JESHI LA POLISI MKOA WA PWANI LAMSHIKILIA ALIYETENGENEZA NA KUSAMBAZA PICHA CHAFU ZA UTUPU MITANDAONI.
Na Gustaphu Haule,Pwani
Club News Editor - Charles Kusaga
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limefanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye anadaiwa kutengeneza na kusambaza katika mitandao ya kijamii picha chafu za utupu zisizo za maadili jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya nchi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Salim Morcase, amewaambia Waandishi wa habari Januari 20, 2025 kuwa kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa huyo hakiwezi kuvumilika kwa nchi yenye maadili mema kama ya Tanzania kwakuwa jambo hilo ni kinyume na Sheria za nchi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Salim Morcase akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu tukio la kukamatwa kwa mtuhumiwa aliyetengeneza na kusambaza picha za utupu katika mitandao ya kijamii.
Morcase, amesema kuwa picha hizo chafu na zisizo za kimaadili waliotengeneza waliunganisha na baadhi ya majengo ya Shule ya Baobab ili kuaminisha Umma kuwa vitendo hivyo vinafanyika Shuleni hapo.
Kamanda Morcase, amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Januari 3, 2025 lilipokea taarifa ya kutoka kwa uongozi wa Shule ya Baobab iliyopo Kata ya Mapinga Wilaya Bagamoyo juu ya kusambazwa kwa picha hizo mitandaoni.
Amesema, baada ya kupokea taarifa hizo Jeshi limefanya uchunguzi na hatimaye limefanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye uchunguzi wa kitaalamu ulisaidia kumfikia na kumkuta na picha hizo na kifaa cha kieletroniki ambacho alikuwa akitumia kusambaza picha hizo chafu.
Kamanda Morcase ameongeza kuwa pamoja na kumnasa mtu huyo lakini pia kwasasa bado Jeshi linaendelea kuwasaka watu wengine waliohusika katika kutengeneza na kusambaza picha hizo za mjongeo.
Morcase amesema, Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu wenye tabia kama hizo za kutengeneza na kusambaza picha kama hizo kwa malengo ya kuchafua wengine au taasisi kwani mkono wa Sheria lazima utawafikia .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Baobab Shani Swai, amesema kuwa tukio la kusambazwa picha hizo limetokea Disemba 31, 2024 na ndipo wakatoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Baobab iliyopo Kata ya Mapinga Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Shani Swai, akizungumza na Waandishi wa habari shuleni hapo kukanusha picha feki za utupu zilizotengenezwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii zikihusishwa na Shule hiyo.
Swai, amesema kuwa picha hizo hazina mahusiano na wanafunzi wa Shule hiyo kwani hata mtindo wa kusuka ni tofauti na hao walioonyeshwa mitandaoni.
Amesema, wanafunzi wa Shule hiyo wanasuka Nywele Tano mpaka Saba kwa stahili ya "Twende Kilioni" na vitanda vyao vya Chuma na sio vya mbao kama vinavyoonekana pichani.
"Kuna picha mbili zilizosambazwa mitandaoni ambapo moja wamedukua picha za mahafali za wanafunzi wetu pamoja na majengo yetu lakini hizo nyingine zenye maudhui machafu na zilizokosa maadili sio za kwetu na hatuhusiki nazo ," amesema Swai
Aidha, Swai amelishukuru Jeshi la Polisi kwakazi kubwa iliyofanya mpaka kufikia hatua ya kumkamata mmoja wa watuhumiwa waliotengeneza na kusambaza picha hizo kinyume na maadili huku akiamini haki itatendeka dhidi ya wale wote waliohusika kuichafua Shule hiyo.
Hatahivyo, Swai ametoa wito kwa wazazi kuondoa taharuki na kuacha kukatishwa tamaa dhidi ya picha hizo kwakuwa Baobab ni taasisi kubwa inayosimamia maadili kupitia kamati ya maadili iliyopo shuleni hapo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Taaluma Mhandisi Fredy Ntevi, amesema kuwa Shule ya Baobab ni miongoni mwa Shule ambazo zimekuwa zikisimamia kikamilifu maadili ya wanafunzi pamoja na Wafanyakazi.
Uongozi wa Shule ya Sekondari Baobab iliyopo Bagamoyo Mkoani Pwani wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na Waandishi wa habari juu ya kukanusha picha feki na chafu za mjongeo zilizotengenezwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii zikihusishwa na Shule hiyo.
Ntevi, amesema Shule ya Baobab hairuhusu mwanafunzi kuingia na Simu na endapo mwanafunzi anagundulika kuwa na Simu unyang'anywa kwa ajili ya kudhibiti utovu wa nidhamu sambamba na kulinda maadili ya wanafunzi na Wafanyakazi kiujumla.
Amesema kuwa, wanachokiona ni ushindani wa biashara japokuwa mpaka sasa hajui kuwa ni nani anayefanya ushindani dhidi yao.
Makamu Mkuu wa Shule Taaluma kutoka Baobab Alphonce Kamisa, amesema pamoja na njama zilizofanywa za kutaka kuichafua Shule hiyo lakini maendeleo ya Shule hiyo bado mazuri.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Baobab upande wa Taaluma Alphonce Kamisa,akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari Januari 20,2025 kuhusu kukanusha picha feki za utupu zilizotengenezwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii zikihusishwa Shule hiyo.
Kamisa, amesema kuwa Shule ya Baobab inajumla ya wanafunzi 1700 ambapo kati ya hao Wanaume ni 730 na wakike 970 ambapo hatahivyo mpaka sasa wanafunzi walioripoti shuleni ni 1600.
Amesema, hao wengine 100 hawajaripoti kutokana na changamoto za kifamilia ikiwemo ugonjwa na kwamba kadri siku zinavyokwenda mbele wanafunzi hao wanazidi kuripoti.
Comments
Post a Comment