BENKI YA CRDB YAHAMASISHA SAMIA BOND, YASEMA NI MKOMBOZI KWA WATANZANIA
Na Gustaphu Haule,Pwani
BENKI ya CRDB imewahamasisha Wananchi kuchangamkia fursa ya kufungua akaunti kwa ajili Hatifungani ya Miundombinu ya Samia( Samia Infrastructure Bond) kwakuwa manufaa yake ni makubwa.
Meneja Mwandamizi Kitengo cha Serikali kutoka Benki ya CRDB Faraja Kaziulaya, ametoa hamasa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Mjini Kibaha.
Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Serikali kutoka CRDB Faraja Kaziulaya, akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji yanayoendelea kufanyika Kibaha Mkoani Pwani.
Maonesho hayo yamefunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Selemani Jafo Disemba 17,2024 ambapo wadau mbalimbali wanashiriki ikiwemo Benki ya CRDB.
Akizungumzia kuhusu Samia Infrastructure Bond Kaziulaya amesema kuwa mpango huo unafanyika kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA ) ambapo ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha mpango huo.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Selemani Jafo akipokea maelezo kutoka kwa Meneja Mahusiano kitengo cha Serikali Benki ya CRDB Makao Makuu Ndugu Elia Mapunda, baada ya kutembelea banda hilo leo lililopo katika maonesho ya Viwanda na Biashara Mjini Kibaha.
Amesema lengo la Samia Bond ni kuhakikisha inafanyakazi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara lakini pia inatoa fursa kwa Watanzania kujiwekea akiba kwa ajili malengo maalum.
Kaziulaya, amesema kuwa Samia Bond unaweza kuwekeza kuanzia kiasi cha Sh. 500,000 na mhusika unapata faida ya asilimia 12 kila baada ya miezi mitatu na mwisho mtu anaweza kuchukua kiasi alichowekeza pamoja na riba yake.
Amesema kuwa,anayeweza kuwekeza katika Samia Bond ni watu binafsi , Waajiriwa,Watanzania waishio nje ya nchi ,wanafunzi ,wastaafu na wawekezaji wa pamoja.
Wengine ni vikundi mbalimbali kama vile Vikoba,vikundi vya familia,vikundi vya mitandao ya Jamii kama vile WhatsApp, Taasisi, wajasiriamali wadogo na Kati,Taasisi za Kiserikali , Taasisi binafsi,Mawakala wa Serikali na hata makundi mengine.
Meneja Mwandamizi Kitengo cha Serikali kutoka Benki ya CRDB Faraja Kaziulaya akitoa hamasa Kwa Wananchi kutumia fursa ya kutumia Samia Infrastructure Bond kwenye maonesho ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji yanayofanyika Mjini Kibaha .
"Naomba Watanzania watumie fursa hii muhimu kuwekeza katika Samia Bond kwakuwa ni mpango muhimu ambao unakwenda kuwainua kiuchumi na hata katika kuchangia maendeleo ya Taifa,"amesema Kaziulaya
Kaziulaya ,amesema madhumuni ya Hatifungani ya Miundombinu ya Samia ni hatifungani mahsusi inayotolewa na Benki ya CRDB kushirikiana na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA)kwa ajili kufadhili miradi muhimu ya Miundombinu nchini Tanzania.
Amesema kuwa,miradi hiyo itaongeza mtandao wa usafiri nchini ikilenga kuboresha kwa kiasi kikubwa usafiri wa Vijijini na Mijini ambapo mwekezaji anaweza kutumia tawi lolote la Benki ya CRDB lililopo katika maeneo anayoishi.
Hatahivyo, awali Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Selemani Jafo alitembelea banda la Benki ya CRDB lililopo katika maonesho hayo huku akisifu jitihada zinazofanywa na Benki hiyo kwa ajili ya kusaidia Watanzania.
Mwisho.
Comments
Post a Comment