RC PWANI AZINDUA MPANGO WA UGAWAJI VITAMBULISHO VILIVYOBORESHWA KWA WAMACHINGA,ASEMA HATAKI KUONA WAMACHINGA WANASUMBULIWA
Na Gustaphu Haule,Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (Kulia) akizindua mpango wa ugawaji wa vitambulisho vilivyoboreshwa kwa ajili ya Wamachinga hafla ambayo imefanyika Disemba 4,2024 katika ukumbi wa ofisi ya Mkoa wa Pwani.
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezindua mpango wa ugawaji wa vitambulisho vilivyoboreshwa kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ( Machinga) waliopo katika maeneo tofauti ndani ya Mkoa huo.
Kunenge,amezindua mpango huo Disemba 4,2024 katika kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Pwani (RCC) kilichofanyika katika ukumbi mkubwa wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa iliyopo Mjini Kibaha.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (Kulia) akizindua mpango wa ugawaji wa vitambulisho vilivyoboreshwa kwa ajili ya Wamachinga hafla ambayo imefanyika Disemba 4,2024 katika ukumbi wa ofisi ya Mkoa wa Pwani.
Katika uzinduzi huo Kunenge alianza Kwa kuwakabidhi vitambulisho hivyo baadhi ya Wamachinga akiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Pwani Philemoni Maliga na mmoja kutoka kundi la Mama lishe.
Mbali na kugawa kwa Wamachinga hao lakini pia vitambulisho vingine alivikabidhi kwa Wakuu wa Wilaya ili kusudi waweze kuvikabidhi kwa wafanyabiashara waliopo katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (Pichani katikati mwenye Shati rangi nyeupe) akimkabidhi kitambulisho mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Philemoni Maliga mara baada ya zoezi la uzinduzi wa vitambulisho hivyo lililofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkoa wa Pwani Disemba 4,2024 na anayeshuhudia kushoto ni Mbunge wa Kibaha Mjini Silvestry Koka.
Aidha, Kunenge baada ya uzinduzi huo amesema kuwa mafanikio ya utoaji wa vitambulisho hivyo imetokana na juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye anataka kuona namna ambavyo Wamachinga wanapangwa na kuhudumiwa vizuri katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichofanyika Disemba 4,2024 Mjini Kibaha.
Amesema, Wamachinga ni kundi la watu muhimu na ni Watanzania ambao wanahitaji kupata huduma kutoka katika Serikali yao ndio maana Rais ameamua kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao bila usumbufu.
"Namshukuru Rais wetu Dkt .Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha mpango huu muhimu wa kugawa vitambulisho hivi kwakuwa itasaidia katika kuwapanga Wamachinga wetu na hata kuwahudumia kwa urahisi zaidi katika mahitaji yao,"amesema Kunenge
Kunenge,amewataka wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanakwenda kusimamia ugawaji wa vitambulisho hivyo pamoja na kuwapanga vizuri katika maeneo yao ili waweze kufanya biashara katika mazingira mazuri.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani Grace Tete, amesema kuwa vitambulisho hivyo kwasasa vimeboreshwa na vimekuwa na msaada mkubwa kwa Wamachinga.
Tete, amesema kuwa vitambulisho hivyo vitamsaidia Machinga kuweza kukopa benki kirahisi na hata kupata huduma nyingine muhimu za kijamii na kwamba kila Mmachinga anatakiwa kuwa na kitambulisho hicho.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani Grace Tete akionyesha kwa wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Pwani (RCC) vitambulisho vya Wamachinga vilivyoboreshwa katika hafla ya uzinduzi wa vitambulisho hivyo uliofanyika Disemba 4,2024 Mjini Kibaha.
"Vitambulisho hivi kwasasa vimeboreshwa zaidi maana ukiingia katika mfumo kinakuletea kila kitu kwakuwa kimeunganishwa na namba ya NIDA ya mhusika na pia kimewekwa picha juu na endapo kinapotea unaweza kukipata au kupewa kingine kwa gharama ndogo,"amesema Tete
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Pwani Philemoni Maliga,amemshukuru Rais Samia kwa kutambua umuhimu wa Wamachinga hapa nchini sambamba na Mkoa kwa kulisimamia jambo hilo vizuri.
Maliga,amesema kupitia vitambulisho hivyo anaamini Wamachinga wapo sehemu salama na watafanyakazi katika mazingira mazuri na hivyo kupata kipato cha kuendesha familia zao na hata katika kuchangia pato la Taifa.
Mwisho
.jpg)


.jpg)

Comments
Post a Comment