WAZIRI PROF. KABUDI AKUTANA NA WADAU SEKTA YA HABARI NA UTANGAZAJI


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.  

* Wizara hii ndiyo inayobeba Taswira na Haiba ya Tanzania na Taswira na Haiba ya Mtanzania

  * Sekta ya Habari ni mhimili usio rasmi wa nne wa demokrasia 
  
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa sekta ya habari na utangazaji jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere tarehe 18 December 2024.


Wadau walioshiriki mkutano huo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Umoja wa Klabu za Waandishi wa HabarI Tanzania (UTPC), Umoja wa Haki ya kupata Taarifa (CoRI), Idara ya Habari Maelezo, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Waandishi wa habari na wadau wengine wa Sekta ya Habari na Utangazaji.



Mkutano huo ndio wa kwanza tangu Waziri Prof. Kabudi ateuliwe kushika nafasi hiyo. Katika hotuba yake ameeleza kuwa amefanya hivyo kwa makusudi kabisa kukutana, kuonana na kufahamiana na wadau hao akiwapongeza kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata taarifa sahihi kwa wakati na kwa uwazi sawa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ameongeza kuwa kukutana huko ni kwa ajili ya kutatua changamoto za Sekta ya habari ili kuiimarisha kwa maendeleo ya Taifa letu.

"Wizara ndiyo inayobeba Taswira na Haiba ya Tanzania na Taswira na Haiba ya Mtanzania" 

Katika hotuba yake Waziri ameeleza kuwa Wizara hii ndiyo inayobeba Taswira na Haiba ya Tanzania na Taswira na Haiba ya Mtanzania. Alieleza kuwa Vyombo vya habari ni kioo kinachoonyesha Taswira ya Tanzania ndani ya Nchi na nje ya Nchi, akifafanua kuwa Vyombo hivi ndiyo Taasisi ya kutunza na kuendeleza Fahari ya Tanzania, Upekee  wa Tanzania (The Uniqueness of Tanzania) na Upekee wa Watanzania (The Uniqueness of Tanzanians).

"Sekta ya Habari ni mhimili usio rasmi wa nne wa demokrasia"

Pia katika hotuba yake Waziri alieleza kuwa Sekta ya Habari ni mhimili usio rasmi wa nne wa demokrasia baada ya Mihilimili ya Utawala, Bunge na Mahakama. Akifafanua hii alieleza kuwa chombo cha habari kina haki na wajibu kwa wananchi wa Tanzania na kwa wanadamu wote na kina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Hii ndio sababu Sekta ya Habari kupewa  nafasi maalum na kuiwezesha inaimarika. Waziri alieleza kuwa Serikali inachukua hatua mbalimbali kuhaikisha kuwa Sekta ya habari inakuwa na inatoa huduma kwa weledi na kuzingatia maadili ya Kitanzania, kwa kufanya hivyo alieleza kuwa Serikali inatimiza wajibu wake na sio kuwa inatoa hisani kwa Sekta ya Habari. 


Katika mkutano huo wadau mbalimbali wa sekta ya habari na utangazaji walitoa salamu fupi wakimshukuru waziri kuwaita na kuongea nao.


Club News Editor - Charles Kusaga

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA