HAMOUD JUMAA AWATAKA WANAPWANI KUMUOMBEA ULEGA.
Na Omary Mngindo, Mlandizi
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa kupitia Jumuia ya Wazazi (MNEC) Humoud Abuu Jumaa, amewataka wananchi Mkoa wa Pwani kumuombea Dua Waziri wa Ujenzi Alhaj Abdallah Ulega.
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega
Jumaa ametoa rai hiyo Jumanne ya Disemba 31,2024 akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mlandizi, chini ya Mwenyekiti wake Malinganya Fundi ambapo MNEC huyo aliambatana na MwenyekIti wa chama hicho Wilaya Mkali Kanusu.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa( MNEC) Hamoud Jumaa.
katika mkutano huo wa kuwashukuru wananchi kwa kuwachagua wenyeviti wanaotokea ndani ya chama hicho, Jumaa alianza kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kumteua mwanaPwani huyo kushika Wizara hiyo muhimu.
"Leo (Jana Jumanne ya Disemba 31) Alhaj Ulega amefanya mkutano mkubwa wa kuwasomea utekelezaji wa Ilani ya chama chetu, nikapata nafasi ya kutoa neno ambapo nimewaomba wanaPwani tumuombee dua kwani Wizara aliyopewa ni muhimu sana," amesema Jumaa.
"Nimemkumbushia changamoto zinazotukabili sekta ya miundombinu katika barabara zetu zilizoko Pwani, ikiwemo kilio kikubwa cha Barabara ya Makofia, Yombo, Mlandizi, Mzenga mpaka Vikumbulu kwani hii barabara ni muhimu sana kwetu," amesema Jumaa akiwashukuru wanaMlandizi hao kwa kukiaminisha chama hicho kwa kuwachagua wagombea wote wanaotokea ndani ya chama hicho, huku akiwaasa Wenyeviti hao kuwatumikia kwa moyo wote.
"Kumalizika kwa uchaguzi wa nafasi zenu ni mwanzo wa uchaguzi utaofuata mwaka 2025, tumebakiza masaa machache kuuanza mwaka huo, hivyo kufanya kwenu vizuri mtakiheshimisha chama chetu kinachoongozwa na Mwenyekiti wetu Dkt. Samia Suluhu Hassani," amesema Kanusu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kata hiyo Malinganya amewaonya Wenyeviti hao kutokutumia vibaya nafasi zao, huku akiwataka wakawatumikie wananchi kwa weledi mkubwa.
Mkutano huo uliofanyika kwenye Kitongoji cha Kitemvu katani hapa mamia ya wakazi walihudhuria sherehe hiyo, iliyoendelea na mkesha wa kuupokea mwaka 2025 uliofanyika katika eneo la Vikuruti katanihapa.
MWISHO.
Club News Editor
Comments
Post a Comment