MIAKA 63 YA UHURU NA ONGEZEKO LA UZALISHAJI UMEME BWAWA LA MWALIMU NYERERE
Na Gustaphu Haule, Tanzania
# KAZI INAONGEA
SERIKALI ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika huku ikifurahia mafanikio ya kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme nchini kwa asilimia 62 ikilinganishwa na mwaka 2021.
Maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika yanayo adhimishwa kila Disemba 09 ya kila mwaka tangu mwaka 1961, yameadhimishwa kwa kushuhudia maendeleo ya kiuchumi yaliyofanywa na Rais Samia katika kipindi cha miaka mitatu tangu alipoingia madarakani.
Kwa hivi sasa, Watanzania wananufaika na huduma ya uhakika ya umeme ambayo kiwango chake kimeongezeka na kufikia Megawati 2,607.96 ikilinganishwa na Megawati 1,605.86 za mwaka 2021.
Haya ni matokeo chanja na ya mafanikio ya mradi wa kuzalisha umeme katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99.2 na tayari wanazalisha Megawati 1,115 kutoka kwenye Mradi huo.
Disemba 22, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishiriki hatua ya kufunga njia ya kuchepusha maji na kuanza ujazaji maji kwenye Bwawa la kuzalisha umeme.
Februari 25, 2024 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, akiwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere aliviambia Vyombo vya Habari kuwa, kuanzia Februari 22, 2024 mtambo wa kwanza kati ya mitambo 9 umeanza kuzalisha umeme katika Bwawa hilo la Mwalimu Nyerere lililogharimu Shilingi Trilioni 6.5 kulijenga.
Mwaka 2012 hadi 2015 kulikuwepo tatizo kubwa la umeme nchini na kusababisha mgao hali iliyoilazimu nchi kukodisha mitambo inayotoza Capacity charge, hivyo kuigharimu nchi fedha nyingi
Mradi huo ambao unajengwa kwa fedha za ndani upo katika eneo la Selous linalotajwa kuwa moja ya maeneo ya urithi wa Dunia ambapo Tanzania inakusudia kupata umeme wa kutosha kupitia mradi huo.
Hatua ya kuanza kwa mradi huo inakuja baada ya miaka 40 tangu utafiti wa uzalishaji wa umeme kutoka Mto Rufiji uliofanywa wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ujenzi wa bwawa hilo unaofanywa na Wakandarasi kutoka nchini Misri unatarajiwa kugharimu dola za Marekani Bilioni 2.9 sawa na Shilingi Trilioni 6.5 za Kitanzania.
*#KAZIINAONGEA*

Comments
Post a Comment