TRA PWANI YAFURAHIA MAONESHO YA VIWANDA YASEMA YAMEKUWA NA MAFANIKIO,YAWAOMBA WALIPAKODI KUDAI NA KUTOA RISITI PINDI WANAPOUZA NA KUNUNUA BIDHAA

 

Na Gustaphu Haule,Pwani

MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Mkoa wa Pwani Masawa Masatu amesema maonesho  ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji yaliyofanyika Mjini Kibaha yamekuwa na mafanikio makubwa pamoja na kutoa fursa kwa walipa kodi wengi kupata elimu.


Masatu ameyasema hayo Desemba 20 mwaka huu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea katika banda  la TRA kwa ajili ya kujionea shughuli zilizokuwa zikifanywa na TRA katika maonesho hayo .

Masatu ,amesema kuwa TRA ambao ni moja ya wadhamini wa maonesho hayo waliona kushiriki maonesho hayo ni fursa kwa walipakodi kupata huduma sambamba na elimu ambayo itawasaidia katika kusimamia biashara zao.

Amesema kuwa, huduma zilizokuwa zikitolewa katika maonesho hayo ni zile zile ambazo zilikuwa zinapatikana ofisini ambapo miongoni mwa huduma hizo ni kusajili TN namba, kutoa huduma ya namba za kulipia (Control Number), kurekebisha taarifa mbalimbali za walipakodi pamoja na kutoa elimu ya Kodi.

"Huduma zote tunazozitoa ofisini ndizo tulizokuwa tunazitoa katika maonesho haya na tunashukuru Wananchi wengi wameitikia na kuelimika na huduma zetu,", amesema Masatu


Masatu amesema maonesho hayo ni moja ya sehemu ya kutangaza Mkoa lakini pia yanatoa fursa kwa wananchi kupata elimu na kuzifahamu bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda vilivyopo Mkoani humo.

"Mwitikio wa wananchi umekuwa ni mkubwa lakini kwa hapa kwenye banda letu tumepata nafasi ya kutoa elimu kwa wananchi waliotutembelea na nina imani sasa mabadiliko yatakuwa makubwa kupitia maonesho haya," amesema.

Meneja huyo amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa lakini amefurahi zaidi kuona maonesho ya mwaka 2025 yanakuwa ya Kitaifa na yatafanyika tena Mkoa wa Pwani.

Masatu amewakumbusha wananchi kuelekea mwisho wa mwaka kuzingatia kanuni za Kodi ikiwa pamoja na kuhakikisha kuomba risiti pindi wanaponunua bidhaa kwani kwa kufanya hivyo inachangia ongezeko la makusanyo ya Kodi ambayo yanakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo.

TRA Mkoa wa Pwani imetunukiwa tuzo ya kuwa miongoni mwa taasisi za serikali zilizofanya vizuri katika maonesho hayo ambapo tuzo hiyo imetolewa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani.



MWISHO.
Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA