WAZIRI JAFO ATAKA WAWEKEZAJI WAZALISHE BIDHAA ZENYE UBORA KUENDANA NA SOKO LA DUNIA
Na Gustaphu Haule,Pwani
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amewataka wawekezaji kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye viwango vya juu ili kuendana na Soko la dunia.
Jafo, ametoa wito huo wakati akifungua maonesho ya Nne ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji yanayofanyika viwanja vya stendi ya zamani Kibaha Mailimoja Mkoani Pwani.
Amesema kuwa, Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri na wezeshi kwa wawekezaji hivyo ni vyema sasa bidhaa zinazozalishwa ziwe za viwango.
"Nawaomba wawekezaji kuzalisha bidhaa zenye ubora ili ziweze kupata Soko la dunia lakini na sisi Watanzania tujitahidi kupenda vyakwetu kwakuwa uwezo wa kuzalisha bidhaa bora tunao,"amesema Jafo
Amesema Wizara inakuja na mpango mahususi wa miaka mitano wa kuwakwamua vijana kupitia Kilimo cha matunda utakaonza mwaka 2025 hadi 2030 ambapo utakuwa unasimamia vijana katika Uzalishaji wa matunda ya aina mbalimbali na tayari Soko lipo.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt .Selemani Jafo akikagua mabanda katika maonesho ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Pwani, maonesho hayo yameanza Disemba 16 na kumalizika Disemba 20 mwaka huu,wa katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.
Katika hatua nyingine Jafo amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kwa kazi nzuri anayoifanya hasa katika kuhamasisha wawekezaji kuingia Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kufanya uwekezaji wa Viwanda mbalimbali.
Amesema Mkoa wa Pwani ndio Mkoa kinara wa Viwanda na ni mfano wa mikoa mingine na kwamba maonesho hayo lazima yawe endelevu huku akisema mwaka ujao yatakuwa maonesho ya Kitaifa.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt .Selemani Jafo akiwa katika Banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya kukagua Maonesho ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Pwani,anayeonekana kushoto ni kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima na katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.
"Maonesho haya yatafanyika tena mwakani lakini kwasasa yatakuwa yakitaifa na yataratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani,"amesema Jafo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema kuwa katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Samia Mkoa wa Pwani umefanikiwa kujenga Viwanda vikubwa 78.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani
Kunenge, amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na Rais Samia kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na hivyo kuvutia idadi ya wawekezaji kuongezeka Mkoani Pwani.
Maonesho ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Pwani yameanza kufanyika Disemba 16 na yatamalizika Disemba 20 mwaka huu.
Mwisho
Comments
Post a Comment