SERIKALI YA RAIS SAMIA YAFANIKIWA UWEKEZAJI DP WORD DAR ES SALAAM.
Na Gustaphu Haule, Tanzania
*●Yawekeza Sh.Bilioni 214.425 katika miezi mitano*
#KAZIINAONGEA
Kwa mujibu wa mkataba kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Kampuni ya DP World (DPW), inapaswa kuwekeza Dola za Marekani Milioni 250 sawa na Shilingi Bilioni 675 katika kipindi cha miaka mitano.
Katika kipindi cha miezi mitano tangu kuanza uwekezaji kwa kampuni hiyo, tayari wameshawekeza Shilingi Bilioni 214.425 ambayo ni asilimia 31, kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya kisasa, ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA, na usanifu na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA wa kisasa wa uendeshaji wa Bandari.
Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam amesema kuwa, tangu Kampuni ya DP World ianze uendeshaji wa shughuli za Bandari mwezi Aprili 2024, mafanikio mbalimbali yamepatikana.
Msemaji wa Serikali GERSON MSIGWA
Ameyataja mafanikio hayo ni kwamba, katika Bandari hiyo wastani wa muda wa meli kusubiri umepungua kutoka siku 46 mwezi Mei, 2024 hadi kufikia wastani wa siku saba (7) ikiwa ni siku 0 kwa meli za makasha, siku 12 kwa meli za kichele, na siku 10 kwa meli za mizingo mchanganyiko.
Kutokana na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa yaani "Ship-to-Shore Gantry Crane" na "Rubber-Tired Gantry Crane" (SSG na RTG) katika kupakia na kushusha mizigo, muda wa kuhudumia meli za makasha gatini umepungua kutoka wastani wa siku saba (7) hadi wastani wa siku tatu (3) hivyo kupunguza idadi ya meli zinazosubiri kutoka wastani wa meli 35 mwezi Septemba 2023 hadi wastani wa meli 15 mwezi Septemba 2024.
Katika kipindi cha miezi mitano gharama za matumizi ya uendeshaji wa Bandari zimepungua hadi kufikia asilimia 2.7 ya makusanyo wakati ambapo matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa asilimia 15.1 kwa mwezi kabla ya kukabidhiwa uendeshaji wa Bandari kwa Kampuni ya DP World Dar es Salaam
Katika kipindi cha miezi mitano (Aprili hadi Septemba 2024) tangu DPW Dar es Salaam waanze kuendesha Gati 0-7 katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imeshakusanya jumla ya Shilingi Bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World, ikijumuisha tozo ya pango (Land rent), tozo ya mrabaha (Royalty), na Ardhi (Warfage).
Kutokana na kuongezeka kwa mapato na kupungua kwa gharama za uendeshaji kufuatia maboresho yaliyofanyika, serikali, kupitia TPA, imeanza uwekezaji katika miradi yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.922 sawa na Dola za Marekani Milioni 686.628 kwa kutumia makusanyanyo yanayopatikana.
Miradi hii ni Ujenzi wa Kituo cha Kupakulia Mafuta (SRT), Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao (Mtwara), na Ujenzi wa Gati za Majahazi (Dhow Wharf) Dar es Salaam.
Kuunganishwa kwa Mifumo ya Forodha (Tanzania Customs Integrated System - TANCIS) na ile ya Bandari (Tanzania Electronic Single Window System-TeSWS), Hii imewezesha kupunguzwa/kuondolewa kwa mifumo iliyokuwa inafanana na hivyo kupunguza muda wa kuondoa mizigo Bandarini, kuongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano.
Kutokana na Uwekezaji huo mkubwa, Mapato ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka hadi kufikia Shilingi Trilioni moja kwa mwezi Septemba 2024 ikilinganishwa na wastani wa Shilingi Bilioni 850 kwa mwezi Septemba 2023, hii imetokana na TRA kuweza kuchakata mizigo mingi zaidi ndani ya muda mfupi.
Kwa ujumla wake, maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam kufuatia kukabidhiwa kwa DP World na Makampuni mengine kuendesha Bandari ya Dar es Salaam yanaonesha kuwa na faida kubwa kiuchumi kwa kuchochea kuongezeka kwa biashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Uwekezaji huu ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango kuu la usafirishaji mizigo katika Ukanda wa Afrika.
*#KAZIINAONGEA*
Comments
Post a Comment