SERIKALI YA RAIS SAMIA YANADI FURSA ZA UWEKEZAJI FALME ZA KIARABU.


Na Gustaphu Haule, Tanzania 

#KAZIINAONGEA

Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea na mkakati wake wa kufungua fursa za Uwekezaji ambapo imeikaribisha Saudi Arabia kuwekeza nchini katika fursa mbalimbali zikiwemo Utalii, Kilimo, Madini, Uendelezaji wa miundombinu pamoja na Uchumi wa Buluu.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu  Nchemba, ametoa mwaliko huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi na Mipango wa Saudi Arabia mhandisi Ammar Naqadi, 


Nchemba amekutana na Mhandisi Naqadi katika mkutano wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji lililoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirika la Kuendeleza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), lililofanyika hivi karibuni Mjini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Dkt. Nchemba amebainisha kuwa, Tanzania inaendelea na mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) ambapo imeshakamilika kipande kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na ujenzi unaendelea kwa vipande vinavyoelekea Mwanza na DRC kupitia Burundi.

Ujenzi wa reli hiyo ni fursa kwa Saudi Arabia kuwekeza katika miundombinu hiyo itakayochochea ukuaji wa biashara kati ya Saudi Arabia, Tanzania na nchi za Afrika Mashariki.

‘‘Bado tunakusanya rasilimali tunatamani wewe na Taasisi yako kuona namna ambavyo tunaweza kushirikiana katika ujenzi na uendeshaji wa mradi huu wa reli ya kisasa ambao utahusisha na Sekta binafsi, ikiwemo katika usafirishaji wa mizigo na safari za kila siku’’, ameeleza Dkt. Nchemba.


Ameeleza kuwa, Tanzania ina fursa katika Sekta ya kilimo na ina ardhi ya kutosha na yenye rutuba kuweza kuzalisha mazao ya aina mbalimbali kwa wingi hivyo ni vema Saudi Arabia ikatazama fursa katika sekta hiyo muhimu.

‘’Tunaweza kushirikiana katika kilimo ikiwemo uzalishaji wa ngano, mafuta ya kupikia pia tuna ranchi ambazo zinaweza kutumika kuzalisha nyama za kutosha na hivyo kupata mazao na bidhaa za kusafirisha nje ya nchi jambo litakalotunufaisha sisi pamoja na ninyi pia’’, amefafanua Dkt. Nchemba.

Nchemba amesema,Tanzania ina aina ya madini ambayo yanapatikana Tanzania tu, hivyo hiyo ni fursa muhimu kwa Saudi Arabia kuweza kushirikiana na Tanzania kuwekeza katika sekta hiyo kwa kujenga viwanda vya kuchakata madini ili kuyaongezea thamani.

Uwekezaji huo utawezesha kubadilishana uzoefu na Saudi Arabia wa rasilimali watu pamoja na teknolojia itakayoisaidia Tanzania katika kupiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi haraka zaidi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchumi na Mipango wa Saudi Arabia  Ammar Naqadi, amesema Saudi Arabia iko tayari kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa miundombinu ya reli ili kurahisisha usafirishaji wa watu, mazao na mizigo ili kuchochea ukuaji wa biashara ambapo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Amesema, nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania katika fursa za kuendeleza sekta ya madini, kilimo, mafuta na gesi, utalii, uchakataji wa mazao ya bahari, miundombinu pamoja na utalii ambapo wataandaa timu ya Wataalamu kwa kushirikiana na Sekta binafsi kutembelea Tanzania kujionea fursa za uwekezaji katika sekta hizo ili kujiridhisha na mazingira ya fursa za Tanzania ili kuweza kuwekeza.

Amesisitiza kuwa, katika kufanikisha ukuaji wa biashara baina ya Tanzania na Saudi Arabia suala la utozaji kodi mara mbili ni muhimu kufanyiwa kazi ili kuwawezesha wafanyabiashara kutopata changamoto wafanyapo biashara kati ya pande hizo.

*#KAZIINAONGEA*

Club News Editor - Charles Kusaga


Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA