WAZIRI JAFO ALIPONGEZA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI MKOA WA PWANI, AWASHAURI KUTOA ELIMU ZAIDI KWA WANANCHI.
Na Gustaphu Haule,Pwani
Club News Editor
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Selemani Jafo, amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani kwa kazi nzuri wanayofanya katika kukabiliana na majanga mbalimbali yanayotokea katika jamii ikiwemo ya moto.
Jafo, ametoa pongezi hizo Disemba 17,2024 wakati alipotembelea banda la Zimamoto lililopo katika maonesho ya Biashara na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani.
Jafo, akiwa katika maonesho hayo pamoja na mambo mengine alitembelea Banda la Zimamoto kwa ajili ya kujionea kazi wanazofanya na hivyo kueleza kuridhishwa na kazi ya Zimamoto inayofanywa hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea maelezo mafupi kutoka kwa Afisa habari na Mafunzo wa Zimamoto kutoka Kibaha Mjini Joyce Kapinga, Jafo amesema kuwa Kikosi cha Zimamoto kinafanyakazi kubwa ya kuokoa majanga kwa jamii hapa nchini hivyo lazima wapongezwe na kuheshimiwa.
Aidha,Jafo amekishauri Kikosi hicho kuendelea na juhudi za kusaidia Uokoaji wa Majanga katika jamii huku akisema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ipo pamoja na Kikosi hicho.
Jafo,amemshauri Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mrakibu Mwandamizi wa Zimamoto (SSP) Jenifa Shirima kuhakikisha wanajipanga na wanakuwa tayari muda wowote ili kukabiliana na majanga yanayotokea ikiwa pamoja na kuhakikisha magari yao yanakuwa na maji.
"Mnafanyakazi nzuri sana lakini naomba mjipange zaidi kuhakikisha mnaendana na teknolojia kwakuwa na vifaa ya kutosha na vyakisasa sambamba na magari ambayo muda wote yanakuwa na maji ya kutosha pale majanga yanayotokea,"amesema Jafo.
Pamoja na hilo lakini pia Waziri huyo amewashauri Zimamoto kujipanga kwa ajili ya kurudi katika jamii kwa ajili ya kuwashauri wanapojenga nyumba zao waache nafasi kwa ajili ya kupitisha gari la Zimamoto pale ambapo Majanga ya moto yanayotokea,"amesema Jafo.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima ,amemshukuru Waziri Jafo kwa kutembelea Banda hilo na kwamba ushauri wake utafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
"Zimamoto Mkoa wa Pwani mara nyingi tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kukabiliana na majanga yanayotokea hususani ya moto lakini mafanikio yake yamekuwa makubwa sana na sasa tunakwenda kuyafanyiakazi maelekezo na ushauri uliotoa,"amesema Shirima.
Awali afisa Habari na Mafunzo wa Zimamoto Kibaha Joyce Kapinga, amesema kwasasa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashirikiana zaidi na jamii ili kupata taarifa mapema kuhusu majanga yanayotokea na hivyo kuweza kuyadhibiti kwa haraka kabla hayajaleta madhara.
Mwisho.
Comments
Post a Comment