TANROADS WAPEWA MWEZI MMOJA UJENZI WA KITUO CHA MAEGESHO CHIMBUYA KUKAMILISHWA




Na Mwandishi wetu
Novemba 19, 2024

📌 Waziri ashuhudia foleni kubwa ya Malori Tunduma

📌 Atoa mwezi mmoja ujenzi wa kituo cha maegesho Chimbuya kukamilishwa 

📌 Aagiza upembuzi kufanyika ili kujenga barabara ya Mchepuo, magari yanapita kwa kupokezana 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuelekeza Wakala ya Barabara (TANROADS) kufunga mizani mitatu inayohamishika (mobile weighbridge) ya kudhibiti uzito wa magari katika eneo la Tunduma ili kuongeza kasi ya upimaji wa magari na kupunguza msongamano wa malori yanayosubiria kwa muda mrefu kupima katika mzani mmoja wa Mpemba unaopima Magari yanayoelekea Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia.

                                       Malori katika mzani eneo la Mpemba, Tunduma Mkoa wa Songwe

Bashungwa ametoa agizo hilo Wilayani Tunduma Mkoani Songwe na kueleza kuwa Serikali inatambua changamoto wanayopitia Wasafarishaji na wananchi katika eneo hilo kutokana na msongamano wa malori wa muda mrefu na kukwamisha matumzi ya barabara kwa watumiaji wengine.

“Kutokana na changamoto za upimaji wa magari eneo la Mpemba nimeelekeza mizani mitatu ije ikae pale mpemba mmoja ukiharibika wanaweka mwingine ili kuondokana na adha hii ya foleni, nimemuelekeza  Meneja wa TANROADS Mkoa Songwe kufikia Jumatano [tarehe 20 Novemba 2024] wafunge mzani wa kuhamishika”, amesisitiza Bashungwa.

Malori yakiwa katika foleni kuelekea katika mzani eneo la Mpemba, Tunduma Mkoa wa Songwe

Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mzani mpya katika eneo la Iboya ili kurahisisha wasafirishaji wanaotoka Zambia kuelekea Mbeya na maeneo mengine ya nchi kupima magari yao bila ya kikwazo chochote.

Aidha, Bashungwa ametoa mwezi mmoja kwa  TANROADS Mkoa Songwe kukamilisha ujenzi wa kituo cha maegesho katika eneo la Chimbuya ili kufikia wiki ya kwanza ya mwezi wa Disemba, maegesho hayo yaanze kutumika kwa kupunguza foleni ya malori kukaa barabarani.

Kituo cha maegesho ya Magari katika eneo la Chimbuya

Kadhalika,  Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour pamoja na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta ndani ya mwezi mmoja kufanya usanifu utakaowezesha kujenga barabara ya michepuo katika maeneo ya milima mitatu ya Mbalizi, Nyoka na Igawa katika barabara ya Mbeya - Tunduma ambapo  magari makubwa na madogo yanapita kwa kupokezana.

Waziri Bashungwa akitoa maelekezo alipofanya ziara ya kikazi Mkoani Songwe


Naye, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameeleza kuwa Mkoa tayari umepata eneo la hekari 1,800 kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Tunduma ili  kupunguza changamoto za foleni ya magari ambapo hivi sasa wanaendelea na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Jimbo la Tunduma, David Silinde amemshukuru Waziri Bashungwa kwa kusikia kilio na kufika kujionea adha ya foleni katika mji wa Tunduma ambapo kwa siku takribani magari makubwa 3,000 yanavuka katika mpaka wa Tanzania na Zambia ambayo ni asilima 72 ya mizigo inayopakuliwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam





Mbunge wa Jimbo la Vwawa, Japhet Hasunga ameiomba Serikali kushughulikia changamoto ya msongamano wa malori katika eneo la Tunduma kwani inasababisha ongezeko la gharama kwa wafanyabiashara na Wasafirishaji kutumia muda mrefu barabarani.

Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA

TANROADS YATOA UFAFANUZI KUTOZWA FAINI GARI LA SIMBA LOGISTICS KITUO CHA MIZANI YA VIGWAZA MKOA WA PWANI