WAFANYABIASHARA WADOGO DODOMA WAMPONGEZA RAIS SAMIA, WASEMA MACHINGA COMPLEX NI MKOMBOZI WA MAISHA YAO
Na Gustaphu Haule, Tanzania
#KAZIINAONGEA
WAFANYABIASHARA wadogo jijini Dodoma, wameipongeza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuwaondolea umasikini.
Pongezi za wafanyabiashara hao zimekuja mara baada ya Rais Samia kuweka jitihada za kuwatengea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao.
Wafanyabiashara waliompongeza Rais Samia wanatoka katika Soko la Machinga Complex Jijini Dodoma ambao wanasema Rais Samia amewafanya waishi katika maeneo mazuri na salama Kwa biashara zao.
Wamesema kuwa kwa namna alivyowahamisha kutoka barabarani walipokuwa wanafanyia biashara zao na kuwajengea soko maalum maarufu kama Machinga imekuwa ni msaada mkubwa kwao tofauti na awali waliokuwa wanafanya biashara kiholela.
Kaimu mwenyekiti wa Machinga Complex, Lucas Kingamkono, ameishukuru serikali ya Rais Samia huku akisema uwepo wa soko la Machinga limerahisisha ufanyaji wa biashara kwa wafanyabiashara wadogo wa Mjini Dodoma.
Kingamkono ,amesema kuwa awali walikuwa wanafanya biashara katika maeneo ambayo hayakuwa rasmi na hivyo kufanya biashara kwa mashaka.
Nae Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ameupongeza uongozi wa soko kwa kuandaa mkutano wa kusikiliza kero za wafanyabiashara ambapo pamoja na mambo mengine ameahidi kutunisha mfuko wa soko kwa kuchangia Shilingi Milioni 10.
Mavunde ameahidi kusaidia upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara hao kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji na taasisi za fedha na kutumia fursa hiyo kuwataka askari mgambo wa Jiji kuacha kutumia mabavu makubwa kushughulika na wafanyabiashara hao.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaj Jabir Shekimweri ameahidi kusimamia na kushughulikia utatuzi wa kero na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa soko la Machinga Complex ili kuweka mazingira bora ya biashara.

Comments
Post a Comment