MWEKEZAJI KEDA CERAMICS CO LTD AWAUNGANISHA WANANCHI MBEZI -SHUNGUBWENI, ATOA MILIONI 150 KUJENGA DARAJA,WANANCHI WAFURAHIA UWEKEZAJI HUO.


Na  Gustaphu Haule,Pwani

WAWEKEZAJI wa kiwanda cha KEDA (T) Ceramics Co Limited  kilichopo Mkiu Wilayani Mkuranga wameendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kujenga daraja kubwa  katika Mto Msolwa uliopo barabara ya Mbezi Msolwa inayounganisha Kata ya Mbezi na Shungubweni.

Viongozi wa Kiwanda cha Keda Ceramics Co Ltd wakiwa eneo la ujenzi wa daraja la Mbezi -Shungubweni Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya kukamilisha ahadi ya mwekezaji wa kiwanda hicho ambapo awali aliwaahidi Wananchi wa maeneo hayo kuwajengea daraja hilo ili waweze kupata mawasiliano kwa urahisi ikiwa pamoja na kusafirisha mazao yao.

Aidha, daraja hilo limejengwa likiwa na urefu wa Mita Sita, upana wa Mita Saba na kina cha Mita 1.5 ambapo fedha za utekelezaji wa mradi huo zimetoka katika kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii na hivyo kufanya Wananchi wanaoishi karibu na uwekezaji huo  kunufaika.


Muonekano katika picha wa Mradi wa Ujenzi wa Daraja katika Mto Msolwa katika barabara ya Mbezi Msolwa inayounganisha Kata ya Mbezi na Shungubweni.

Akizungumza katika eneo la mradi huo afisa biashara wa kiwanda cha Keda  Masoud Suleyman amesema mradi huo wa kuimarisha miundombinu ya barabara utawezesha kata ya Mbezi- Shungubweni kurahisisha shughuli za kiuchumi na huduma za kijamii kwa wananchi wa kata hizo na kurahisisha usafirishaji wa  malighafi ya mchanga katika utengenezaji wa bidhaa ya kioo.

Afisa biashara wa kiwanda cha KEDA CERAMICS CO LTD Bw. Masoud Suleyman

"Gharama za mradi umetekelezwa kwa kutumia fedha za ufadhili wa kiwanda cha KEDA ceramics (T) Co Ltd  kwa mwaka 2024 gharama ya mradi ikiwa  ni Tsh . milioni 150  ambapo utekelezaji wa mradi huo umejengwa kwa kutumia wataalamu,vifaa na malighafi za kiwanda cha Keda Ceramic," amesema Suleyman
 
Suleyman, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo  umeanza tangu Oktoba  28,2024 kwa kushirikiana na wataaalamu kutoka ofisi ya Meneja Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA)Wilaya ya Mkuranga  ambapo vifaa na  malighafi za ujenzi wake  vimetolewa na Keda Ceramics (T) Ltd.

Eneo la ujenzi wa daraja katika  Kijiji cha Msolwa Kata ya Mbezi lililojengwa na mwekezaji wa kiwanda cha Keda Ceramic Co Ltd kilichopo Mkiu Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo  imekuwa ni mkombozi na kuleta manufaa makubwa kwani  mradi huo  utawezesha wananchi kupita kiurahisi kipindi chote cha mwaka ikiwemo kipindi cha mvua .

Kwa upande wao baadhi ya wananchi katika VAjeijiji tofauti vilivyonufaika na mradi huo akiwemo Mohammed msumi mkazi wa Kitongoji cha Kikopi Kijiji cha Msolwa anasema walikuwa wakipata tabu kuvuka katika eneo hilo haswa katika kipindi cha mvua.

"Wakati wa mvua maji yalikuwa yanajaa na Watu kushindwa kupitia hivyo Vijana wa maeneo haya walikuwa wakivusha watu kwa pesa lakini baada ya mwekezaji huyu wa Keda kuona changamoto hii waliamua kutusaidia kulijjenga daraja hili  katika ubora mzuri na sasa tunapita kwa urahisi zaidi bila shida yoyote,"amesema Msumi.

Aidha Msumi ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wawekezaji kutoka Keda Ceramic huku akiwakaribisha wawekezaji wengine waendelee kujitokeza kwa ajili ya kusaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa barabara ya Mbezi -Shungubweni na hata katika Sekta ya elimu,na afya.

Nae Amina Juma amewashukuru wawekezaji wa Keda kwa kuwajengea daraja ambalo lilikuwa  korofi wakati wa mvua huku akisema eneo hilo lilikuwa linajaa maji ambapo wananchi ,magari kukwama kwa kushindwa kupita hali iliwanyima usingizi wananchi wanaotumia barabara hiyo kwa muda mrefu na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo yao.

 Jumanne Mtambwe ni mwenyekiti  wa kijiji cha Kisayani Mkuranga  amesema wanafurahia ujenzi huo kwakuwa daraja hilo limewaunganisha kati ya  Kjiji cha Kisayani, Msolwa  na Shungubweni amesema  ujenzi huo utaleta chachu ya maendeleo kwakuwa barabara zitapitika vizuri kwakuwa mwanzoni daraja lilikuwa bovu halipitiki.

 Hatahivyo,Mtambwe ameushukuru uongozi wa  Keda kwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo lakini pia amewaomba wawajengee   barabara ambayo kwa sasa inasumbua kutokana na kasi ya magari yanayobeba mchanga ambao ni malighafi ya kutengenezea  vioo ambayo inatumika katika kiwanda chao.

Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA