JITIHADA ZA SERIKALI YA DKT.SAMIA KUOKOA MAISHA YA WANANCHI MAFIA ZAONEKANA



Na Gustaphu Haule, Tanzania 

#KAZIINAONGEA

KATIKA  jitihada za kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania kote nchini hasa wale walioko maeneo yenye changamoto za usafiri ikiwemo Wilaya ya Mafia iliyopo Mkoani Pwani  sasa zinafanyiwa kazi.

Kwasasa Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan tayari imefanya jitihada za kuweka usafiri wa Boti maalumu ya kisasa kwa Wananchi wa Wilaya Mafia Mkoa wa Pwani.


Boti hiyo maalum ni kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa kutoka katika Visiwa mbalimbali, Kata, Vijiji na Vitongoji na kuwaleta katika  Hospitali ya Wilaya iliyoko kata ya Kilindoni.



Boti hii imekuwa mkombozi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya Visiwani ambapo miundombinu ya barabara haifiki moja kwa moja na hivyo kusaidia kurahisisha utoaji huduma wa haraka kwa wagonjwa wa dharura, wakiwemo wajawazito, watoto, na wagonjwa wa ajali.

Wagonjwa hao kwa sasa wanaweza kupatiwa huduma ya haraka na salama hatua inayosaidia kupunguza vifo vinavyotokana na kuchelewa kufika hospitalini.

Mradi huu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Rais Dkt. Samia aliyoitekeleza katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za msingi popote alipo. 

Serikali hii ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza miradi ya kijamii inayolenga kuboresha maisha ya wananchi hususan wale walioko pembezoni na maeneo yenye changamoto za miundombinu na kufanya juhudi za kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania wote.

*Faida za kuwepo Mradi huo.*

Mradi wa Boti maalumu ya dharura umesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa msaada wa haraka kwa wagonjwa wa ajali, wajawazito na wagonjwa wengine wa dharula na  kuokoa maisha ya watu na imekuwa mkombozi wa kutoa usafiri salama na wa haraka kwa wagonjwa na kuwawahisha katika hospitali ya Wilayani Mafia kwa Rufaa na matibabu zaidi.

Mbali na kutoa huduma hizo za haraka imesaidia kuwawahisha wagonjwa kupatiwa huduma zaidi za Kitabibu, na pia Boti hii imewekwa vifaa vya kisasa kama Oxygen na sehemu maalumu za kuwahifadhi wagonjwa mahututi.

Kuwepo kwa boti hii kumeboresha upatikanaji wa huduma za Rufaa kwa wakazi wa maeneo ya Visiwani ambao walikuwa wanakabiliwa na changamoto za usafiri wa haraka hasa kwa wagonjwa.

Katika kuendelea kuyatafakari maono ya Serikali ya Rais Samia, ilikaa na kuona mbali kwa kuangalia njia ya kutokomeza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, ikaona kuna haja ya kuwekwa Boti hiyo ili kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.

Mradi huu ni mongoni mwa miradi mingi iliyotekelezwa na Rais Samia katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake.

Mafia ni mojawapo kati ya Wilaya nane za Mkoa wa Pwani, na eneo lake ni Kisiwa cha Mafia na Visiwa vidogo karibu nacho, likitazama mwambao wa Afrika Mashariki kilomita130 Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam.

Ni Kisiwa Kikuu chenye urefu wa kilomita 50 na upana wa kilomita nane, na kinajulikana pia kwa jina "Chole shamba" kutokana na Mji wa kale wa Chole uliokuwepo kwenye Kisiwa kidogo cha Chole karibu na kisiwa kikuu na ni Mji mkubwa na Makao Makuu ya wilaya ni Kilindoni.

Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka 2022 imebaini Kisiwa cha Mafia kuwa na wakazi wapatao 66,180.

*#KAZIINAONGEA*
Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA