongeza wadau hao kwa kuandaa mashindano hayo ambayo ni makubwa kwenye mkoa huo ambapo mashindano mengine makubwa yaliandaliwa na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga ambaye pia Mbunge wa Mafia.
Hatahivyo,katika ufunguzi wa mashindano hayo ya Samia Cup yalizikutanisha timu mbili ikiwemo timu za Kujiandikisha na timu boresha taarifa ambapo mpaka kumalizika kwa mchezo zilikuwa zimetoka sare ya bao 1-1.
Mwisho.
Club News Editor
Comments
Post a Comment