IJUE SIRI YA JOSEPHINE MAENDAENDA KUCHAGULIWA MARA TATU KITONGOJI CHA JANGA.
Na Gustaphu Haule, Pwani
Club News Editor
UNAPOTAKA kuwataja wenyeviti wa Vitongoji Wanawake waliopo katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini hutakosa kumtaja Josephine Maendaenda mwenyekiti wa Kitongoji cha Janga kilichopo Kata ya Janga.
Maendaenda ameshinda katika uchaguzi wa Serikali ya Mitaa,Vijiji na Vitongoji uliofanyika Novemba 27 mwaka huu kwa kupata kura 2066 ushindi ambao unamfanya kuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Janga kwa awamu ya tatu mfululizo.
Ushindi wa Maendaenda kwa Kitongoji hicho sio wa bahati mbaya bali nikusudio jema kwa Wananchi wake kutokana na umahiri wa kiuongozi katika vipindi viwili vya nyuma alivyowai kuongoza.
Maendaenda ambaye pia ni mama mjasiriamali mwenye watoto wanne amekuwa na uzoefu mkubwa wa kiuongozi na hivyo kuwafanya Wananchi wake wafurahie kumchagua katika kila uchaguzi unapowadia.
Maendaenda katika uchaguzi wake hakuwa na mpinzani ambapo wakati wa uchaguzi, mpiga kura alikuwa na chaguo la kutiki Ndio au Hapana jambo ambalo pia liliwapa wepesi wapiga kura.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Maendaenda alifanya mahojiano na mwandishi wa Makala haya na hizi ndizo simulizi zake halisi.
MAENDAENDA ULIYAPOKEAJE MATOKEO BAADA YA KUTANGAZWA KUWA MSHINDI?
Kiukweli wakati natangazwa kuwa mshindi niliyapokea matokeo kwa furaha kubwa sana huku nikimshukuru Mungu juu ya ushindi lakini kwa imani ambayo Wananchi wa Janga wanayonipa.
Hatahivyo,kwakuwa nafasi ya mwenyekiti nilikuwa mgombea pekee angu sikuwaza sana bali nilijipa moyo na kumtanguliza Mungu mbele kutokana na jinsi ambavyo nimekuwa nikiishi na Wananchi wangu wa Janga.
NI AWAMU YA TATU SASA UNASHINDA KATIKA KITONGOJI HIKI,NINI SIRI YA USHINDI WAKO?
Ndugu Mwandishi siri ya ushindi wangu ni upendo,na kuheshimu raia au wananchi ninaowatumikia na kufanya kazi kwa bidii kwani kiongozi ni kama wito wa Kanisa lakini tunatofautiana tu kulingana na maeneo.
Niseme tu,wapo wachungaji wa Kanisani , wengine Misikitini lakini pia wapo wachungaji ambao wanachunga kupitia nafasi zao za uongozi,kwahiyo kufanyakazi kwa hofu ya Mungu hamna kinachoshindikana ila inategemea unawahudumiaje, unawasikilizaje,na unajitumaje kwao wewe kama mtumishi wao kwahiyo ukifanya vizuri wanapokuona wanajisikia faraja.
NI MAKUBWA KIASI GANI UMEFANYA MPAKA UKOSE MPINZANI KWENYE UCHAGUZI?
Kiukweli mimi nimefanya mambo mengi na makubwa katika Kitongoji hiki lakini zaidi katika elimu.
Katika elimu, wapo watoto ambao wanahitaji kusoma lakini wazazi wenzetu hawana uwezo kwahiyo mimi nilikuwa najitoa kuwasaidia.
Wakati mwingine ninapompeleka mtoto Shule, nikifika shuleni nakuta kuna watoto wanahitajika kupeleka Majembe, Kwanja na mahitaji mengine lakini wazazi wanakosa uwezo hivyo mimi nilikuwa nawanunulia na kuwapelekea .
" Hayati John Magufuli alipoingia madarakani alitangaza elimu bure lakini mimi bado nilikuwa nawasaidia wanafunzi wanaosoma hosteli hususani wale wa Magindu,Ruvustation na Kwala kwa kuwalipia fedha za hosteli na kuwanunulia vifaa vya Shule,",amesema Maendaenda
Haikuishia hapo, kwani katika uongozi wangu nimewai kuwasomesha watoto wengi akiwemo mmoja anayetambulika kwa jina la Mariam.
Mariam, alichaguliwa kusoma Chuo cha Uhasibu lakini wazazi wake hawakuwa na uwezo lakini binti akaja kwangu kuniomba nimsaidie ili aweze kusoma na kama hataenda Shule basi ataolewa mapema.
"Nilijitahidi mpaka Mariam alienda Shule kusoma na sasa amepata ajira Dodoma lakini hatahivyo wazazi wake na Mariam walinipigia simu kipindi nikiwa katika kampeni za uchaguzi wakinishukuru kwa kazi kubwa niliyofanya kwa mtoto wao," amesema Maendaenda
Mbali na Mariam lakini pia nimemsomesha mtoto mwingine wa kiume anaitwa Said Kombo na huyu nilimsomesha Shule binafsi (private) kidato cha kwanza mpaka cha nne lakini naye matokeo ya kidato cha nne hakufaulu vizuri na kushindwa kuchaguliwa .
Licha ya kushindwa kuchaguliwa lakini pia Kombo nilimsaidia kusoma tena Shule binafsi kidato cha Tano na Sita na baadae kwenda Chuo cha Ualimu Kampala na amemaliza mwaka huu.
