BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA MWANASHERIA MKUU LAKUTANA KUFANYA TATHMINI YA UTENDAJI KAZI MWAKA 2024/2025.


Na Gustaphu Haule,Pwani

BARAZA  la wafanyakazi la ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali limekutana katika kikao chake cha kwanza kwa ajili ya kujadili masuala  mbalimbali yatakayosaidia kurahisisha utendaji kazi na kutoa huduma za kisheria kwa wananchi.

Kikao hicho kimeanza kufanyika  juzi katika Chuo Cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa Mkoa wa Pwani kwa kuwashirikisha wajumbe mbalimbali wakiwemo wakuu wa vitengo,wakurugenzi wasaidizi ,wakuu wa divisheni,mawakili wa Serikali na wajumbe wa Tughe.

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliofanyika leo Januari 24,2025 katika Chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Hamza Johari, amesema kuwa lengo la kukutana katika kikao hicho ni kufanya tathmini ya namna ambavyo utendaji kazi wao ulivyokuwa katika kipindi cha mwaka uliopita na namna wakatavyoendelea mwaka 2025.

Johari, amesema kuwa ni wazi kuwa mwaka uliopita wamefanya vizuri katika eneo la Sheria ikiwemo kuweka kliniki za Sheria ambazo zimetolewa bure kwa wananchi ambapo lengo lake ni kusogeza huduma za kisheria karibu na Wananchi.

Amesema kuwa, kwasasa huduma hiyo inaendelea kufanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba kazi hiyo ni  mpango wa ofisi ya AG ambayo itaendelea kuwekewa mkazo juu ya huduma ya Sheria kwa wananchi pamoja na huduma nyingine za masuala ya kisheria.

"Mbali na kliniki za kisheria lakini ofisi ya AG inafanya kazi ya kupitia mikataba  inayoletwa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha na kutoa ushauri wa kisheria kazi ambayo imefanyika kuanzia Julai hadi Disemba mwaka 2024." amesema Johari.

Johari ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kazi hiyo imekuwa ikifanyika vizuri na pale ambapo panahitajika  kutoa maoni yao wamekuwa wakifanya hivyo kwa maslahi ya Taifa.

Aidha , Johari amesema ofisi ya AG pia imekuwa ikifanya kazi ya kuhakikisha mawakili na wanasheria wao wanaendelea kuwa vizuri na uwezo wa kutoa huduma za kisheria hapa Nchini.

Kutokana na hali hiyo kikao hicho kimeangalia namna ya kuwawezesha mawakili na wanasheria hao kwa kuwapa mafunzo mbalimbali licha ya kuwa zipo baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo uhaba wa fedha.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari (AG) akizungumza na Waandishi wa habari katika Chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Pwani kuhusu mkutano wa Baraza Kuu la wafanyakazi wa ofisi yake uliofanyika Januari 24,2025 chuoni hapo.

"Lengo la mkutano huu pia ni kuangalia changamoto zao na kuzipatia majibu hasa katika suala la mafunzo stahiki ambayo yanahitaji fedha na sisi tutaangalia na kuweka Mkakati wa namna gani ili tuweze kutoa mafunzo Kwa wanasheria na mawakili," amesema Johari 

Amesema, pamoja na mambo mengine lakini kikao hicho kimeangalia namna ya kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari ( TEHAMA)katika kuboresha hutoaji huduma za kisheria ili kuweza kuendana na wakati pamoja na kuleta urahisi katika kuwafikia Watanzania.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi, ameipongeza ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya kazi zao vizuri sambamba na kuona umuhimu wa kuitisha Baraza hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi akizungumza katika mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliofanyika Januari 24,2025 katika Chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani 

Maswi, amesema kuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kiungo muhimu kwa maendeleo ya nchi na Serikali imekuwa na imani kubwa na ofisi hiyo na kwamba Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa ofisi na watumishi wote wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

Amesema, anatambua ofisi ya AG imekuwa na majukumu mazito sambamba na changamoto ya uchache wa raslimali lakini Wizara ya Katiba na Sheria itaona namna ya kusaidia katika utatuzi wa baadhi ya changamoto ikiwemo kuajiri Wafanyakazi na vitendeakazi.

Maswi, ameiomba ofisi hiyo kuendelea kuishughulikia mikataba mbalimbali yenye maslahi kwa nchi yetu na lazima mikataba hiyo ijulikane ambapo kutokana na umuhimu wa mikataba hiyo lazima kufanyakazi kwa bidii.

Mbali na hayo, lakini pia Maswi amemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushirikiana na ofisi yake kuhakikisha wanafuatilia na kuboresha mikataba ya Serikali kwa maslahi mapana na Taifa.

Kikao cha Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kilichofanyika Januari 24,2025 katika Chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani,anayeonekana Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi na Kulia kwake ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari na aliyesimama kushoto ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Samwel Maneno.

"Mikataba hii ya Serikali ni muhimu sana, kwahiyo niiombe ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuanza kutoa mafunzo kwa watumishi juu ya upekuzi wa mikataba ya Serikali ili kusudi tuweze kulinda maslahi ya Taifa na hata katika kutoa huduma za kisheria kwa wananchi," amesema Maswi.

Awali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Samwel Maneno, amesema katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Jumla ya mikataba 1799 ilifanyiwa upekuzi ambapo kati ya hiyo mikataba 1,639 ya manunuzi,120 imehusu fedha, mkataba (1) kuhusu Maliasili na 39 ni ya ushirikiano wa kimataifa.

Mwisho 
Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA