SERIKALI YA RAIS SAMIA YAREJESHA KM 74 .7 ZA BARABARA HANANG
Na Gustaphu Haule,Tanzania
SERIKALI ya Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara wiki hii imekamilisha zoezi la kurejesha miundombinu ya barabara iliyoathiriwa na mafuriko ya tope, magogo na mawe yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2023.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Hanang Mhandisi Paul Mlia, amesema kwamba jumla ya Kilomita 74.7 ziliathirika zenye jumla ya madaraja 14 kati ya barabara hizo Kilomita 19.7 ni za Katesh Mjini na Kilomita 55 ni barabara za pembezoni mwa mlima Hanang, zimekamilika.
“Serikali kupitia TARURA ilifanya tathimini ya uharibifu uliojitokeza katika miundombinu hiyo ili kurejesha haraka huduma kwa wananchi”, amesema.
Aidha, amebainisha maeneo mengine yaliyoathirika ni maeneo ya kijamii ikiwemo nyumba za Ibada, soko la kateshi na makazi ya wananchi ambapo utekelezaji wake wa muda mfupi walifanikisha uondoaji wa mawe, tope, magogo na kurejesha mawasiliano katika barabara ya kateshi mjini yenye urefu wa Kilomita 19.7 pamoja na uondoaji wa matope ndani ya nyumba za wananchi 61.
"Kwa upande wa wilaya ya Hanang tulipewa jukumu la utekelezaji wa mradi wa barabara ya Dawar-Mogitu na barabara za mita eneo la makazi ya waathirika ya maporomoko ya tope Kilomita 13.50".
Pia amesema upande wa makazi mapya ya walioathirika na mafuriko eneo la Walet ambapo walipewa jukumu la kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe Kilomita 13.5.
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha waathirika wa mafuriko kwa kupata makazi mapya”, amesema
Hatahivyo, amesema katika kipindi cha miaka mitatu wameweza kuongezewa bajeti ya ujenzi na matengenezo ya barabara kutoka Sh.milioni 800 hadi kufikia bilioni 2.3 hivi sasa .
Fedha hizo zimewezesha kujenga barabara ambazo zinaweza kupitika mwaka mzima na sambamba na kuweka taa 27 katika Mji wa Kateshi na kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao muda wote na hivyo kuwasaidia kukuza uchumi wao.
Nao wananchi wa wilaya hiyo wameishukuru Serikali kupitia Wakala kwa kurejesha miundombinu katika makazi yao kipindi cha mafuriko ya tope.
Mkazi wa Hanang, Rogat Petro amesema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwani wilaya yao imenufaika na mambo mengi licha ya wilaya hiyo kuwa ni ya muda mrefu na hivyo kupatiwa barabara katika kata za pembeni ni jambo jema.
“Tunamshukuru Rais ametusaidia hasa kipindi cha mafuriko kwa kutuma viongozi wake na kuweza kuturejeshea mawasiliano na hadi sasa watu wote tunaendelea na shughuli zetu za kila siku”.
Amemalizia kusema kwamba wananchi wa Hanang wanaheshimu miundombinu ya Serikali na kwamba wana umoja na wapo tayari kulinda uwekezaji wote uliowekezwa na Serikali.
*#KAZIINAONGEA*
Comments
Post a Comment