Mbali na hayo lakini pia,mimi huwa nafanya makongamano ya Wanawake kila mwaka na kupitia kongamano hilo nimekuwa nikihamasisha kuwasaidia wanafunzi wa kike katika kuwapelekea vifaa mbalimbali vya kusomea huko katika Sekondari ya Uhuru ikiwemo daftari,Peni ,Soksi,na vitu vingine.
Aidha,mara ya pili tulipeleka tofali 400 Kwa ajili ya kuchangia ujenzi Shule ya Sekondari Disunyara na wakati mwingine wakati wa mitihani mimi mwenyewe huwa napeleka boksi la Peni,Soda na mahitaji mengine.
WEWE NI MWANAMKE,TUELEZE NI CHANGAMOTO GANI UMEZIPITIA KATIKA UCHAGUZI ?
Changamoto katika uchaguzi ni kubwa kwani watu wengi wameninenea vibaya kwakuwa wanapokuona Mwanamke wanasema Malaya na wamekuwa wakisema mimi ni Malaya kwakuwa nimejenga ofisi ya Kitongoji na kuweka vyoo vya Kisasa ndani .
"Nimejenga ofisi nzuri ya kisasa katika Kitongoji changu na naweza kusema katika ofisi za Vitongoji zilizopo katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini ofisi yangu ipo standard (Kiwango cha Juu).
Lakini pamoja na maneno mengi ya kusemwa vibaya wapo watu walikuwa wanaona jinsi ninavyojitoa mpaka nikafanikiwa kujenga ofisi ya Kitongoji .
" Mimi wakati nagombea awamu ya kwanza niliahidi kutafuta eneo la kujenga ofisi na niliposhinda nikapambana kutafuta eneo na nikafanikiwa na awamu ya pili nilivyochaguliwa nikapambana na kufanikiwa kujenga,"amesema Maendaenda
NINI KIPAUMBELE CHAKO BAADA YA KUSHINDA?
Kwakweli nina mambo mengi ya kuwatumikia Wananchi wa Kitongoji cha Janga lakini kwasasa nimeweka kipaumbele cha kuhakikisha nakwenda kujenga uzio wa ofisi.
Ofisi niliyojenga ni nzuri lakini haina uzio jambo ambalo kwasasa inapelekea watu kupitia hovyo na kutumia jengo hilo kama sehemu ya kuweka vijiwe vya kufanya mambo ambayo ni tofauti na malengo ya kuwepo kwa ofisi hiyo.
"Malengo yangu ya sasa ni kuanza na kujenga uzio wa ofisi ambao utaleta heshima ambapo Wananchi watakaokuja kupata huduma wakiwa na magari yatapata sehemu ya kuegesha na hivyo kuleta usalama wa mali na hata kutoa huduma kwa jamii mazingira mazuri zaidi," amesema Maendaenda
Kwasasa watu wanalala maeneo ya ofisini na kamwe siwezi kuwafukuza kwakuwa hiyo ni ofisi yao hivyo kujenga ofisi itakuwa njia sahihi ya kuondokana na baadhi ya changamoto.
UMEJIPANGAJE KUJENGA UZIO WAKATI OFISI HAINA FEDHA?
Hata wakati najenga ofisi Kitongoji hakikuwa na fedha lakini nilitumia njia ya kuandika barua na kupeleka Halmashauri kwa ajili ya kuomba msaada na nilifanikiwa kupata fedha kiasi cha Sh milioni nne kutoka Mfuko wa Jimbo.
Lakini pia katika kukamilisha ujenzi huo na masuala mengine ya kimaendeleo huwa nawashirikisha Wananchi kupitia mkutano wa Kitongoji na hivyo kukubaliana na mara nyingi huwa tunafanyakazi pamoja na mabalozi ndio maana mambo yanaenda vizuri.
Kwahiyo hata katika kujenga uzio huo naamini nitafanikiwa kwa kutumia njia ileile ya kuwashirikisha Wananchi na Mabalozi kupitia mkutano ambao utapendekeza na kuomba msaada katika Halmashauri yangu na ujenzi huo utaanza maramoja.
NINI USHAURI WAKO KWA WANAWAKE WENZIO?
Mimi huwa napenda kuwatia moyo Wanawake kwakuwa wanaweza na hamna tofauti na wanaume lakini kikubwa ni kuhakikisha unachotaka kugombea unakitilia nia na kiwe na wito katika moyo wake .
Ukishatilia nia na ukafanikiwa kushinda ni lazima utafanyakazi kwakuwa vitu vingine unajifunza kupitia wenzio hivyo nawashauri Wanawake wenzangu kutorudi nyuma kwakuwa hakuna aliyezaliwa kuwa kiongozi .
"Mimi huwa nawapigania sana Wanawake wenzangu na mara nyingi huwa nawahamasisha kugombea nafasi za uongozi na katika jitihada zangu nimefanikiwa katika Kata yangu kuhakikisha tunafikia hamsini Kwa hamsini na sasa katika uongozi tupo Wanawake wawili na wanaume wawili.
LIPI NENO LAKO LA MWISHO KWA WANANCHI WA KITONGOJI CHA JANGA?
Ninachoweza kuwaambia Wananchi wangu ni kwamba uchaguzi umepitia na hategemei kuona watu wanalipizana mabaya ila kilichobaki ni kuwatumikia Wananchi na nitawajibika kama walivyonizoea na kama nilivyowazoea.
MWISHO.
Comments
Post a Comment